ACT Wazalendo: Tumeamua Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Mapambano Yanaendelea!

 

“ACT Wazalendo tutautumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama jukwaa la kuitetea na kuilinda demokrasia yetu. Ni vizuri niseme hapa kuwa tumejiandaa kwa hili. CCM ijue kuwa tutaikabili vile itakavyokuja. Tupo tayari kuwaongoza Watanzania kupitia vuguvugu la wananchi kutetea thamani ya kura ili kulinda msingi wa katiba yetu kuwa madaraka yote yanatoka kwa wananchi. Tupo tayari kwa mapambano.”



Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, akitangaza rasmi kuwa chama hicho kitashiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025. 


Akizungumza mbele ya wanachama, viongozi na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Dorothy alisema chama hicho kimeamua kuchukua wajibu wa kihistoria katika mapambano ya kidemokrasia.

Maamuzi ya Kamati ya Uongozi

Dorothy alieleza kuwa Halmashauri Kuu ya Chama ilikutana tarehe 23 Februari 2024 na kuwasilisha maazimio tarehe 24 Februari 2025, yakiacha uamuzi wa ushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu kwa Kamati ya Uongozi ya Taifa.

"Naomba kuwajulisha kuwa baada ya tafakuri ya kina, Kamati ya Uongozi ya Taifa imeamua kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 kwa nafasi zote; Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani," alisema.

Sababu za Ushiriki

Alisisitiza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya uchambuzi wa kina wa hali ya kisiasa nchini na uzoefu kutoka nchi mbalimbali duniani zenye mazingira kama ya Tanzania. "Tunashiriki uchaguzi kutoa jukwaa kwa wananchi kupigania ukombozi wao kiuchumi, kijamii na kisiasa. Tunaenda kutoa jukwaa kwa wananchi KUIKATAA CCM!" alisisitiza Dorothy.

Aliongeza kuwa chama kinashiriki uchaguzi kwa ajili ya vijana wasio na ajira, wakulima, wafanyakazi, na wananchi wote waliokandamizwa na kunyonywa. “Tunashiriki kupigania Taifa la wote, Maslahi ya wote,” alisema.

Mapambano Dhidi ya Ubadhirifu na Uzembe

Dorothy alikemea vikali hali ya ubadhirifu na uzembe serikalini ambao umesababisha kupotea kwa fedha ambazo zingeweza kuboresha huduma za maji, afya, elimu, miundombinu na kuleta ajira. “Hizi ni fedha ambazo zingeweza kuboresha maisha ya Watanzania, lakini zimepotea kwa tamaa na kutowajibika,” alieleza.

Operesheni Linda Demokrasia

Katika kuhitimisha hotuba yake, Dorothy alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kupigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi hadi dakika ya mwisho. “Tunashiriki tukipambana na tunapambana tukishiriki! Mimi Kiongozi wa Chama nipo tayari kuongoza mapambano hayo! Viongozi wenzangu pia wapo tayari kulipa gharama za mapambano hayo,” alisema.

Kupitia Operesheni Linda Demokrasia, chama hicho kinalenga kuunganisha nguvu za wananchi kuitetea na kuilinda demokrasia ya nchi.

“Wito wangu kwa Watanzania wote: tusichoke wala kukata tamaa katika kuipigania demokrasia yetu. Hakuna kurudi nyuma, mapambano yanaendelea!” Dorothy alihitimisha kwa msisitizo.

0 Comments:

Post a Comment