Mahakama Kuu jijini Nairobi imesitisha agizo la serikali la kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya maandamano ya wananchi, na kuamuru vituo vyote vya televisheni vilivyozimwa kurejeshwa hewani mara moja.
Katika uamuzi uliotolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), jaji alieleza kuwa hatua ya serikali ni kinyume cha sheria na inakiuka haki za msingi za kupata taarifa kama zilivyowekwa kwenye Katiba ya Kenya. "Agizo hili ni la kiholela, la ukandamizaji na halina msingi wa kisheria," ilisema LSK kupitia taarifa rasmi.
Serikali ilikuwa imeamuru kuzimwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yaliyoendelea katika miji kadhaa nchini humo, ikieleza kuwa matangazo hayo “yalihatarisha usalama wa taifa.” Maafisa wa polisi walivamia mitambo ya utangazaji ya vituo vya KTN, Citizen TV na NTV vilivyoko Naivasha, na kuizima.
Hata hivyo, vituo hivyo viliendelea kurusha matangazo kupitia majukwaa ya mitandaoni kama YouTube, Facebook na X. Rais wa Chama cha Wahariri, Zubeida Koome, alilaani vikali hatua hiyo na kusema: “Kupokonya wananchi haki ya kufahamishwa ni ukiukaji wa wazi wa Katiba ya Kenya. Wananchi wana haki ya kujua kinachoendelea katika nchi yao."
Maandamano hayo yaliyopewa jina la #GenZRevolution yaliitishwa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Juni 25, 2024, ambapo watu 60 waliuawa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka huo.
Katika maandamano ya leo, taarifa ya pamoja kutoka kwa Chama cha Madaktari wa Kenya, Chama cha Wanasheria wa Kenya na Kikosi Kazi cha Marekebisho ya Polisi imesema kuwa watu wanane wameuawa na zaidi ya 400 kujeruhiwa. “Wanane kati yao walikuwa na majeraha ya risasi. Wengine 83 walihitaji matibabu maalum,” ilisema taarifa hiyo.
Rais wa Chama cha Madaktari, Dkt. Simon Kigondi, alithibitisha kuwa majeruhi wengi walikuwa na majeraha mabaya, yakiwemo ya risasi kichwani. “Tumehudumia watu waliokuwa wanavuja damu kichwani kutokana na majeraha ya risasi. Wengine walikuwa na majeraha ya kuvunjika viungo,” alisema Dkt. Kigondi. Wagonjwa walihamishwa hadi Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta kwa matibabu zaidi.
Katika mji wa Matuu, watu wawili waliripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi. Ripoti kutoka kwa kituo cha televisheni kilichoruhusiwa kurusha matangazo kwa muda mfupi zilithibitisha tukio hilo.
Pia, afisa wa polisi wa kike alijeruhiwa baada ya kushambuliwa na kundi la waandamanaji. Inaripotiwa kuwa alikuwa miongoni mwa maafisa waliokuwa na bunduki za kurusha mabomu ya machozi. Waandamanaji wengine walimsaidia na kumkimbiza kwa matibabu. Baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Katika miji ya Nairobi, Eldoret, Nyeri, Nakuru, Mombasa na Kisii, shughuli za kawaida zilisitishwa huku barabara zikifungwa kwa vizuizi, na magurudumu kuchomwa moto. Umma wa waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana, walitembea kwa mshikamano wakidai haki zao, mageuzi serikalini na kukomeshwa kwa ukatili wa polisi.
LSK imeitaka serikali kuheshimu maamuzi ya mahakama na kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinaendelea kutekeleza jukumu lao la kikatiba bila hofu wala masharti. Katika maneno yao: “Vyombo vya habari si adui wa serikali, bali ni mhimili muhimu katika kulinda na kukuza demokrasia.”
Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea nchini, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamewataka raia kuwa waangalifu na kuzingatia usalama wao. “Tunawaomba wale ambao bado wako mitaani wawe waangalifu ili kuepusha maafa na majeruhi zaidi,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya pamoja.
Kwa sasa, macho ya taifa na jumuiya ya kimataifa yanaelekezwa Kenya, ambapo kizazi kipya cha vijana kinaendelea kushinikiza mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi – kwa sauti moja, kupitia maandamano na mitandao ya kijamii.






0 Comments:
Post a Comment