Kesi ya madai iliyofunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Zanzibar, ikipinga kile kinachodaiwa kuwa ni ubaguzi na kutengwa kwa upande wa visiwani katika shughuli za chama hicho, imeahirishwa na sasa imepangwa kusikilizwa Julai 10, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya Jaji Hamidu Mwanga, lakini ilishindikana baada ya Mahakama kutoa taarifa kuwa Jaji huyo hayupo kwa sababu anasikiliza kesi nyingine katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara. Kutokana na hali hiyo, Msajili Aziza Mbage aliiahirisha kesi hiyo hadi tarehe mpya.
Wajumbe waliowasilisha kesi hiyo ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis, na Maulida Anna Komu.
Mnamo Juni 10, 2025, Mahakama hiyo ilikubali ombi la zuio la muda lililowasilishwa na wajumbe hao, ikiizuia CHADEMA kufanya shughuli zozote za kichama hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Pamoja na hilo, Mahakama imeagiza kuwa mali zote za chama hicho, zisitumike kwa kipindi chote cha zuio hilo, hadi pale uamuzi wa mwisho wa kesi hiyo utakapotolewa.
Kesi hiyo inazidi kufuatiliwa kwa karibu na wadau wa siasa nchini, hasa kutokana na madai ya kuwepo kwa mgawanyiko wa kiuendeshaji ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

0 Comments:
Post a Comment