Happy Lazaro,Arusha .
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahamasisha wananchi na wawekezaji kutumia fursa ya kuanzisha vituo vya mafuta vijijini ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo, kuongeza usalama wa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya pembezoni.
Akizungumza leo katika Maonesho ya Nanenane Njiro ,Meneja wa EWURA kanda ya kaskazini , George Mhina amesema mamlaka hiyo imepunguza masharti ya uwekezaji wa vituo vya mafuta vijijini ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Amesema hatua hiyo inalenga kumaliza tatizo la uuzaji wa mafuta kwenye vidumu na chupa, jambo ambalo linaweka maisha na mali za wananchi katika hatari kutokana na mafuta kuwa kemikali zinazoweza kusababisha majanga endapo zitahifadhiwa au kuuzwa isivyo salama.
Mhina ameongeza kuwa tofauti na vituo vikubwa vya mijini vinavyohitaji mtaji wa zaidi ya Sh milioni 200 hadi 300, uwekezaji wa kituo cha mafuta kijijini unaweza kuanza kwa mtaji wa takribani Sh milioni 40 hadi 50.
"Wananchi wengi zaidi wanaweza kuingia kwenye biashara hiyo huku wakihakikisha mafuta yanayouzwa yanakidhi viwango vya ubora na bei zilizopangwa na EWURA."amesema Mhina .
Amefafanua zaidi kuwa, uwekezaji huo utasaidia pia kukuza shughuli za kilimo, mifugo na biashara nyingine za vijijini kwa kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika, jambo litakalorahisisha usafirishaji na uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
"Mbali na sekta ya mafuta, banda letu katika maonesho ya Nanenane linatoa elimu kuhusu sekta za maji, umeme na usafi wa mazingira."amesema Mhina .
" Wananchi wanapata fursa ya kufahamu miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa na Serikali katika maeneo ya Arusha, Same, Mwanga, Handeni, Korogwe, Tanga na Pangani, inayolenga kuboresha huduma za maji kwa maelfu ya wananchi."amesema Mhina .
Aidha amewataka wananchi kutumia mafundi wa umeme wenye leseni zinazotolewa na EWURA wakati wa kufunga miundombinu ya umeme majumbani au kwenye biashara zao na kuonya kutumia mafundi wasio na sifa kwani kunaweza kusababisha hitilafu za umeme, ajali na hasara kubwa za mali na maisha.
"Nawakaribisha wananchi kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao katika sekta zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazochochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii."amesema Mhina .
"Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi, haki za watumiaji wa huduma za nishati na maji, pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko wanapokumbana na changamoto za huduma."amesema Mhina .
Amesema kuwa ,Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan gesi ya LPG, ili kulinda afya za wananchi na mazingira. Alisema EWURA ina jukumu la kusimamia sekta hiyo na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia viwango na usalama.
Ameongeza kuwa , maandalizi ya michuano ya AFCON inayotarajiwa kufanyika Tanzania yameongeza umuhimu wa matumizi ya nishati safi, ikiwemo kwenye magari na mabasi, ili kuchangia utunzaji wa mazingira na kuendana na viwango vya kimataifa vya usafiri wa kisasa.
"Mbali na kutoa elimu kuhusu nishati safi, EWURA pia inawafundisha wananchi namna ya kutambua na kutetea haki zao wanapopata huduma za maji, umeme na mafuta. Alieleza kuwa wananchi wengi hukumbana na changamoto kama kucheleweshwa kuunganishiwa maji au umeme, bili zisizo sahihi, au kupata mafuta yasiyo na ubora yanayoweza kuharibu vyombo vya usafiri."amesema Mhina .
Mhina amesisitiza kuwa badala ya kuvumilia changamoto hizo, wananchi wanapaswa kufahamu njia sahihi za kuwasilisha malalamiko kwa EWURA ili yapatiwe ufumbuzi kwa wakati. Kwa mujibu wake, mamlaka hiyo imeweka mifumo ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma zote inazosimamia.
"EWURA imewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu matumizi salama ya nishati, haki za watumiaji wa huduma za maji na nishati, pamoja na fursa mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma na maendeleo ya wananchi"amesema .

0 Comments:
Post a Comment