Chadema wadai polisi wameanza kuandamana, yao jumatatu

>
> WAKAZI wa jiji la Arusha jana walikumbwa na hofu kutokana na polisi
> wengi waliojihami kwa silaha za moto na mabomu kutanda maeneo
> mbalimbali wakiwa kwenye magari, pikipiki na gari la kuwasha.
>
> Aidha, walikuwepo polisi waliokuwa wamevaa kiraia ambao kwa pamoja
> walilenga kudhibiti wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, (UKAWA),
> ambao walipanga kuanza maandamano na migomo isiyo na kikomo kuanzia
> jana kwenye wilaya zote za jiji la Arusha.
> Polisi wengi na gari la kuwasha walikuwa maeneo ya Philips
> yalipotazamiwa kuanza maandamano hayo pamoja na eneo la viwanja vya
> Samunge yalipotazamiwa kumalizikia.
>
> Aidha polisi hao wenye silaha walionekana maeneo mengine wakiwa
> kwenye magari wakizunguka huku wengine wakiwa kwenye magari yao yakiwa
> yameegeshwa maeneo mablimbali ambapo Tanzania Daima iliyashuhudia
> kwenye maeneo ya njia panda ya Nairobi, Mianzini, Sanarawi, Njia panda
> ya Sombetini na barabara kuelekea maeneo Unga Limited.
>
> Baadhi ya wananchi walielezea kushangazwa na hatua hiyo ya polisi
> kutumia nguvu kubwa kuzuia maandamano hayo ya amani yanayolenga
> kutetea fedha zinazoliwa na watu wachache huku wengine wakitaabika kwa
> kukosa huduma za msingi ikiwemo zile za afya.
>
> "Mimi nimekuja asubuhi nimekuta polisi wametanda kila mahali nikauliza
> kuna nini nikaambiwa ni Chadema wanaamana lakini nikashangaa hakuna
> maandamano wala nini nikajiuliza kama yalikuwa maan damano ya amani
> kwa nini polisi wasiwalinde waandamane kama sheria inavyotaka,"
> alisema Abihudi Ulomi.
>
> Akiongelea suala hilo Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas
> alisema ni ya kawaida huku akisema kuwa hakuna mtu aliyekamatwa na
> jeshi hilo kwani hakuna maandamano yaliyofanyika huku akidai kuwa
> ulinzi ni wa kawaida.
>
> Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, mkoani hapa, Amani Golugwa
> alisema kuwa lengo lao la kufikisha ujumbe kwa wananchi limetimia kwa
> polisi kuanza kuandamana kabla ya wao kuanza rasmi jumatatu.
>
> "Kama kuna kitu tulikuwa makini kwenye mikakati yetu ni kuhakikisha
> ujumbe wetu wa kupinga ufujaji wa fedha unaofanywa na Bunge la Katiba
> unafika bila kuvurugwa kwa namna yoyote na hapa niisifu inteligensia
> ya Chadema imefanya kazi yake ipasavyo…
>
> "Tulijizatiti kuhakikisha hakutokei tukio lingine litakalotutoa
> kwenye mstari, hatukutaka kabisa kusikia polisi wameua wananchi au
> wamepiga mabomu ingevuruga kabisa mkakati wetu wa kupinga ufujaji wa
> fedha zinazotokana na kodi zetu unaofanywa na Bunge la Katiba,"
> alisema Golugwa.
>
> Alisema kuwa wakati polisi walipokuwa wakizunguka maeneo mbalimbali
> huku wakifuatilia kwa karibu nyendo za viongozi wa Chadema kulikuwa na
> makundi ya watu waliosambaa maeneo mbalimbali waliokuwa na kazi ya
> kuwaeleza wananchi sababu za polisi kutanda mji mzima ni kuzuia
> maandamano ya amani kupinga ufisadi wa bunge la katiba.
>
> Golugwa ambaye pia ni Katibu wa Chama hicho kanda ya kaskazini alisema
> kuwa kwa kiasi kikubwa polisi wamewafanikishia malengo yao ya kupaza
> sauti kupinga uovu huo kwani kila mwananchi aliyeshitushwa na kuzagaa
> kwa polisi alijua sababu za maandamano.
>
> Kwa upande wake diwani wa Kata ya Levelos, Ephata Nanyaro, (CHADEMA),
> alisema kuwa polisi ni sehemu ya Watanzania ambao kimsingi walipaswa
> kuungana na Chadema kupinga matumizi mabaya ya kodi za umma hivyo
> aliwapongeza kwa kuandamana kabla ya maandamano yao kuanza.
>
> Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), alisema kuwa
> alishangazwa na hatua ya polisi kumfuatilia kuanzia ametoka nyumbani
> kwake majira ya saa tano asubuhi kwa kile alichodai kuwa inteligensia
> ya polisi haiko vizuri kwani walipaswa kubaini hakungekuwa na
> maandamano.
>
> "Polisi wananifuatilia mimi wakidhani mimi ndiyo naandaa maandamano,
> ila tunafurahi kwa sasa polisi haipati mikakati yetu vinginevyo toka
> jana usiku baada ya kikao chetu cha viongozi wangeweza kujua leo
> hakuna maandamano hivyo wasingeanza kuandamana wao….
>
> "Ila niwahakikishie wanahabari kuanzia jumatatu watu wataanza kuingia
> barabarani kwa ajili ya maandamano na kwa namna ambavyo polisi
> wameonyesha udhaifu wao leo hakuna namna wataweza kuzuia nguvu ya
> umma," alisema Lema aliyekuwa amekaa mbele ya magari ya polisi ikiwemo
> lile la maji ya kuwasha maeneo ya Philips.
>
> MWISHO