Udhibiti wa Mapato kutoka Kodi za Kimataifa Utasaidia Kupunguza Kodi kwa Wafanyakazi Nchini,
Salaam za Kiongozi wa ACT Wazalendo Kwa Wafanyakazi wa Tanzania, Mei Mosi 2017
Ndugu Wafanyakazi
"Leo ni siku yenu katika mwaka. Kama ilivyo kawaida siku hii husherehekewa kwa maadhimisho makubwa ambapo Waajiri (Serikali na Sekta Binafsi) na waajiriwa hutoa hotuba mbalimbali. Wakati mwengine ni siku kama siku nyengine tu za miaka ya nyuma, hotuba, ahadi, kula na kunywa. Hata hivyo Wafanyakazi wa Tanzania wana changamoto nyingi sana na ni vema kutumia siku hii kutafakari Kwa kina changamoto hizi na kutafuta majawabu yake.
Sisi ACT Wazalendo tunaamini katika siasa za Kijamaa, siasa zenye kupigania zaidi maslahi ya wanyonge, Wafanyakazi, Wakulima, Wavuvi na Wakwezi. Katika salaam zangu mwaka huu nawaomba mtafakari hotuba yangu hii niliyotoa Arusha tarehe Machi 25, 2017 na mapendekezo machache ninayoyatoa mwishoni mwa waraka wangu huu kwenu.
Nchini Tanzania Wafanyakazi kwenye sekta rasmi ni milioni 2.1 sawa na 9% tu ya nguvu kazi yote ya Taifa. Hawa wameajiriwa kwenye sekta binafsi (1.4m sawa na 67%) na sekta ya umma (700,000 sawa na 33%). Hawa wanalipwa mishahara na posho mbalimbali kama chanzo cha mapato yao.
91% ya Watanzania wapo kwenye sekta isiyo rasmi na rekodi ya mapato yao yaweza kuwa kizungumkuti kuipata. Hata hivyo tunajua kuwa wengi wameajiajiri wenyewe kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa madini na utoaji huduma.
Ni muhimu kusisitiza kuwa Watanzania wengi hawamo kwenye ajira rasmi au isiyo rasmi. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa Jijini Dar es Salaam kwa mfano ni asilimia 60 tu ya wakazi wake wapo kwenye ama ajira rasmi au ajira isiyo rasmi na asilimia 40 hawana kazi yeyote.
Uchambuzi pekee ambao tunaweza kuufanya kwa sasa ni kwa kutumia vyanzo vya mapato ya serikali ambapo tutaona mchango wa Wafanyakazi kwenye mapato ya Serikali kulingana na vyanzo yake vya mapato.
Kwa mfano, Kitabu cha Mapato ya Serikali Kuu cha mwaka 2016/17 kinaonyesha kuwa Wafanyakazi wote wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi watachangia jumla ya shilingi trilioni 3 kwenye mapato yote ya Serikali kulinganisha na wenye mitaji (waajiri) ambao watachangia jumla ya shilingi bilioni 900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la mitaji na riba (taxes on income/interests, profits and capital gains).
Hata ukitazama miaka miwili ya nyuma utaona kwamba mwaka 2015/16 makampuni yalichangia shilingi 773 bilioni wakati Wafanyakazi walichangia shilingi 2.2 trilioni na mwaka 2014/15 makampuni yalichangia shilingi 600 bilioni na wafanyakazi shilingi 1.9 trilioni kama kodi zao kwenye mapato ya Serikali. Kwa kutumia kigezo cha Kodi za Mapato, matajiri (waajiri) wanachangia robo tu ya mapato yote ya serikali na wafanyakazi wanachangia robo tatu iliyobakia. Hii inachangia sana kuwepo kwa tofauti ya kipato ndani ya jamii.
Kwanini wafanyakazi wanachangia zaidi kuliko wenye mitaji ni swali ambalo tutalieleza. Sababu kubwa ni kuwa wenye Miraji/Mabepari wana fursa ya kukwepa kodi kisheria wakati wafanyakazi hawana uwezo huo. Kodi za wafanyakazi hukatwa moja kwa moja na waajiri kutoka kwenye mishahara yao.
Kwanini Kodi za Makampuni ni kidogo kuliko za Wafanyakazi?
Wafanyakazi wao hukatwa kodi zao kutoka kwenye mishahara yao moja kwa moja ikiwemo pia makato mengine kama michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya. Makato hayo huanzia asilimia 9 kwa mishahara ya ngazi ya chini mpaka asilimia 30 kwa wenye kulipwa mishahara ya juu kabisa. Kwa hiyo kodi ya wafanyakazi ni kodi ambayo serikali ina uhakika nayo moja kwa moja. Kwa takwimu ambazo tumeziona tayari, ni wafanyakazi wa sekta rasmi tu ndio hubeba mzigo wote wa kodi za wafanyakazi hapa nchini. Lakini kwanini kodi zinazotokana na mapato ya makampuni ziwe kidogo kuliko kodi zinazotokana na mapato ya wafanyakazi?
Kwenye makampuni, Kodi ya Mapato ni asilimia 30 ya faida ambayo kampuni imepata. Lakini mapato yanayokusanywa kwenye kodi hii ni kidogo sana kama tulivyoona, shilingi bilioni 900 tu kati ya mapato yote ya serikali mwaka 2016/17 sawa na asilimia nne tu ya mapato yote ya serikali yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali halisi hii sio ya Tanzania peke yake.
Mwanazuoni Thomas Piketty anaeleza kuwa "Ingawa kodi za faida za makampuni ni kati ya asilimia 40 - 50 kwenye nchi za magharibi, mapato kwenye kodi hizi hayazidi asilimia 2.5 - 3 ya Pato la Taifa. Nadharia ya faida inayotozwa kodi ni nyembamba kuliko nadharia ya mapato ghafi ya ziada kwa sababu makampuni huondoa gharama za uchakavu wa mitambo, riba kwa mikopo na hata gharama za bima. Kodi kwenye faida imegubikwa na matundu mengi kwenye mfumo mzima wa kodi duniani" (msisitizo ni wangu).
Matundu haya ndiyo njia za ukwepaji kodi zinazofanywa na makampuni na hasa makampuni ya kimataifa (Multinational Corporations). Nchi za Afrika zimeathirika mno na mfumo wa kodi wa kimataifa na hivyo kupelekea fedha nyingi kutoka Afrika kutoroshwa kwenda ughaibuni. Azimio la Tabora la Chama cha ACT Wazalendo limeeleza kidogo kadhia hii ambayo Serikali za Afrika hazitilii maanani kabisa licha ya taarifa nzuri ya Rais mstaafu Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini.
Katika kitabu cha 'Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans & Capital Flight Bled a Continet' waandishi Leonce Ndikumana na James Boyce, wameonesha kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, jumla ya dola za Kimarekani bilioni 11.4 (wastani wa shilingi trilioni 24) zimetoroshwa kutoka Tanzania kwa njia mbalimbali.
Hizi ni sawa na wastani wa dola za Kimarekani 285 milioni kutoroshwa kila mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi zinatoroshwa na makampuni makubwa ya kigeni yanayofanya biashara na kuwekeza hapa nchin. Africa Progress Panel na kikosi kazi kilichoongozwa na Rais Thabo Mbeki ilieleza kuwa Afrika hupoteza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 50 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha unaofanywa hususan na makampuni haya ya kimataifa.
Inasemekana asilimia 30 ya utajiri wa fedha wa bara la Afrika umewekwa kwenye pepo za kodi (tax havens) kwa mujibu wa kitabu cha 'The Hidden Wealth of Nations' kilichoandikwa na Gabriel Zucman, mhadhiri wa London School of Economics.
Katika kitabu hicho, Zucman ameonyesha takwimu kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi zinazothibitisha kuwa takribani dola za kimarekani bilioni 150 kutoka Afrika zimehifadhiwa kwenye mabenki ya nchi hiyo. Jumla ya Pato la Taifa (GDP) ya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni dola za kimarekani 147.3 bilioni, hivyo fedha za Afrika zilizopo Uswisi ni zaidi ya GDP ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja. Fedha hii ni mara tano ya gharama za kujenga mradi wa Inga Dam kule Kongo ambao ungeweza kuzalisha umeme wa kutosha bara zima la Afrika.
Pamoja na mambo mengine, matundu haya ya ukwepaji kodi yamejengwa ndani ya mfumo wa kodi za kimataifa. Kuna kitu kinaitwa kwa lugha ya kigeni Base Erosion and Profit Shifting ikiwa na maana kuwa makampuni ya kimataifa yanapowekeza hapa nchini huhamisha faida kupeleka nchi zenye viwango vidogo vya kodi na hivyo kutolipa kabisa kodi hapa nchini ama kulipa kodi kiduchu sana.
Kwa mfano, katika kukokotoa kodi kampuni huondoa gharama za riba za mikopo, bima na gharama za utawala na kinachobakia ndio faida ambayo hutozwa kodi. Kampuni hizi huchukua huduma hizi za mikopo, bima na utawala kutoka kwa makampuni dada na kuongeza gharama maradufu na hivyo kuhamisha fedha hizi kana kwamba wanalipia hizi gharama na hivyo kupunguza sana wigo wao wa kodi. Ndio maana siku za nyuma tulisikia kampuni za madini hazilipi kodi ya mapato kwa sababu nyingi zilikuwa zikitumia mtindo huu wa kumomonyoa wigo wa kodi.
Wakati nikiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Madini ya Jaji Mark Bomani tulikuta ushahidi wa kampuni ya Geita Gold Mines ambayo uwiano wa mtaji wake na mikopo (debt-equity ratio) ulikuwa asilimia milioni 12. Hii iliifanya kampuni hii kumomonyoa kila walichokipata katika uchimbaji wa dhahabu nchini kwetu na kukihamishia njia kana kwamba ni malipo ya mikopo waliyochukua kumbe ni mbinu ya kukwepa kodi na kupora dhahabu ya Tanzania. Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, tuliagiza ukaguzi wa ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa na iligundulika kuwa karibia kila sekta ya uchumi ilihusika na ukwepaji kodi.
Mfano ambao huwa naukumbuka mara kwa mara ni mfano wa mauzo yetu ya Korosho kwenda nje. Hupenda kuurudia na nitaurudia tena hapa. Mwaka 2011 Tanzania iliuza Korosho kwa nchi ya India. Kwenye rekodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ilionyesha kuwa tuliuza tani 80,000 za korosho kwa bei ya dola za marekani 1000 kwa kila tani sawa na dola za kimarekani 80 milioni.
Uchunguzi ulionyesha kuwa katika nchi ya India rekodi yao ya Korosho walizonunua kutoka Tanzania ilikuwa ni dola za kimarekani 120 milioni kwa sababu wao walinunua tani 120,000 za korosho kutoka Tanzania. Hii ina maana kuwa tani 40,000 hazikurekodiwa kwenye forodha zetu na hivyo wauzaji kukwepa kodi ya ushuru wa korosho wa zaidi ya dola za kimarekani 12 milioni.
Pia kwenye kodi ya Mapato ya kampuni iliyouza korosho hizi mapato ya zaidi ya dola 40 milioni hayatoonekana na hivyo kufanikiwa kukwepa kodi. Huu ni mfano ninaopenda kuuleza katika kueleza namna mfumo wetu wa kodi ulivyojaa matundu na kuhitaji kufanyiwa kazi kubwa ya kuufumua.
Kwa hiyo makampuni yana njia nyingi za kukwepa kulipa kodi na hivyo wamiliki wake kujilimbikizia mali nyingi na kuongeza tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi. Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tofauti ya kipato itazidi kuongezeka na kuleta hatari kubwa kwa ustawi wa wananchi na usalama wa nchi yetu.
Moja ya suala ambalo chama cha ACT Wazalendo ililieleza na halikuelezwa na chama kingine chochote katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ilikuwa ni hili la kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ili kila anayepaswa kulipa kodi alipe kwa haki na kwa uwazi.
Tuliahidi "kuweka mfumo mpya wa kodi za kimataifa ili kuzuia makampuni ya kimataifa kumomonyoa wigo wa kodi kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za kimataifa za kurekebisha mfumo wa kodi za kimataifa, kupitia mikataba ya kikodi na nchi nyengine ili kuzuia ukwepaji kodi na kujengea uwezo kitengo cha kodi za kimataifa ili kudhibiti ukwepaji kodi".
Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini katika eneo hili?
Serikali ya Awamu ya Tano ilisifika kwa makusanyo makubwa ya kodi katika miezi yake ya mwanzo ya kuongoza nchi yetu. Lakini haijafanya juhudi yeyote ya ndani au ya nje kuhakikisha kuwa nchi inaondoa tofauti kubwa ya kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho. Juhudi hizi za kukusanya kodi hazijaweza kupunguza mzigo Wa kodi kwa wafanyakazi wa Tanzania.
Juhudi za kuendesha kampeni ya kimataifa ili kuboresha mfumo wa kodi za kimataifa zimeshuka chini na kiukweli kama nchi tumerudi nyuma wakati dunia nzima inashiriki kwenye kampeni hizi. Juhudi za ndani za kuongeza makusanyo ya kodi kama hazitatazama mfumo wa kodi za kimataifa, basi hazitakuwa na faida yeyote na tutabakia na kodi za wafanyakazi na vibarua tu tukiwakamua zaidi ili kupata fedha za kuendesha nchi yetu.
Tunapendekeza nini?
1. Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi zinazohusisha makampuni ya kimataifa (MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo wa kodi ( Base Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni hizi. Hili linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba ya kikodi (double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi nyingine duniani.
Tafiti mbalimbali katika eneo hili zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza 5% ya Pato la Taifa kutokana na vitendo vya kampuni kubwa kukwepa kodi kwa kutumia mbinu za kihasibu (tax planning measures). Serikali yetu inapaswa kushirikiana na Serikali nyengine za nchi mbalimbali duniani katika kampeni ya kimataifa ya haki za kodi (International Tax Justice Movement).
Vyama vya Wafanyakazi nchini vinapaswa kuwa mbele kuishinikiza Serikali kushiriki kwenye kampeni hizi na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye sheria zetu za kodi ili kulinda wigo wetu wa kodi.
2. Serikali itazame upya michango ya wafanyakazi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Viwango vya michango Kwa Tanzania vipo juu mno na vinapunguza kipato cha mfanyakazi na kuongeza gharama kwa waajiri. Michango ya Hifadhi ya Jamii ishushwe mpaka jumla ya 12% ya mshahara; kwa Waajiri kuchangia 7% na Wafanyakazi kuchangia 5% ya mishahara yao.
Hii itasaidia kupunguza gharama za kuajiri kwa Waajiri. Vile vile Tozo ya mafunzo SDL ishushwe mpaka 3% . Eneo hili ni muhimu liangaliwe kwa muktadha wa kukuza ajira nchini hivyo ajira zinapoongezeka mapato kwenye maeneo haya yanaongezeka pia.
3. Serikali idhibiti mfumuko wa bei kuhakikisha inapunguza gharama za maisha kwa wafanyakazi. Katika wakati kama huu ambao bei za vyakula zimepanda zaidi ya mara 2 kipato cha wafanyakazi wengi nchini kimebaki palepale, hali hii inaongeza ugumu wa maisha kwao. Ni muhimu Serikali kuchukua hatua mahsusi kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula nchini.
Mwisho, Wafanyakazi wa Tanzania, nawakumbusha kuwa kuna mahusiano chanya kati ya maslahi yenu na aina ya uongozi wa kisiasa uliopo kwenye nchi. Msikae pembeni kwenye harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini. Vyama vya Wafanyakazi vina nguvu zaidi ya kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya kidemokrasia na utawala wa kikatiba nchini."
Nawatakia Mei Mosi Njema.
Salaam za Kiongozi wa ACT Wazalendo Kwa Wafanyakazi wa Tanzania, Mei Mosi 2017
Zitto Kabwe |

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Dar Es salaam.
Mei 1, 2017
0 Comments:
Post a Comment