EXCLUSIVE: Hali si shwari Loliondo, Wachomewa nyumba zao..


HALI si shwari eneo la Loliondo baada ya kuwepo kwa taarifa za maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba zao zaidi ya 70 kuchomwa moto kwenye kijiji  cha Ololosokwan wilayani Ngorongoro.


Akiongea na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu diwani wa kata ya Ololosokwan, Yannick Ndoinyo alisema kuwa zoezi hilo lililoanza Agosti 14, mwaka huu linaongozwa na polisi wa Longido wakishirikiana na wale wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, (SENAPA) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA).

Alisema kuwa zoezi hilo ambalo mpaka jana bado lilikuwa linaendelea limeleta athari kubwa kwa maelfu ya wananchi kwani wengi baada ya kuchomewa nyumba zao kwa sasa wanaishi nje huku wengine wakikimbilia vijijini vyajirani kutafuta hifadhi


"Hatukupewa taarifa yoyote juu ya kutakiwa kuondoka, polisi wako na askari wa SENAPAna hifadhi ya  Ngorongoro wakifika wanakwambia fanya haraka utoe vitu vyako ukichelewa wanachoma moto," alisema diwaniNdoinyo.


Alipoulizwa endapo zoezi hilo ni utekelezaji wa mapendekezo ya kamati ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo walikubali kupisha ili eneo hilo litumike kama Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori, (WMA).

"Sisi hatujui mapendekezo ya kamati, tume haijawahi kurudi kuongea na wananchi baada ya kupokea mapendekezo yao," alisisitizadiwani Ndoinyo.

Alisema kuwa wanaoendesha zoezi hilo wanadai kuwa wanaondoa mifugo kwenyehifadhi jambo alilodai kuwa halina ukweli kwani hicho kijiji kipo kisheria na wanaishi hapo miaka mingi.

Kwa upande wake Meneja uhusiano wa Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA), Paschal Shelutete alisema kuwa wanaandaa taarifa kamili juu ya suala hilo.

Kaimu Meneja uhusiano wa NCAA, Vicent Mbirikaa, alisema kuwa yuko safarini Kiteto hivyo hajui kwa undani juu ya suala hilo ambapo aliahidi kutolea ufafanuzi leo.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo, alisema kuwa operesheni hiyo haifanyiki Loliondo wilayano Ngorongoro bali wilayani  Serengeti mkoani Mara hivyo atafutwe RPC wa Mkoa huo.

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Bw. Rashid Taka hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani kwa siku nzima ya jana.

Mgogoro katika Pori Tengefu la Loliondo umedumu kwa zaidi ya miaka 25 sasa ambapo mapema mwezi April mwaka huu kamati maalum iliyoundwa na waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilitoa mapendekezo eneo hilo kuwa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) ili litumike kwa ajili ya maslahi yao, maslahi ya wanyamapori pamoja na kulinda vyanzo vingine vya wanyamapori.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ilitoa mapendekezo hayo baada ya kukutana na pande zote zinazokinzana juu ya umiliki wa eneo hilo  eneo hilo la kilometa za mraba 1,500 lenye  vyanzo vya maji, ikolojia ya wanyamapori ikiwemo mazalia na mapito ya wanyama walitangaza kuwa wananchi wameamua kwa pamoja kupendekeza

Pori Tengefu la Loliondo lina ukubwa wa kilometa za mraba 4,000, Wizara ya Maliasili na Utalii ikatenga kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya kuhifadhiwa na nyingine 2,500 zilirudishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

0 Comments:

Post a Comment