BENKI YA CRDB KUINGIA BURUNDI



BENKI ya CRDB katika kuhakikisha inaingia ipasavyo kwenye ushindani wa kibiashara ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki imeamua kupanua matandao wake wa kibenki ambapo sasa wanaendelea na taratibu za kufungua matawi ya benki hiyo nchini Burundi.

Wanahisa wa benki hiyo kwa kauli moja waliridhia pendekezo hilo lililotolewa na bodi ya wakurugenzi wa CRDB juzi wakati wa mkutano wao mkuu wa 17 uliofanyika kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano cha Arusha (AICC).


Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Dk Charles Kimei alisema kuwa wamefanya utafiti wa kutosha kabla ya kufikia uamuzi huo kwani wamebaini kuwa nchini Burundi kuna fursa za kibiashara watakazonufaika nazo zinazotokana na ukuaji wa uchumi na kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama nchini humo.


“Kenya  takriban asilimia 25 ya wananchi wake wamefikiwa na na huduma za kibenki ,a Uganda asilimia 12.4 lakini Burundi hakuna ushindani kwani ni asilimiasita tu ya wananchi wake ndiyo imefikiwa na huduma za kibenki hivyo ni rahisi kufanya biashara ukilinganisha na nchi nyingine za jumuiya ya Afrika mashariki”


“Ukienda kuanzisha shamba huku ukiogopa nyoka hauwezi kufanikisha lengo, sisi wachaga hatuogopi, tukienda kufungua mapori tunaingia nyoka wanakimbia wenyewe, ila niwatoe hofu juu ya Burundi, tumechukua bima, ila mna wasiwasi tu wenzetu wameenda Somalia na Sudani ya Kusini wanapigana risasi unakwepa unaendelea kufanya biashara na unapata fedha” alisema 


Dk Kimei wakati akijibu masawali ya wanahisa ambapo majibu hayo yaliwafanya wanahisa hao kuangua vicheko.
Aidha kwenye mkutano huo ulifanyika uchaguzi uliowezesha wanahisa,  Rose Meta kutoka kwenye kundi la wenye hisa zaidi ya asilimia moja na Juma Abdulrahim na Selina Mkony kutoka kundi la wanahisa chini ya asilimia moja kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo.


Awali Dk Kimei akitoa taarifa ya utendaji kwa mwaka 2011 alisema kuwa utoaji wa mikopo uliongezeka kwa asilimia 27 kutoa shilingi bilioni 1,123 za mwaka 2010 mpaka shilingi bilioni 1,429 mwaka 2011 ambapo asilimia 30 ya fedha hizo zilienda kwenye sekta ya kilimo.


Alisema kuwa amana za wateja zilikuwa kwa asilimia 19 kufikia shilingi bilioni 2,409 ukilinganisha shilingi bilioni 2,019 za mwaka 2010 ambapo alisema kwa sasa benki hiyo ina matawi 82, mashine za kutolea fedha zaidi ya 190 na inaushirikiano na taasisi ndogondogo za kifedha 490 hapa nchini.


Dk Kimei alisema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi zilizoikabili dunia lakini mpaka sasa wanaona mwaka 2012 utakuwa ni mafanikio  zaidi ambapo wanatarajia mtaji wao kukua zaidi kwani kwa mwaka 2011 walifanikiwa kuongeza mtaji kufikia  zaidi ya shilingi bilioni 258 kutoka shilingi bilioni 233 kwa mwaka 2010.

0 Comments:

Post a Comment