WAKILI mkuu wa serikali, Fredrick Manyanda kwenye kesi inayomkabili wakili maarufu nchini, Mediun Mwale amedaiwa kuidanganya mahakama baada ya kudai kuwa walishasajili notisi ya kukata rufaa kwenye mahakama ya rufaa nchini wakati wakiwa hawajafanya hivyo.
Aidha ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali inadaiwa kukiuka sheria kwa kuiandikia barua Mamlaka ya Mapato Nchini, (TRA) mkoani Arusha kuzuia isitekeleze amri halali ya mahakama iliyowaagiza kumrejeshea Mwale magari yake saba
Hayo yalibainika jana mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Charles Magesa wakati mshitakiwa kwenye shauri hilo la jina namba 330/2011 Wakili Mwale aliyejitetea alipokuwa akijibu hoja zilizowasilishwa na wakili wa Serikali Manyanda akidai kuwa hana imani na hakimu kwa madai kuwa wana mwingiliano wa kikazi na kibinafsi huku akisisitiza umuhimu wa uamuzi mdogo wa mahakama hiyo kutekelezwa.
Wakili Manyanda alidai mahakamani hapo kuwa walisajili notisi hiyo juni 6, mwaka huu lakini hakimu alipomtaka atoe nakala ya notisi hiyo na kuisoma mahakamani hapo ilibainika kuwa notisi hiyo ilisajiliwa juni 7, mwaka huu tofauti na kauli aliyotoa mahakamani hapo siku shauri hilo lilipokuwa mbele ya hakimu huyo juni 6, mwaka huu.
“Notisi hii imeandikwa tarehe 6 juni, mwaka huu na imepekelewa mahakamani juni 7, mwaka huu , mlipokuja mahakamani juni 6 mliieleza mahakama kuwa tayari meshafaili notisi ya kwenda mahakama ya rufaa, kwa hiyo siku ile mlikuwa mnaidanganya mahakama, mlikuwa hamjaileta, kesho yake ndiyo mkaileta” hakimu Magesa alimuuliza wakili wa Serikali ambaye alikuwa akibisha huku akiridia tarehe hizo kama hakimu alivyokuwa akizitaja.
Hakimu Magesa alimtaka wakili Manyanda kujibu hoja kuhusiana na kushindwa kutekeleza uamuzi mdogo uliotolewa na mahakama hiyo wa kutaka mshitakiwa Mwale arejeshewe magari yake saba pamoja na simu za kiganjani baada ya mahakama hiyo kuridhika kuwa vilichukuliwa kinyume cha taratibu na sheria kwa kile alichoeleza kuwa jalada hilo bado halijaitwa mahakama ya rufaa hivyo amri inayosimama ni ile ya mahakama kuu iliyoelekeza jalada hilo lirudishwe mahakama ya hakimu mkazi sanjari na utekelezaji wa amri za mahakama hiyo.
Awali wakili Mwale aliieleza mahakama hiyo kuwa anasikitishwa na hatua ya upande wa serikali kuamua kwa makusudi kuvunja sheria kwa kuamua kuiandikia barua TRA wakiitaka isitekeleze amri ya mahakama wakati tayari juni 12, mwaka huu walikuwa wameshamuandikia barua ya kumwarifu kuwa juni 14, saa 9 alasiri watayakabidhi magari hayo kwa watu waliowapa nguvu kisheria (Power of atorney).
Alisema kuwa alishangazwa siku hiyo watu wake walipofika kwenye ofisi za TRA, walipewa barua nyingine yenye kumbukumbu namba TRA/RM/AR/SMGG/89/VOL.II iliyosainiwa na meneja wa TRA mkoani hapa, E L Kileva ikidai kuwa walisitisha zoezi la kukabidhi magari baada ya kupata barua kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ikitaka zoezi hilo lisitishwe mpaka juni 20, mwaka huu mahakama itakapotoa uamuzi juu ya suala hilo.
“Nchi hii inazingatia utawala bora wa sheria, mwanasheria mkuu wa serikali tunamheshimu sana ni wakili namba moja nchini, tena aliwahi kuwa jaji wa mahakama kuu, siamini kama anahusika kwenye hili, kuna watu wanatumia ofisi yake vibaya, kwani yeye anajua amri ya mahakama hata siku moja haiwezi kuzuiwa kutekelezwa kwa kuandika barua”
“Hata inapotolewa notisi ya rufaa, haisitishi utekelezaji wa hukumu ya mahakama, kwa sasa wenye mamlaka ya kuzuia utekelezaji wa maamuzi madogo ya mahakama ya hakimu mkazi yaliyopata baraka za maamuzi ya mahakama kuu ni majaji wa mahakama ya rufaa pekee ambao mpaka sasa hawajakaa” alisema wakili Mwale huku akirejea maamuzi ya mashauri mbalimbali yanayofanana na suala hilo.
Akijibu hoja iliyotolewa na upande wa serikali ya kumtaka hakimu ajitoe kusikiliza shauri hilo kwa kigezo kuwa yeye amefanya kazi kwa muda mrefu Arusha watakuwa wanamwingiliano wa kimawasiliano kibinafsi na kikazi, Mwale alisema hazina msingi na ina lengo la kuidhalilisha mahakama kwani amefanya kazi kwenye mahakama mbalimbali hapa nchini ikiwemo mahakama kuu ya Moshi, Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na Arusha.
Aidha wakili huyo aliiomba mahakama itoe onyo kwa mawakili wa upande wa Serikali kuacha kuchafua jina lake kwa kutoa taarifa zisizo za kweli kwenye vyombo vya habari huku akitolea mfano wa taarifa zinazoandikwa kwenye magazeti zikidai kuwa alikutwa na shilingi bilioni 28 kwenye akaunti yake.
Alisema kuwa wakati mwingine inaandikwa alikutwa na shilingi bilioni 18 kwenye akaunti yake huku akidai kuwa anatangazwa kuwa wakati alipokamatwa na polisi kwenye gari yake alikutwa na shilingi milioni 10 alizodai ni za matumizi madogo mambo aliyosema kuwa hayana ukweli na yanalengo la kumchafua kwani hakuna kesi hata moja alizofunguliwa kuhusiana na taarifa hizo.
“Kukaa kwangu kimya isiwe sababu ya mimi kuendelea kuchafuliwa, na mheshimiwa hakimu wanafanya hivi makusudi ili kuuonyesha umma kuwa mahakama inanipendelea kwa kuwa nina fedha nyingi, sitapenda jina langu liendelee kuchafuliwa vinginevyo ulete ushahidi au mnishitaki kwa makosa hayo”
Akijibu hoja hizo wakili mkuu wa Serikali Manyanda alisema kuwa hao wanaoandika magazetini wamejiandika na mwandishi wetu labda kama yeye Mwale anaweza kuwajua huku akiendelea kusisitiza kuwa hawakuridhika na mwenendo wa shauri hilo kuanzia mahakama ya hakimu mkazi mpaka mahakama kuu ndiyo maana wakaamua kukata rufaa huku akidai kuwa barua waliyoiandika kwenda TRA ilikuwa ni kwa ajili ya taarifa tu na si kusitisha kutekelezwa kwa amri ya mahakama.
“Kuna barua nyingi zimetolewa hapa mahakamani ni maneno ya mitaani tu….. tena barua hizo hakunakilishwa Mwale lakini tunashangaa yeye kuwa nazo” alisema Manyanda alipokuwa akijaribu kukwepa swali juu ya barua alizowasilisha Mwale akionyesha mawasiliano kati ya upande wa Jamhuri na TRA wakiomba wahifadhi magari hayo hivyo kwenda kinyume na madai ya mawakili wa serikali waliyoiandikia mahakama hiyo kuwa magari hayo yanashikiliwa kwa kukwepa kodi.
0 Comments:
Post a Comment