KANGI ATAKA WATENDAJI MCHWA WAONDOLEWE KWENYE HALMASHAURI

SERIKALI imetakiwa kuchukua hatua madhubuti za kushughulikia tatizo la watendaji wabovu ndani ya Halmashauri hapa nchini vinginevyo hata bajeti ya maendeleo ikiongezwa na kupelekwa kwa wakati haiwezi kuleta tija kwa wananchi.

Hayo yalisemwa jana na mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, (CCM) wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kamati ya kudumu ya bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoendelea na vikao vyake jijini hapa.


Alisema kuwa sababu zinazotolewa na wataalam toka hazina kuwa fedha zinazochelewa kupelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye halmashauri hapa nchini ni zile zinazotolewa na wahisani na washirika wa maendeleo hazina ukweli.

Lugola alisema kuwa kuna uthibitisho hata fedha zinazotolewa na Serikal ambazo hukusanywa Mamalaka ya mapato nchini, (TRA) nazo huchelewa vilevile hivyo akawataka watendaji wa hazina kubadilika kiutendaji.


“Hata mkipeleka fedha zinazotosheleza kwenye hizi halmashauri kama mapendekezo ya bajeti zao yanavyoonyesha, tusitegemee mabadiliko chanya kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi kama tutaendelea kuwa na watumishi wa umma hawa hawa wanaotafuna fedha za umma kama mchwa” alisema Lugola.
Aidha Lugola  aliitaka ofisi ya Hazina itoe maelezo ya kina juu ya utaratibu walioanzisha wa kupeleka mabilioni ya fedha kwenye halmashauri kabla hazijapitishwa na Bunge.

 “Mniambie hapa mnapata wapi madaraka haya ya kupeleka fedha halmashauri bila sisi wabunge kuzipitisha Bungeni kama utararibu wa kisheria unavyotaka?,”alihoji Lugola huku akitolea mfano kiasi cha shilingi shilingi milioni 500 zilizopelekwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Korogwe bila kupitishwa na bunge.

Alisema kuwa baada ya kufuatiliwa fedha hizo zilikutwa zimetumika zote kulipia posho za madiwani na kuendesha uchaguzi jambo alilodai kuwa linadhihirisha kuwa huo ni mwendelezo wa mtandao wa kutafuna fedha za umma.

Kwa upande wake akifanya majumuisho  Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajabu Mbarouk na kusema Hazina inawapasa watoe ufafanuzi, japo wamesahampa taarifa Mkaguzi Mkuu wa  Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kuwa ni vema halmashauri zikapanuliwa uwigo wa kukusanya mapato kwa kukusanya kodi kwenye mabango ya barabarani, matangazo yanayodandikwa kwenye maeneo mbalimbali pamoja na yale yanayochorwa kwenye nyumba sanjari nay ale yatayotangazwa na magari.
 Kwa upande wake,Afisa Usimamizi  wa Fedha Mkuu Hazina Arusha, Charles Mwamwaja, aliomba apewa muda wa kuzifanyia kazi hoja hizo jambo litakalomwezesha kutoa majibu stahili.
Akijibu hoja za Wabunge hao, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kasim Majaliwa alisema kuwa kwa sasa Serikali imejizatiti kushughulikia watendaji wabovu kwenye wizara, mikoa na halmashauri nchini.

Alisema kuwa hata wale waliohusika na kashfa ya kuchakachua fedha za umma kwa kupelekea sh milioni 800 halmashauri ya Mbozi badala ya sh milioni 80 waliyokuwa wameomba ambao nao walizitumia ndani ya miezi miwili tayari wameshachukuliwa hatua ambapo wengine wamesimamishushwa vyeo ili kupisha uchunguzi zaidi wa suala hilo.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa majina yapo ila kwa wakati huo hakuweza kuyataja kwani hayakuwa yote ambapo alisema kuwa idara nzima ya uhasibu kwenye ofisi za TAMISEMI imewajibishwa na aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri alishushwa cheo na kuwa mkuu wa idara pamoja na afisa Elimu naye amewajibishwa.

0 Comments:

Post a Comment