KIMATAIFA : Jaribio Jipya la Kombora la Korea Kaskazini Limeshindwa

Jeshi la Marekani limesema kombora lililorushwa na Korea Kaskazini leo alfajiri, halikuvuka eneo la mpaka wa nchi hiyo. Kamandi ya Pasifiki imesema kombora hilo lilirushwa kutokea Bukchang kwenye jimbo la South Pyong, majira ya saa 11:30 Alfajiri leo Jumamosi kwa saa za Korea Kusini.

Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap, limemnukuu mkuu wa majeshi ya nchi hiyo akisema kombora hilo lililipuka sekunde chache baada ya kurushwa. Majeshi ya Korea Kusini na Marekani yanakusanya taarifa za kina ikiwemo aina ya kombora hilo.

Korea Kaskazini inapinga vikali mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayoendelea kati ya Korea Kusini na Marekani. Jumanne juma hili, Korea Kaskazini ilifanya kile ilichokiita mazoezi makubwa ya kijeshi yaliyojumuisha vikosi ardhini, majini na vya angani.

0 Comments:

Post a Comment