WAHANGA WA MABOMU YA ARUSHA WAELEZA MACHUNGU WANAYOPATA

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) janauari 5, mwaka huu kimetoa misaada kwa wahanga wa matukio ya mabomu yanayodaiwa kurushwa na polisi kwenye mikutano mbalimbali ya chama hicho.

Shughuli hizo zilizowakutanisha wahanga 40, viongozi na wanachama wa chama hicho zilifanyika kwenye ofisi za wilaya ya Arusha za chama hicho zilizopo Ngarenaro.
Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Ephata Nanyaro na Katibu wake, Martn Sarungi waliwagawia wahanga hao vitu mbalimbali vilivyotolewa na wanachama na wapenzi wa chama hicho ikiwemo fedha taslim, Sabuni, unga, mchele, matunda na vyakula mbalimbali
Zoezi hilo la kupokea misaada na kuigawa kwa waathirika hao litadumu kwa wiki moja kuanzia januari 4 mpaka 11 mwaka huu ambapo wahanga hao 39 ni kutoka jiji la Arusha huku mmoja akitokea wilayani Arumeru ambaye ni mjane wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo aliyefariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni

Wahanga hao ambao ni wale walipoteza ndugu zao, waliumizwa maeneo mbalimbali ya mwili na hivyo kupata ulemavu wa kudumu siku ya maandamano na mkutano wa chama hicho wa janiari 5, 2011 ambapo polisi waliwauwa kwa risasi watu watatu Juma Ismail, Denis Shirima na mmoja wa Kenya huku wananchi wengine kadhaa kujeruhiwa.
                                      
Wahanga wengine ni wale wa tukio la June 15, mwaka jana ambapo bomu ambalo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alidai lilirushwa na polisi kwenye viwanja vya Soweto wakati akifunga mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne za Arusha ambapo walifariki watu watano akiwemo Katibu wa Chadema Kata ya Sokon1, Judith Mollel  ambapo  wengine kadhaa walijeruhiwa.

Aidha wahanga wengine ni wale waliojeruhiwa Juni 18, mwaka jana wakati walipokusanyika kwenye viwanja vya Soweto kwa lengo la kuagaa miili ya wenzao waliuwawa June 15 ambapo polisi waliwatawanya wananchi hao bila kutoa taarifa ya onyo ya kuwataka kutawanyika ambapo viongozi kadhaa wa chama hicho walikamatwa na kufikishwa polisi lakini hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yao.

WAHANGA WANENA
Rafael Amosi anasema kwa sasa anaishi maisha magumu baada ya kupata ulemavu wa kudumu kwani mkono wake wa kushoto umepinda na haunyooki huku mkono wake wa kulia akiwa hawezi kuuzungusha kutokana na kujeruhiwa vibaya kwenye bega.

Anasema kuwa siku ya juni 18 mwaka jana alikuwa ni miongoni mwa wananchi wa Arusha walijitokeza kwa ajili ya kwenda kuaga miili ya wananchi wanne waliofariki kwa kupigwa mabomu na risasi za moto kwenye mkutano wa kufunga kampeni za Chadema kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne.

Amos anasema akiwa anasikiliza viongozi wa Chadema wakiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na  wabunge  wakiongea alishtushwa na milio ya mabomu ya machozi na maji ya kuwasha yaliyokuwa yanarushwa na polisi ambapo alihamaki na kuanza kukimbia.

“Kabla sijafika mbali nilianguka ambapo kutokana na watu kukimbia hovyo kila mmoja akijaribu kuokoa maisha yake walikuwa wakinikanyaga pale chini nilipokuwa, nilipata maumivu makali mpaka nikapoteza fahamu”

“Nilizinduka nikakuta nimezunukwa na kundi la polisi wenye virungu ambapo nilipokuwa nikijaribu kusimama nilishindwa baadaye nikabaini kuwa nimevunjika mguu wa kushoto kutokana na kukanyagwa na watu, hapo sasa polisi wakaendelea kunishambulia kwa virungu.”

“Huu mkono wa kushoto na bega la kulia vilivunjika wakati nikijitahidi kujikinga virungu vya polisi visinipate usoni kwa kweli nilisikitika sana kwani polisi badala ya kunisaidia wao ndiyo waliniumiza zaidi.” Anaeleza Rafael kwa masikitiko.

Anasema kuwa kwa sasa yeye hana ajira kwani taxi aliyokuwa akiendesha alikua ameajiriwa tu hivyo kutokana na ulemavu alio nao hawezi kufanya kazi hiyo tena. Anaomba msaada wa fedha walau aweze kulipia watoto wake ada ya shule ingawa alisema kuwa bado anaamini mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yatapatikana kupitia Chadema.


Sagida Rajab (30)
Anaongea huku machozi ya uchungu yakitiririka machoni pake, anasema kuwa tukio la juni 15, mwaka jana ni gumu sana kwake kwani limesababisha maisha yake yabadilike kabisa na kuemsababisha sasa awe mjane.
Anasema siku hiyo ilikuwa mbaya kwake kwani alimpoteza mwanaye Fahad Jamal, (7) aliyekuwa darasa la kwanza ambaye alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya kwa risasi huku mwanae mwingine Abuu Adam, (10) akijeruhiwa vibaya hali iliyomsababisha akatwe mguu wake wa kulia hivyo kwa sasa ni ulemavu wa kudumu.
“Mume wangu, Adam Kareem amefariki dunia oktoba 25, mwaka jana kutokana na kuzidiwa na shinikizo la damu. Alikuwa akiwaza sana juu ya tukio hilo lililosababisha kifo cha mtoto wetu na mwingine kuwa mlemavu” anasema Sagida huku akiendelea kulia hali iliyosababisha watu wengine walikuwa wakimsikiliza nao kulia.
 Anaelezea namna watoto wake walivyokumbwa na kadhia hiyo Juni 15, mwaka jana  wakati wakitoka madras ambapo walikuwa wanapita eneo karibu na mzunguko wa magari uliopo karibu na viwanja vya Soweto.

Anasema kuwa watoto wake hao walijeruhiwa vibaya kwa  risasi ambapo Fahad alifariki dunia na Abuu mpaka sasa anendelea na matibabu akiwa amekatwa mguu wake wa kulia alipigwa risasi ikatokea upande wapili.

Sagida anasema kwa sasa hali yake kiafya si nzuri kwani tukio hilo limemchanganya sana akili na anaomba Chadema na  Serikali waangalie namna ya kumsaidia kwani yeye ni mama wa nyumbani alikuwa anamtegemea mume wake ambaye  naye kafariki hivyo anahitaji asaidiwe ili aweze kumhudumia mtoto wake ambaye ni mlemavu kwa sasa.

Ibrahim Rashid (14) mkazi wa Mianzini ambaye wakati wa tukio alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Levelos anasimulia namna alivyojeruhiwa kwa risasi kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika kwenye viwanja vya Soweto, juni 15, mwaka jana.

Anasema mpaka sasa anatembea na risasi iliyopo maeneo karibu na kitovu baada ya madaktari kumueleza kuwa eneo iliyopo ni hatari hivyo inabidi asubiri mpaka ipande juu ndipo arudi hosptali waweze kuitoa.
Anasema kuwa kuna wakati akikaa anapata maumivu makali maeneo karibu na kibofu cha mkojo kutokana na risasi hiyo ambapo risasi nyiongine iliyokuwa kwenye paja aliitoa mwenyewe.
“Hospitali hawakunitoa risasi zote, kuna siku nilikuwa nimevaa suruale laini nikaipandisha mpaka juu kwenye kidonda kilichopo kwenye paja nikaondoa plasta iliyowekwa nikaona kitu kama ganda sikujua ni nini nikamwambia dada.”

“Dada akaniambia nikifute taratibu nikakivuta mpaka kikatoka kumbe ilikuwa ni risasi mpaka leo nimeiweka wala sijaitupa ila kwa sasa naomba nisaidiwe kwenda kuitoa hii iliyopo hapa karibu na kitovu inaniuma sana, baba yangu ni mzee hana fedha.” Anasema mtoto Ibrahim.

“Mimi nilikuwa napita pale kwenye njia karibu na uwanja wa Soweto nikasikia kitu kinaniwasha hapa kwenye paja la kulia nikagusa nikaona damu nikamkimbilia baba mmoja aliyekuwa mbele yangu nikamshika kwa nguvu” anasema mtoto Ibrahim akielezea namna alivyokumbwa na mkasa huo.

“Nikamwambia nakufa huku nikilia nikalala chini, akanifungua suruale akaona jeraha akanibeba akaniweka kwenye gari lake akanikimbiza kwenye hospitali ya dkt Mohamed wakanipa huduma ya kwanza kuzuia damu isitike nyingi wakashauri niwahishwe hospitali ya Mount Meru.”

“Tukaondoka kufika pale watu waliokuwa mapokezi wakasema hakuna huduma wote hawa ni wa Chadema yule baba akanichukua akanipeleka hospitali ya Selian nikapatiwa matibabu” anasema mtoto Ibrahim ambaye aliambatana na mama yake, Buni Rashid, (30).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wilaya hiyo Nanyaro akiongea kabla ya kugawa misaada kwa wahanga hao anadai kuwa mbinu mbalimbali zinazofanywa na watawala  ikiwemo kuwajeruhi na kuwauwa viongozi na wanachama wao kwa mabomu na silaha za moto kwa lengo la  kurududisha nyuma harakati zao za kuwaamsha wananchi kujua haki zao na hazitafanikiwa.

Anasema kuwa mbinu hizo ovu haziwezi kufanikiwa kwa kuwa Chadema wanamtegemea Mungu hivyo wataendelea kushinda jambo alilodai kuwa hata sasa licha ya matukio mengi ambayo wananchi wameuwawa na kuumizwa lakini bado wameshikamana na harakati zinaendelea.
Nanyaro ambaye pia ni diwani wa kata ya Levelos anasisitiza kuwa wataendelea kupigania uhuru wa kweli wa Taifa hili kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao, kodi inayokusanywa inatumika vizuri na nchi inaongozwa kwa misingi ya utawala bora huku uwazi kwenye kila jambo ikiwemo mikataba mikubwa inayohusu rasilimali za umma ikiwekwa wazi kwa wananchi.
“Msingi wa mauaji haya yanayofanywa na vyombo vya dola ni kurudisha nyuma harakati zetu za kupigania wanyonge na kuwaamsha watu kudai haki zao, wanatumia risasi tulizonunua kwa fedha zetu wenyewe kwa kodi  tunazolipa, badala ya kutulinda wanatuua lakini sisi tunawaambia haya wanayoyafanya hatukatishi tama bali yanatuongezea ari ya kupigania kuhakikisha nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora.” Anasisitiza Nanyaro.
MWISHO
Mhanga wa mabomu, Rafael Amaos akionyesha namna mikono yake ilivyolemaa hivyo kushindwa kuinyoosha.
MTOTO Ibrahim
Rashid (14) akionyesha eneo linalomuuma kwa sasa kutokana na risasi ambayo haijatolewa mwilini kwake ambayo iko eneo karibu na kitovu

Sagida Rajab (30) mwenye hijabu akiwa anaelezea namna mtoto wake mmoja alivyofariki na mwingine amekatwa mguu wa kulia walipopigwa risasi wakitoka madrasa hali iliyosababisha mumewe afe kwa shinikizo la damu

0 Comments:

Post a Comment