WANAODAIWA KUMUUA MWENYEKITI WA CHADEMA USA RIVER WATOROKA CHINI YA ULINZI WA POLISI


WASHITAKIWA wawili wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, juzi walitoroka wakiwa chini wa ulinzi wa polisi kwenye mahakama ya mkoa wa Arusha.

Washtakiwa hao ni Samweli Mtinange maarufu kama Samu na Mohamed Shabani Limu ambao walitoroka Oktoba 4, mwaka huu  majira ya saa saba na nusu mchana wakati wakitolewa kwenye chumba cha mahabusu mahakamani wakipelekwa kwenye karandinga la polisi kwa ajili kurudishwa rumande kwenye gereza la mkoa, Kisongo.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa kesi hiyo ya mauaji namba 184/2012 ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji aprili 27, mwaka huu majira ya saa tatu usiku eneo Mji Mwema Usa River wilayani Arumeru.

Kutoroka kwa washitakiwa hao kumefanya washitakiwa  wanaoendelea kushikiliwa kuhusiana na mauaji ya Mbwambo ambaye aliuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni  kubaki wanne  wakiwemo wenyeviti wa serikali  vitongoji wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Davis Mkumba ( Kisambaramajengo) na Mathias Nathan( Magadini) ambapo washitakiwa wengine ni Said Florianna  Swalihi na Yohana . 

Sabas  alitumia fursa hiyo kukanusha taarifa kuwa watuhumiwa hao wakati wakitoroka walifanikiwa kumnyang’anya bunduki  mmoja wa askari aliyekuwa akiwalinda kwa kile alichoeleza kuwa watuhumiwa hao wakiwa kwenye harakati za kutoroka walimpiga kikumbo askari huyo ambaye alianguka chini pamoja na silaha yake na wao kupata fursa ya kupita hivyo hakuna bunduki iliyonyang’anywa.

Hata hivyo mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakuwa tayari majina yao kutajwa magazetini walilieleza Tanzania Daima kuwa watuhumiwa hao walimnyang’anya  silaha aina ya SMG mmoja wa askari polisi aliyekuwa akiwalinda jambo lilizua hofu kubwa miongoni mwa baadhi ya watumishi wa mahakamani ambao baadhi waliamua kujifungia ndani ya vyumba vya mahakama wakihofia mahabusu huyo kuwafyatulia risasi.

Mashuhuda hao waliendelea kudai kuwa mmoja wa mahabusu hao alikuwa wa kwanza kutoka kwenye chumba cha mahabusu na alipomkaribia askari huyo ambaye jina wala cheo chake hakijafahamika alimvamia na kumpora silaha hiyo inayodaiwa kuwa na risasi 30 na kuruka uzio mrefu wa mahakama hiyo.

Hata hivyo baadaye polisi walifanikiwa kuipata silaha hiyo ikiwa imetelekezwa kwenye mto Sanawari unaopita pembeni ya mahakama hiyo ambapo taarifa za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa polisi wote waliokuwa kwenye eneo la tukio wanashikiliwa.

Jeshi la polisi limewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa washitakiwa hao ambapo limetangaza zawadi nono ya shilingi milioni tano kwa wananchi watakafanikisha kukamatwa ikiwa ni shilingi milioni 2.5 kwa kila mtuhumiwa.

0 Comments:

Post a Comment