VIJANA Mashuhuri nchini, mwanamuziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul maarufu Diamond Plutnumz na mwanasoka wa kimataifa, Mbwana Samatta wameteuliwa kutunukiwa tuzo katika tamasha lililoandaliwa na Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) litakalofanyika Dallas nchini Marekani.
Wengine wataopewa tuzo hizo ni pamoja na Dk Steve Meyer ambaye ni daktari bingwa katika Hospitali ya Mercy iliyopo jiji la Sioux, Marekani aliyewatibu manusura wa ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent.
Mratibu wa tamasha hilo, Ben Kazora amevieleza vyombo vya habari kuwa wanampa tuzo daktari huyo kwa kutambua mchango wake katika kuokoa maisha ya watoto hao.
“Sote tunatambua namna ajali ilivyokuwa mbaya na ilivyopoteza wapendwa wetu wengi. Dk Meyer na timu yake walifanya kila njia kuokoa maisha ya watoto wale watatu walionusurika,” amesema na kuongeza ...
“Tunampa Diamond zaidi kwa kutumia kipaji chake cha muziki kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa, vivyo hivyo Samatta kwa kutumia kipaji chake cha kusakata kabumbu kuitangaza Tanzania,”.
Kwa mujibu wa Kazora, mwingine ni mwanariadha John Akhwari ambaye mwaka 1968, alimaliza mbio katika michezo ya Olympic iliyofanyika Mexico City licha ya kuumia mguu.
Naye meya wa Dallas Texas nchini Marekani, Mike Rawlings aliwakaribisha Watanzania hao kushiriki tamasha la Tanzania Day, litakalofanyika jijini humo kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na utalii.

0 Comments:
Post a Comment