Naibu waziri wa Nishati na Madini Mh.Steven Masele ametoa tuhuma nzito bungeni akimuhusisha balozi wa Uingereza nchini kwa tuhuma za Rushwa kuhusiana na sakata la IPTL na pia kufanya ujasusi na kudai kuwa balozi anatakiwa kuchukuliwa hatua huku akimtaka akajieleze wizara ya mambo ya nje.
Hizi ni tuhuma nzito kabisa na ujasusi ni kinyume cha sheria za nchi na sheria za kimataifa.Waziri Masele amewatangazia Watanzania na Dunia kuwa Uingereza sio nchi rafiki kwa Tanzania na ni adui mkubwa anayehujumu uchumi wa nchi yetu.
Ni kinyume na kifungu namba 6 cha sheria ya kuzuia Rushwa sura y 329 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 ikisomwa pamoja na aya ya 1 jedwali la kwanza ikisomwa na aya vifungu 57(1) na 60 vyote vya uhujumu uchumi na uhalifu uliopangwa sura ya 200(Iliyofanyiwa Mapitio mwaka 2002).
Mkataba wa kimataifa Vienna unaoshughulikia muhusiano ya kidiplomasia wa Mwaka 1961(Vienna convention on diplomatic relations 1961) katika ibara ya 41(1) unakataza mabalozi na wanadiplomasia kuingilia masuala ya ndani ya nchi wenyeji na pia kutimiza wajibu wa kuheshimu kinga ya kidiplomasia .
Tuhuma za ujasusi na Rushwa ni tuhuma nzito zinazokiuka ibara hii na pia zinavunja sheria za nchi mwenyeji(Host Country) .
Ni makosa ya jinai kujihusisha na utoaji na upokeaji wa Rushwa na mbaya zaidi kufanya ujasusi. Ibara ya 29 ya mkataba huo huo wa Vienna inatoa kinga kwa wanadiplomasia kushotakiwa kwa kesi za kiraia au za jinai(Immune from Civil and Criminal Prosecution) labda kama ibara ya 32 ya mkataba huo huo itatumika kumuondolea kinga.
Anachosema Waziri Masele ni kuwa Balozi wa Uingereza anastahili kufukuzwa nchini kwa kutumia ibara ya 9 ya mkataba huo huo wa Vienna na kumtangaza kuwa ni mtu asiyetakiwa nchini (Persona non grata)? Uingereza ni wahisani wakubwa wa bajeti ya nchi yetu na pia ni wafadhili wa mradi wa umeme vijijini REA ambako wamechangia Paundi 71 Milioni.
Ni lazima ufisadi wa IPTL uwaguse maana Uingereza wanatumia fedha za walipa kodi wao kuifadhili serikali ambako Mafisadi wamekwapua kwa maslahi binafsi. Pia benki ya Standard Chartad ni Benki ya Uingereza na ni wajibu wa Balozi katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kufuatilia kwa karibu sakata hili.Kazi ya Balozi ni kufuatilia na kuhamasisha au kutoa msaada kwa makampuni na wafanyabiashara kutoka nchi yake wanapokua na changamoto bila kuvunja sheria za nchi husika au sheria za kimataifa.
Ni jambo la ajabu kuwa Waziri anatoa tuhuma Bungeni na kumuamuru Balozi akajieleze wizara ya mambo ya nje.Wizara ya Mambo ya nje kupitia mwanadiplomasia mkuu (Top Diplomat) ambaye ni waziri wa Mambo ya Nje ndiye aliyetakiwa kufanya mashauriano na Balozi kuhusu tuhuma hizo na sio kauli za kihuni zinazoweza kuharibu mahusiano ya kihistoria kati ya Uingereza na Tanzania.
Miaka Michache iliyopita Uingereza kupitia shirika la SFO waliweza kuthibitisha nia njema kwa Tanzania katika kulinda raslimali zetu kuliko tunavyoweza kuzilinda wenyewe kwa kupigania na kurudisha mabilioni ya fedha yaliyoibiwa wakati wa ununuzi wa Rada ya Kijeshi,shukrani kwa Bi.Claire Short aliyesimama kidete kuhakikisha Fedha za walipa kodi wa Tanzania maskini zinarudishwa nchini wakati ambao viongozi wetu tuliowachagua walionekana kutokua na moyo wala ari ya kushughulikia Tatizo hilo.
Sasa natoa Rai kwa Waziri wa Mambo ya Nje Mhe.Bernard Membe atoe Msimamo wa Serikali kuhusu tuhuma hizi za kushtua na zinazoweza kuharibu mahusiano ya kihistoria kati ya wananchi wa Tanzania na Uingereza
Imeandikwa na Ben Saanane
0 Comments:
Post a Comment