TAMKO LA CHADEMA KUMSIMAMISHA MWENYEKITI WAKE WA NGORONGORO

 

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO – CHADEMA

MKOA WA ARUSHA

 

TAARIFA KWA UMMA

TAREHE 8 MACHI 2014

 

KUSIMAMISHWA KUTOKA KUWA MWENYEKITI WA CHADEMA WILAYA YA NGORONGORO KUANZIA TAREHE 8 MACHI 2014 NDUGU REVOCATUS WILLIAM PALAPALA

Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa la chama lililoketi tarehe 7 Machi 2014 hapa jijini Arusha ninapenda kuwajulisha wanachama wa CHADEMA wa Wilaya ya Ngorongoro, wakazi wote wa wilaya na Watanzania wote kwa ujumla wapenda mabadiliko ya kweli kuwa ndugu Revocatus William Palapala amesimamishwa kutoka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Ngorongoro kuanzia tarehe 7 Machi 2014.

Uamuzi huu wa kumsimamisha uongozi umechukuliwa na baraza la mkoa ambalo ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa wilaya kwa mujibu katiba ya chama Ibara sehemu ya 6.3.6 (iv) na msingi wa uamuzi ukiwa ni kwa mujibu wa ibara ya 6.5.2 (d) – nyongeza ya 3 ya 5 Aprili 2013 kuwa baraza linaweza kuchukua hatua ya dharura katika kunusuru heshima ya chama na wanachama na hii ni kutokana na tuhuma nzito, mbaya na za aibu zinazoelekezwa juu yake akiwa kiongozi. Aidha kwa tuhuma hizi baraza limemuelekeza ndugu Palapala kwa kumpa fursa nyingine tena sanjari na ile ya awali aliyopewa na kamati tendaji ya wilaya kwa barua ya tarehe 26 Desemba 2013 na nyingine ya tarehe 02 januari 2014, sasa ndani ya siku SABA (7) atatakiwa alete majibu yake yawe sehemu ya utetezi wake kwa nini usifukuzwe uanachama wa CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO.

Aidha tuhuma zinazoelekezwa juu yake ambazo awali aliwahi kukiri mbele ya wajumbe wa kamati tendaji kwenye kikao cha tarehe 2 Januari 2014 na kisha kwa namna ya kushangaza ameendelea kuonyesha kutojali maagizo aliyopewa ya kujibu kwa maandishi ni hizi zifuatazo;

  1. Anatuhumiwa kufanya utapeli, kufoji mkataba na kuandika barua ya uongo ili kummilikisha Bi Esta Warioba eneo ambalo halikuwa mali yake. Bi Esta amekiri (kwa barua ambayo ipo nakala kwa afisa mtendaji wa kijiji cha WASO) kuwa eneo hilo halikuwa lake na kuwa ndugu Palapala alimuandikia barua hiyo ya utapeli jambo ambalo lilipelekea kuchonganisha wananchi, kupotosha ukweli, kuidanganya mahakama na kughushi mkataba.

Kitendo hiki ni kinyume kabisa na katiba ya chama kwenye kanuni za uendeshaji shughuli za chama sura ya 10.1 Maadili ya viongozi, (i) Kila kiongozi anatakiwa kuwa na tabia ambayo ni mfano wa kuigwa na wanachama na jamii kwa ujumla,  sambamba na ibara (vi) kiongozi kujitosheleza kimapato kwa njia  halali na kuepuka tabia ya kukopa kwa kuzidi uwezo ikiwemo na kushiriki tabia za kiudanganyifu ili kujipatia mapato.

2.      Anatuhumiwa kushiriki vitendo vya rushwa baada ya yeye kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati na kisha katibu wa kamati ya kijiji ya kusimamia suala la viwanja katika kijiji cha WASO. Hata baada ya mkutano mkuu wa kijiji wa wananchi wote kuazimia zoezi la kugawa ardhí lisitishwe na hata katika kikao cha ndani ya chama cha kamati tendaji  cha tarehe 15 Februari 2012 kumuonya juu ya tuhuma hizi za rushwa ndugu Palapala alionyesha ubabe na kwa njia zake za pembeni aliendelea na zoezi la kugawa viwanja Jambo hili lilipekea yeye kuandikiwa barua ya terehe 20 Desemba 2013 na afisa mtendaji wa kijiji cha WASO kumtaka kusimamisha matumizi ya ardhí kwenye eneo la Kapongoni ambalo halikuwa limegawiwa kwa njia isiyo ya haki na uwazi na nakala ya barua hiyo ikapelekwa ofisi za TAKUKURU (PCCB) za wilaya na polisi wa kituo cha WASO.

Kitendo hiki ni kinyume kabisa na katiba ya chama kwenye kanuni za uendeshaji shughuli za chama sura ya 10.1 (V) kiongozi hatakiwa kutumia wadhifa wake kujinufaisha yeyé binafsi au ukoo au famila yake, sambamba  na ibara ya 10.2 sifa mahsusi za kiongozi (i) uadilifu na kukubalika katika jamii. Tuhuma hii zimemuondolea mamlaka (moral authority) kwa jamii inayomzunguka kwa vile amekuwa ukifanya jambo hili kwa ubabe bila kutaka kushauriwa hasa ilipokuwa inaonekana kuwa kuna wingu na shutuma ya rushwa dhidi yake kama katibu wa kamati ya kijiji ya suala la ardhí lakini pia akiwa na kofia ya kiongozi wa chama.

  1. Anatuhumiwa kupotosha muongozo wa chama wa usimamizi na utunzaji wa rasilimali za chama kwa kutaka kujimilikisha mali ya chama ili kufanya shughuli zake binafsi. Anatuhumiwa kuwa alipeleka taarifa polisi kusema kuwa pikipiki ya chama imeibiwa na kiongozi mwenzake wa chama huku ukijua fika kuwa pikipiki hii iko kwenye kazi za CHADEMA ni Msingi.

Kitendo hiki cha fedheha ni kinyume kabisa na katiba ya chama kwenye kanuni za uendeshaji shughuli za chama sura ya 10.1 (viii) Ni mwiko kwa kiongozi yoyote kutumia mali za chama kwa maslahi binafsi, sambamba na mwongozo wa usimamizi na utunzaji wa rasilimali  Ibara ya 6 ya “Rasilimali za chama  zitatumika pasipo kuwekewa vikwazo visivyo na sababu na wakati wote viongozi wa chama bila kuathiri wajibu wao wa dhamana wa rasilimali za chama wanatakiwa wawe sababu ya kuona zinatumika kwa manufaa ya chama katika kuwahudumia watu wote”.  Tuhuma hii na vitendo hivi vya aibu ambavyo amekuwa akivifanya mbele ya jamii na viongozi wenzake vimekuwa vikishusha heshima ya yeye kuwa kongozi wa chama kikubwa kinachoaminiwa yaani CHADEMA.

 

4.      Anatuhumiwa kusikika kwa uwazi kabisa akisema mbele ya wananchi na mbele ya baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji (majina ya walio sikia yamethibitishwa) kuwa ameichoka CHADEMA na kuwa anataka kuhama ili awafuate watu anaowaita “maswahiba/Poti” wake, sambamba na hili amekuwa akiwashutumu viongozi mbalimbali wa chama kwa lugha zisizo na staha, za uongo, upotoshaji na uchonganishi.

Kitendo hiki ni kinyume kabisa na katiba ya chama kwenye kanuni za uendeshaji shughuli za chama sura ya 10.1 (iv) kiongozi asijihusishe na vikundi vya ukabila, udini au ukanda kwa makusudi ya kubaguana, sambamba na sehemu ya (xii) marufuku ya kiongozi kukashifu chama, kiongozi au mwanachama. Vitendo hivi havijaonyesha utashi na upenzi wake kwa chama kama ibara ya (iv) katika sura ya 10.(2) kiongozi adhihirishe mapenzi yake na imani yake kwa chama na wanachama na afanye juhudi katika kuendeleza chama na wanachama. 

5.      Anatuhumiwa kushindwa kutimiza wajibu wake kama mwenyekiti wa chama wa wilaya. Ameshindwa kuwa mbunifu katika kufanya kazi ya siasa kwa kuandaa na kutekeleza mikakati na programu za siasa za chama kwenye wilaya, kushindwa kukiendesha chama kwa weledi na hekima badala yake amekuwa akitumia ubabe, kushindwa kusimamia kwa mujibu wa katiba pale inapobidi katika kujaza nafasi za viongozi zilizo wazi, kushindwa kufanya mikutano ya hadhara, kushindwa kukuza chama na kuongeza wanachama, kutoshiriki zoezi ya CHADEMA ni Msingi (amekuwa sababu ya kuzuia zoezi hili) na kushindwa kuandaa mikutano ya mashauriano ya wilaya. Kutimiza wajibu kunategemewa kwa kiongozi kuwajibika katika kujiendeleza na kujielemisha kisiasa kwa kiwango cha kuwajibika kwa umahiri na ufanisi. Sura ya 10.1 sehemu (ii) kutimiza wajibu wa ngazi yako ya uongozi kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za uendeshaji wa chama.

 

Maelekezo na uamuzi huu unaanza mara moja na hivyo ndugu Palapla atatakiwa kukabidhi vifaa vyote vya chama kwa KATIBU WA CHAMA WA WILAYA na KAMATI TENDAJI YA WILAYA mara moja na kuwa kuanzia sasa sio mwakilishi na wala sio msemaji wa chama kwenye jambo lolote lile mpaka shauri lake litakapofikia mwisho wake.

 

 

Imetolewa leo tarehe

8 Machi 2014

Arusha, Tanzania.

 

Amani Golugwa

KATIBU WA MKOA ARUSHA – CHADEMA.

KWA NIABA YA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA.

golugwa@gmail.com

Simu: 0784 343 275

0 Comments:

Post a Comment