SAMIA AMLILIA LOWASSA, ATANGAZA MAOMBOLEZO SIKU TANO

SAMIA AMLILIA LOWASSA, ATANGAZA MAOMBOLEZO SIKU TANO



Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku tano (5) za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo Februari 10, 2024 kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Aliyejiuzulu, Edward Lowassa kilichotokea leo.


"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu.

Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito.

Katika mawasiliano yangu na familia, nimewaeleza kuwa kama taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21." Ameandika Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mtandao wake wa X

Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina.

 https://x.com/SuluhuSamia/status/1756303567286100298?s=20

0 Comments:

Post a Comment