HECHE ANENA MAZITO AKIENDA KUJISALIMISHA POLISI


MBUNGE wa Tarime Vijijini, John Heche ametoa tuhuma nzito kwa viongozi wa Serikali juu ya uwepo wa njama za kumbambikia kesi kama sehemu ya mkakati wa komkomoa baada ya kuibua ufisadi kwenye vitambulisho vya Taifa na passport.



Ndugu zangu,

Nawashukuru wananchi na ndugu mlioguswa na msiba ulionipata.

Napenda kuwatarifu kuwa nipo njiani kurejea Dar es Salaam ili kukabiliana tena na tuhuma ninazobambikiwa.

 Naenda kwa HIARI yangu na bila UOGA wowote, maana MUNGU wetu anajua kuwa sina historia yoyote mbaya ya uhalifu.

Historia yangu ni ya kupigania HAKI tu. Napenda kuwataarifu kuwa nitafikia polisi Dar es Salaam, na hata mahakamani bila shuruti. Nakwenda mwenyewe. Wanaojipanga kunikamata wasipoteze nguvu zao na fedha zetu.

PILI, nina taarifa za kina kuhusu watu wenye hila wanaolenga kutumia vibaya vyombo vya dola kunitungia mashitaka ya kijinga, kwa kunihusianisha na mambo ambayo "wameyachonga" kwa mitandao yao, wakitumia vikundi vya watu waovu, kwa lengo la kunikomoa.

Natambua kuwa hasira zao dhidi yangu zinatokana na *hotuba yangu bungeni kuhusu ufisadi wa e-passport na vitambulisho vya taifa.*

Kwa kuwa nilitaja vigogo katika hotuba yangu, sasa wanajaribu kutumia vyeo vyao kunishughulikia, badala ya kushughulikia ufisadi niliowaonyesha.

Tangu nilipowataja bungeni, ndipo wamejitokeza watu wanaodai kuwa
nilipeleka vijana Ujerumani kwenye mafunzo ya kuumiza watu.


Mara ooh, Heche ni MTU hatari mwenye vikosi, mara wananihusisha na upigaji watu IGUNGA.

Haya yote yanatengenezwa na dola na kutumia wasemaji wasio rasmi kuhalalisha mipango yao dhalimu ambayo iko mezani kwao hawa wanawatuma akina Cyprian Musiba na wamiliki wa kijigazeti - JAMVI LA HABARI.

Wengine wamefika mahali wanadai walikuwa hawanijui, eti wamenijua majuzi baada ya kuniona na kunisikia bungeni - wakasahau kuwa nilikuwa maarufu nchi nzima nikiwa mwenyekiti wa Bavicha, ambaye nilifanya mikutano ya hadhara katika mikoa yote.

Ni kielelezo tu cha njama ambazo wameanza kutunga dhidi yangu baada ya hotuba yangu.

Wote hawa ni askari wa kukodiwa wanaotumwa kufanya njama chafu dhidi ya raia wanaopigania HAKI na UADILIFU.

Nataka wajue kuwa nafahamu mipango yao ya kunibambikia kesi, *lakini nimejipanga, watu wangu wapo tayari,  na MUNGU atasimama nasi kutetea HAKI yetu.*

*John Heche* Mbunge - Tarime Vijijini

0 Comments:

Post a Comment