Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imekiamuru Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi ndani ya siku 21 kuanzia Aprili 18, 2025, katika kesi ya mgawanyo wa mali na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Amri hiyo imetolewa na Jaji Hamidu Mwanga wakati wa kutajwa kwa mara ya kwanza kwa kesi ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, iliyofunguliwa na baadhi ya wanachama wa CHADEMA dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho (mdaiwa wa kwanza) na Katibu Mkuu wa CHADEMA (mdaiwa wa pili).
Katika kesi hiyo, walalamikaji ni Said Issa Mohamed, anayejiwasilisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA, pamoja na Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha kama wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Wakili wa CHADEMA, Jeston Justine kwa kushirikiana na John Chogomo, waliiomba Mahakama wapewe muda wa siku 21 kuandaa na kuwasilisha utetezi wao. Ombi hilo halikupingwa na wakili wa walalamikaji, Shaban Marijani, hali iliyomfanya Jaji Mwanga kuliridhia.
"Maombi yamekubaliwa. Mnapewa siku 21 kuanzia leo kuwasilisha utetezi wenu. Mnatakiwa kuwasilisha mahakamani kabla ya Mei 21, 2025," amesema Jaji Mwanga.
Ameongeza kuwa kesi hiyo itatajwa tena Mei 12, 2025, kwa ajili ya kuangalia kama upande wa wadaiwa umezingatia maelekezo ya Mahakama.
Katika madai yao, walalamikaji wanaiomba Mahakama itamke kwamba uongozi wa CHADEMA umekiuka sheria za vyama vya siasa pamoja na Katiba ya chama. Wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio wa haki wa mali na rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na kuwepo kwa ubaguzi wa kidini na kijinsia.
"Tunaiomba Mahakama itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili," amesema Said Issa Mohamed kwa niaba ya walalamikaji.
Aidha, walalamikaji wanaiomba Mahakama itoe zuio la muda dhidi ya shughuli zote za kisiasa za chama hicho hadi pale maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa kikamilifu. Pia wanataka zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hicho hadi uongozi wa CHADEMA utakapotekeleza matakwa ya kisheria.
Kesi hiyo inaendelea kufuatiliwa kwa karibu huku ikielezwa kuwa inaweza kuwa na athari kubwa kwa uendeshaji wa shughuli za CHADEMA, hususan katika maeneo ya muungano.

0 Comments:
Post a Comment