MAHAKAMA, TAKUKURU KUFANYIA KAZI RIPOTI YA REPOA JUU YA HALI YA RUSHWA KWENYE MUHIMILI HUO

MAHAKAMA, TAKUKURU KUFANYIA KAZI RIPOTI YA REPOA JUU YA HALI YA RUSHWA KWENYE MUHIMILI HUO






JAJI Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,  Prof. Ibrahim Hamis Juma amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji wa haki na utendaji kazi katika Mahakama za Tanzania. 

Aidha, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini, (TAKUKURU) zimekubaliana zifanye utafiti wa pamoja kuhusu hali ya rushwa katika huduma za Mahakama hapa nchini.




Ameyasema hayo leo Februari 29,2024 jijini Arusha wakati akifungua mafunzo maalumu ya kuwaandaa na kuwajengea uwezo Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu, kuwa wakufunzi wa kutoa elimu  kwenye kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa mkoa na wilaya.

Amesema kuwa wamechukua uamuzi huo kutokana na taarifa ya matokeo ya  kitafiti ya Mwaka 2023 ya taasisi isiyo ya Kiserikali inayoshughulikia Kupunguza Umasikini (REPOA) kuhusu wananchi kuridhika au kutoridhia na huduma za Mahakama. 

"Wote tunajua kuwa suala la ukiukaji wa maadili katika Mahakama za chini limekuwa likitajwa tajwa. Taarifa ya REPOA ya 2023, iliuasa Mhimili wa Mahakama ujielekeze na kuchukua tahadhari kuhusu rushwa katika ngazi za Mahakama za Mahakimu," amesema Jaji Mkuu Prof Ibrahim na kuongeza

"Ngazi za Mahakama za Mahakimu zipo chini ya uangalizi wenu, usimamizi wenu na ulezi wenu. Katika sehemu ya ufupisho wa Taarifa yake katika eneo lililotathmini uwazi, Taarifa ya REPOA ilieleza kuwa ingawa kiwango cha rushwa dhania kimepungua kwa ulinganifu na tathmini za 2015 na 2019,'.


" Lakini watumiaji huduma za Mahakama walisema kuwa Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi bado zina changamoto ya rushwa dhania, hivyo panahitaji kutafutiwa ufumbuzi
Ili kutekeleza tathmini iliyofanywa na REPOA (2023),".

Jaji Mkuu amesema kuwa anaamini Majaji Wafawidhi hao watatoa ushirikiano wa kutosha kwa sababu matokeo ya utafiti huo wa pamoja utawasaidia Majaji hao  kutoa mafunzoi na kuziba mianya na viashiria vya uvunjifu wa Maadili.

"Mafunzo haya ya Majaji Wafawidhi kama Wakufunzi ni jitihada za Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama kuonyesha imedhamiria kwa dhati kabisa kulisimamia kwa uzito unaostahili suala la maadili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inachukua hatua mbalimbali za uwajibikaji kwa Maafisa Mahakama wanaotuhumiwa kukiuka maadili, wakiwemo wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa," amesema Jaji Mkuu na kuongeza.



"Majaji Wafawidhi kama Viongozi, ni wasimamizi wa
maadili ya wadau. Uadilifu wa majaji, wasajili, mahakimu na maafisa wa mahakama hautoshi kama wadau katika mnyororo wa Haki sio waadilifu.
   
"Kama walivyo Majaji, Wasajili, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama, wapelelezi, waendesha mashtaka, mawakili wa Serikali, mawakili wa Kujitegemea, madalali wa Mahakama, na wasambaza nyaraka wa mahakama, wanashikilia nafasi zenye mamlaka makubwa kuhusu uhuru binafsi wa watu, mali za watu na Maisha ya watu.


"Wadau hawa, wote wanatakiwa kuwa na sifa ya ueledi, uwajibikaji, kuaminika, na kutegemewa kuwa watatenda haki wenye uadilifu usiotia shaka.Wadau hawa wa Mahakama wakikosa uadilifu, ni Mahakama ndiyo itakayolaumiwa kwa kukosa uadilifu na kuyumbisha mizania ya haki.

AONYA WENYE KESI ZINAZOENDELEA MAHAKAMA KUTAKA MIHIMILI MINGINE KUINGILIA

Hata hivyo  Jaji Mkuu Prof Ibrahim amesema wadaawa, na watumiaji wa huduma za Mahakama lazima nao wawe waadilifu.


"Uadilifu wa Mahakimu, Wasajili, Majaji hauwezi kufikia asilimia 99 tunayotafuta, endapo wadaawa na wananchi katika mnyororo wa Haki uadilifu wao utakuwa ni pungufu," amesema Jaji Mkuu Prof Ibrahim na kuongeza.

"Kwa mfano mdaawa ana kesi inaendelea Mahakamani au anayo nafasi ya kukata rufani lakini ataandika barua kwa Mhe. Rais, Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi. Kwamba “waingilie kati”. Maombi ya aina hii hatarishi kwa uhuru wa Mahakama.



Naye , Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo ya siku mbili kwa washiriki hao kuwa yamelenga la kuwajengea uwezo wa kuwa wakufunzi katika masuala ya maadili, na hivyo kuweza kutekeleza vyema jukumu la kuwafundisha wajumbe wa kamati hizo.

Aidha, ameeleza kwamba suala la uadilifu kwa majaji ni jambo muhimu sana na linahitaji kuzingatiwa kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi unazingatiwa pande zote mbili.



Kwa upande wake,  mshiriki wa mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Juliana Masabo, amesema kuwa anaamini mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kuwa wawezeshaji bora katika kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali katika kamati za maadili za maafisa mahakama za mkoa na wilaya.

0 Comments:

Post a Comment