MSIBA: Mwili wa Mfanyabiashara Mrema umewasili Arusha kwa maziko..


 MWILI wa mfanyabiashara maarufu anayemiliki mlolongo wa vitega uchumi  jijini hapa, Faustine Mrema, umewasili jijini hapa jana.

Mwili huo umewasili leo mchana na kupokelewa kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na kupelekwa kuhifadhiwa moja kwa moja kwenye hospitali ya Seliani.

Mrema alifariki  dunia siku ya jumapili alfajiri akipatiwa matibabu hospitali ya City Garden kwenye jiji la Johanesburg nchini Afrika Kusini.

Bilionea huyo anatarajiwa kuzikwa Agosti 9, mwaka huu  Ngurdoto eneo alipo hoteli yake ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano.

Baadhi ya wanafamilia na ndugu waliyasema hayo jana kwa nyakati tyofauti wakati wakiongea na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu maeneo ya Uzunguni kata ya Sekei.

Walisema kuwa uhakika wa eneo gani atakalozikwa mfanyabiashara huyo utapatikana mara baada ya kumalizika kwa kikao cha familia kilichotarajiwa kukaa jana jioni.

Mmoja wa wanafamilia ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa  mwili wa marehemu Mrema unatarajiwa kuwasili jijini hapa ukitokea nchini Afrika ya kusini kati ya siku ya  Jumatano au Alhamisi.

Alisema kuna uwezekano mkubwa maziko ya Mrema yakafanyika Ngurdoto katika siku ambayo itapangwa na vikao vya familia kutokana na baadhi ya watu kudai marehemu alikuwa akiwaeleza kuwa akifa anapenda azikwe hapo.


Hata hivyo rafiki wa karibu na marehemu Mrema,  mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Vincet Laswai alisema kuwa kwa  bado hawajajua marehemu atazikwa wapi kwani bado wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha mwili wa marehemu unarejea kwa ajili ya maziko.


“Tuko kwenye mchakato wa kumleta, kwa sasa ni mapema sana kusema lolote kwa sababu kuna process za kufanya ili aweze kufikishwa hapa ajili ya kumzika nadhani mpaka kesho (leo) tunaweza kujua ni lini ataweza kufika na tuweze kupanga siku ya maziko,” alisisitiza mmiliki huyo wa hoteli ya kitalii ya Kibo Palace.

Marehemu alikuwa anamiliki kampuni ya The Impala Group of Hotels inajumuisha hoteli za kitalii za Impala zilizopo mkoani Arusha na Kilimanjaro.

Vitega uchumi vingine ni pamoja na hoteli yenye hadhi ya nyota tano ambayo imekuwa ikitumika kuendesha mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ya Ngurdoto Mountain Lodge iliyopo Arumeru mkoani Arusha.

Pia anamiliki hoteli ya kitalii ya Naura Springs iliyopo Sanawari jijini hapa ambayo viongozi wakuu wa awamu ya nne walienda kuitumia akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Marehemu Mrema ambaye alijikita kwenye biashara za utalii alikuwa akimiliki kampuni ya magari ya kusafirisha abiria ya Impala shuttle Services na kampuni ya uwakala wa Utalii ya The Classic Tours & Travels.

Marehemu Mrema kama mtu aliyekuwa na utaratibu wa aina yake katika utendaji kazi wake ambapo alipenda kutumia muda wa usiku kufanya kazi huku akitumia muda wa mchana kupumzika.


Wale wote waliotaka kukutana naye walilazimika kukutana naye kuanzia majira ya saa tatu usiku kwani ndiyo muda aliokuwa akiingia kazini ambapo alifanya kazi mpaka asubuhi ya siku inayofuata.

Inadaiwa kuwa mwishoni mwa miaka ya 1970 marehemu Mrema aliwahi kukishughulisha na shughuli za kufua na kupasi nguo yaani dobi ambapo alifanyia shughuli hiyo maeneo ya mnara wa saa jijini hapa.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Arusha, Walter Maeda,akiongelea wasifu wa Mrema alisema kuwa alikuwa ni mtu alianza kazi kuanzia chini kabisa lakini kutokana na bidii yake aliweza kukuza mtaji na kufikia hatua ya juu ya kibiashara.

0 Comments:

Post a Comment