Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu, ametangaza rasmi azma yake ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.
Nafasi inayoshikiliwa na Freeman Mbowe kwa miaka 20 huku wanachama wakimpa jina la Mwamba kwa namna alivyokabiliana na misukosuko mbalimbali katika kipindi hicho.
Lissu alitangaza uamuzi huo leo Desemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam huku akitoa mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko kwa lengo la kuimarisha chama na kukabiliana na changamoto za kisiasa za sasa.
Akizungumza wakati wa kutangaza azma yake, Lissu alisema:
"Nafasi ya uongozi wa chama hiki, hasa katika kipindi hiki kigumu cha siasa, inahitaji kiongozi mwenye mawazo na fikra mpya, ubunifu, uwajibikaji, na uadilifu. Nimeamua kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa kwa sababu ninaamini nina sifa na uwezo wa kuleta mabadiliko muhimu ndani ya chama."
Kuhusu Fedha na Rasilimali
Lissu alipendekeza mfumo wa usimamizi wa fedha wa chama ubadilishwe ili rasilimali zifike moja kwa moja katika ngazi za chini.
"Utaratibu wa sasa wa kupeleka fedha kupitia Makao Makuu na kisha kuzisambaza ngazi za chini unaleta urasimu na usumbufu usio wa lazima. Tunahitaji mfumo unaowezesha fedha kufika moja kwa moja kwenye akaunti za Kanda, Mikoa, Wilaya, na Majimbo kwa wakati," alisema.
Sekretarieti Mpya na Zenye Utaalamu
Lissu alisisitiza kuwa chama kinapaswa kuimarisha sekretarieti zake kwa kuongeza idadi ya wataalamu na weledi katika masuala ya kisiasa na utendaji.
"Chama chetu kinapitia kipindi kigumu cha mapambano ya kidemokrasia dhidi ya utawala wa kiimla.
Hili linahitaji sekretarieti imara, kutoka Makao Makuu hadi ngazi za chini, zenye uwezo wa kushughulikia changamoto za kisiasa za sasa," alisema.
Uongozi wa Mawazo Mapya
Aliongeza kuwa chama kinapaswa kuwa na uongozi wa kisasa unaozingatia mahitaji ya sasa ya wanachama wake na nchi kwa ujumla.
"Katiba yetu inasisitiza kuwa kiongozi wa chama anatakiwa kuwa na uzoefu wa uongozi, kipaji cha ubunifu, na uadilifu. Viongozi wa sasa wanapaswa kuwa mfano wa mabadiliko tunayoyapigania," alisisitiza.
Kutoa Heshima kwa Freeman Mbowe
Lissu hakusahau kumpongeza Freeman Mbowe kwa uongozi wake wa muda mrefu, akisema:
"Mwenyekiti wetu amelifanyia taifa na chama chetu kazi kubwa kwa zaidi ya miongo miwili. Hata hivyo, sasa ni wakati wa mawazo mapya ili kuendeleza kazi aliyoifanya na kukabiliana na changamoto mpya za kisiasa."
Akihitimisha, Lissu alisema kwamba azma yake ni kuhakikisha CHADEMA inabaki kuwa kiongozi wa mageuzi ya kidemokrasia nchini.
Kwa uzoefu wangu wa kisiasa, kitaaluma, na historia ya utumishi ndani ya chama, nina uhakika wa kuleta mabadiliko tunayoyahitaji. Nakaribisha wanachama kuyajadili mapendekezo yangu na kutoa mawazo yao kwa manufaa ya chama,"* alisema Lissu.
Hatua ya Lissu kugombea nafasi hiyo inaashiria mwanzo wa mchuano mkali ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya kitaifa.
0 Comments:
Post a Comment