HAKIMU Mkazi, Patricia Kisinda amejitoa kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA) baada ya wakili wa Serikali kudai hana imani naye kwa kuwa anafahamiana na mke wa Lema, Neema.
Aidha, mshitakiwa Lema, alishindwa kufika mahakamani hapo kwa kile wakili wake, Sheki Mfinanga alichoeleza kuwa anaumwa na anaendelea na matibabu jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo namba 441 iliyokuwa kwenye mahakama ya Wilaya ya Arusha jana kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali, ilishindikana kuendelea hivyo kuahirishwa mpaka Agosti 2, mwaka huu itakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali baada ya kupangiwa hakimu mwingine.
Hii ni mara ya pili kwa hakimu kujitoa kwenye shauri hilo kwani Mei 29, mwaka huu Hakimu Mkazi, Desderi Kamugisha, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo alijitoa kwa kile alichoeleza kuwa linafanana na shauri lingine la uchochezi linalomkabili mbunge huyo wa Arusha Mjini.
"Kwa kuwa nilikuwa nasikiliza kesi nne za mshitakiwa huyo huyo na aina ya mashitaka hayohayo, naona ni busara nijitoe kwenye shauri hili namba 441 ili faili lirudi kwa hakimu Mfawidhi ili alipangie hakimu mwingine," alisema Hakimu Mkazi Kamugisha.
Kesi nyingine mbili ni za jinai namba 351/ 2016 inayomkabili Lema akidaiwa kuhamasisha maandamano ya ukuta na ile 352/2016 ambayo Lema anashitakiwa pamoja na mke wake, Neema ambazo mawakili wa Lema wamezipeleka Mahakama Kuu wakidai kuwa kuna hoja za kikatiba ambazo haziwezi kujadiliwa kwenye mahakama za chini.
Awali jana wakili wa Serikali, Sabina Silayo alimuomba Hakimu Kisinda ajitoe kusikiliza shauri hilo kwani ana uhusiano wa karibu na mke wa ndoa wa Lema jambo alilodai kuwa wanaona hawatatendewa haki.
Wakili wa Lema, Mfinanga alipinga hoja hiyo kwa kile alichoeleza kuwa hoja hiyo haina mashiko kisheria kwani Watanzania wote ni marafiki na ndugu hivyo akaomba mahakama kutoipa uzito hoja hiyo alichodai kuwa haina msingi hivyo hakuna hana ya hakimu kujitoa.
Baada ya majibishano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote hakimu Kisinda aliahirisha shauri hilo kwa dakika 20 ambapo aliporudi alitoa uamuzi wa kujitoa kwenye shauri hilo.
'Sina mahusiano ya karibu na mshitakiwa ila namjua mke wake hivyo najitoa kwenye shauri hili ili haki ionekane kutendeka," alisema hakimu mkazi, Kitinda.
Katika kesi namba 441/2016 Lema alisomewa mashtaka mawili ya uchochezi ambapo anadaiwa kutoa maneno yenye chuki na yenye kuibua nia ovu kinyume cha sheria ambapo anadaiwa kutenda makosa hayo oktoba 23, mwaka huu
Kosa la kwanza anadaiwa kulitenda Kwenye shule ya sekondari Buraa kata ya Buraa ambapo anadaiwa kusema " kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu elfu mbili na ishirini (2020), haitafika Mungu atakuwa amechukua maisha yake, Rais ana kiburi, rais kila mahali watu wansonewa, wafanyakazi wa serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu wananyanyaswa,".
LEMA APELEKA KESI NYINGINE MAHAKAMA KU
Mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza maelezo ya awali kwenye kesi ya jinai namba 440/2016 ambayo Lema anakabiliwa na shtaka moja la uchochez baada ya wakili wake kusema kuwa wanasubiri maombi yao waliyopeleka Mahakama Kuu juu ya shauri hilo.
Wakili Mfinanga aliyasema hayo mbele ya hakimu Mkazi, Devita Msofe anayesikiliza shauri hilo ingawa hakufafanua ni maombi gani waliyowasilisha kwenye mahakama hiyo ya juu.
Wakili wa Serikali, Alice Mtenga hakuwa na pingamizi juu ya ombi hilo hivyo shauri hilo limeahirishwa mpaka Agosti 2 mwaka huu litakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo oktoba 22, mwaka uliopita Lema akiwa maeneo ya Kambi ya fisi, Ngarenaro jijini hapa kwenye mkutano wa CHADEMA alitoa kauli za uchochezi.
" Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani ipo siku Taifa hili litaingia kwenye umwagaji damu...Rais yeyote ambaye aheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya katiba, Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza," wakili mkuu wa Serikali, Martenus Marando alinukuu maneno yanayodaiwa kuwa ni uchochezi wanayodaiwa kutolewa na Lema

0 Comments:
Post a Comment