Ngorongoro wamjibu Matinyi , wanawake wamuomba Rais Samia akawasikilize




SIKU chache baada ya Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi kueleza kuwa serikali inatoa huduma zote kwa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro, wananchi hao wamekanusha taarifa hiyo wakidai haina ukweli kwani serikali imesitisha kupelekea fedha za miradi ya maendeleo tokea 2021 na fedha zote zimehamishiwa Msomera wilayani Handeni.


Aidha wamedai kuwa hali hiyo imesababisha ukosefu wa huduma za afya hali iliyopelekea kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa surua kutokana na watoto kukosa chanjo huku wakisema kuwa tarafa hiyo haina kituo cha afya hata kimoja bali kuna zahanati ambazo hazina vifaa tiba hivyo zinatoa huduma duni.


Pia wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kufika kwenye eneo hilo ili ajionee hali halisi kuwa hawafi kwa kuliwa na wanyama wakali bali wanawake na watoto wanateseka na kufa kwa kukosa huduma za afya.


Taarifa hiyo wananchi hao  imetolewa leo Desemba 22,2023 jijini Arusha na viongozi wa baraza la wafugaji Ngorongoro,  baadhi ya madiwani na wenyeviti wa vijiji  wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ,(CCM) wakiwa wameambata na wananchi kadhaa ambapo kwa pamoja walisema kuwa huo ni msimamo wa wananchi wote wa tarafa ya Ngorongoro.


Akisoma taarifa hiyo, Katibu wa Baraza la Wafugaji, James Moringe amesema kuwa wanahuzunishwa na kauli ya msemaji wa serikali kutangaza kuwa Ngorongoro ni eneo hatari kuishi binadamu huku akijua si kweli kwani ndiyo eneo pekee duniani ambako binadamu na wanyama wanaishi kwa amani bila kudhuriana.

"Migogoro ya binadamu na wanyama haijawahi kuwa tishio tangu kuanzishwa kwa hifadhi ya Ngorongoro ukilinganisha na vifo vya Watanzania wengi wanaofariki mijini kwa ajali za pikipiki ukiachilia vyombo vingine vya moto," alisema Moringe.
 

Desemba 15, mwaka huu Msemaji wa Serikali, Matinyi aliongea na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza kuwa tarafa ya Ngorongoro ina vituo vya afya vinne , zahanati tisa, hospitali moja huduma za umeme, maji, barabara zinapatikana katika vijiji vyote huku kukiwa na ghala la chakula na chakula cha bei nafuu kinapatikana kama kawaida.

"Hakuna kituo cha afya chochote tarafa ya Ngorongoro, baada ya kuhamishwa milioni 500 kutoka zahanati ya Nainokanoka zikapelekwa Msomera  kumalizia majengo muhimu na kuondoa vifaa tiba katika kituo cha Osinoni na kunyima fungu la uendeshaji kiasi cha shilingi milioni 500 iliyokuwa ikitolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa hospitali ya Endulen sanjari na kuzuia huduma ya dharura iliyokuwa ikitolewa na jimbo katoliki kupitia shirika la FMS," alisema Moringe.

Moringe ambaye pia ni diwani wa Laitole alisema kuwa alisema kuwa kwa miaka mitatu hakuna fedha za miradi ya maji zilizotengwa na serikali kwa ajili ya tarafa ya Ngorongoro ambapo fedha zinazotengwa huelekezwa tarafa za Loliondo na Sale huku fedha zilizokuwa zimeshatengwa kwa ajili ya miradi kwenye tatafa hiyo ikihamishiwa maeneo mengine huku wakitaja maeneo hayo na kisi cha fedha zilizohamishwa.

Alisema kuwa wakati serikali ikisema kuwa zoezi la wananchi kuhamia Msomera ni hiari lakini wamesitisha huduma zote muhimu hata ile ya  chakula cha bei nafuu kwa wananchi hao ambao hawaruhusiwi kuendesha kilimo.

Moringe alisema kuwa serikali ilivunja mkataba wa kugawa chakula hicho uliokuwa kati ya Baraza la Wafugaji na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, (NFRA) ambao walikuwa wakishirikiana kutoa mahindi ya bei nafuu kwa wananchi wa Ngorongoro huku akidai kuwa huduma hiyo imehamishiwa Msomera.

Hata hivyo alisema kuwa wanakiri serikali kwa kushirikiana na NCAA Halmashauri ya Ngorongoro wanawasomesha watoto wanaotoka kwenye familia duni lakini tokea kuanza kwa zoezi la kuhamishia wananchi Msomera wanafunzi hao wamekuwa wakikumbana na adha, tabu na mateso  baada ya NCAA kuamua kuwa kuchelewesha kutoa fedha hizo.

"Tunashangaa kama wakazi wa Ngorongori kusikia kuwa kati ya maeneo yenye huduma ya umeme nchini ni pamoja na tarafa ya Ngorongoro kwani hakuna kijiji au taasisi ya umma yenye umeme ndani ya tarafa hii isipokuwa NCAA  na wawekezaji wakubwa wa hoteli ambao ndiyo  chachu kubwa ya sisi wananchi kupata tabu hizi," alisisitiza Moringe.- 


Alisema kuwa kwenye tarafa hiyo hakuna shule tano za sekondari kama alivyosema Matinyi bali kuna shule tatu tu ambazo ni Embarway, Naionokanoka na ile ya wasichana ya Ngorongoro ambazo kwa sasa zinajiendesha katika mazingira hatarishi kwa afya ya watumishi na wanafunzi baada ya kunyimwa vibali vya ujenzi na ukarabati huku fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili hiyo zikiondolewa.

"Tarafa ya Ngorongoro in shule 29 na si 25 na zinafanya vizuri kitaaluma lakini zinatoa huduma katika mazingira hatarishi baada ya vyoo vyaje kujaa na kunyimwa vibali vya kujenga vyoo vingine na kufanyia ukarabati jambo ambalo likiendelea lilivyo wazazi wengi hawatawapeleka watoto wao shule hivyo watoto kukisa haki yao ya kuoata elimu," alisema Moringe.


Kwa upande wao, Mwakilishi wa wanawake, Nayee Sumare  na Diwani wa viti maalum, Sein Nengosek walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan afike tarafa ya Ngorongoro kuona hali halisi waliyodai  wananchi wengi  wanakufa kwa kukosa huduma za afya na si kwa kuliwa na wanyama wakali kama inavyoelezwa  na msemaji wa serikali.


Naye , Mwenyekiti wa baraza la wafugaji , Edward Maura ambaye pia ni diwani wa kata ya Nainokanoka alitoa mapendekezo ya wananchi hao ya  kupatia suluhisho matatizo yanayowakabili ambapo waliIomba serikali iiagize NCAA kutoa vibaoi vya ujenzi na kuruhusu miradi ya maendeleo iliyokuwa imesimamishwa.

Aidha wamependekeza serikali irejeshe mkataba baina ya baraza la wafugaji na NRFA ili warejeshe utaratibu wa kugawa chakula cha bei nafuu sanjari na serikali kurejesha meza ya mazungumzo na wananchi wa tarafa hiyo kwa lwnga la kuweka mikakati ya kuendeleza na kulinda uhai wa wananchi.

Maura alisema wanapendekeza serikali irejeshe utaratibu wa fedha za kusomesha wanafunzi wanaotokea kwenye familia duni kusimamiwa na baraza la wafugaji.

Pia serikali imuagize mkurugenzi wa halmashauri kuruhusu fedha zote zilizoko kwenye akaunti za vijiji na taasisi za umma zitumike kwa malengo mahsusi.

"Serikali irejeshe fedha za uendeshaji katika hospitali ya Endulen pamoja na kuruhusu mkataba baina ya jimbo Katoliki n wilaya ya Ngorongoro na hatimaye kurejesha huduma ya ndege ya shirika la Flying Medical service ambayo hufanya kazi ya kuwahudumia wananchi walio kwenye maeneo ambayo hayafikiki kwa lengo la kutoa huduma ya mama na mtoto," alisisitiza Maura na kuongeza.

"Serikalo iiagiza NCAA kuacha mara moja manyanyaso dhidi ya wenyeji na kufanya ushirikishwaji wa wenyeji kwenye masuala ya uwekezaji ndani ya eneo la Ngorongoro kwani ndiyo malengo GMP ya NCAA pamoja na sheria iliyoanzisha eneo hilo.

"Serikali ilete fidia ya ng'ombe ili kunusuru wananchi waliofilisika kwa kupoteza mifugobaada ya kula madini ya chumvi yenye sumu iliyonunuliwa na NCAA na kusambazwa kwa wafugaji ambao walizuiwa kupeleka mifugo huyo Kreta ya Ngorongoro walipokuwa wakipata madini hayo kwa njia ya asili,".


Akizungumzia mlipuko wa ugonjwa wa surua Mganga Mkuu mkoani Arusha, Dkt Charles Mkombachepa akiongea na  mwandishi wa habari hizi  kwa njia ya simu alisema kuwa haijathibitika kuwa eneo hilo lina mlipuko wa surua  ingawa baada ya kupata taarifa za kuhisiwa kuwepo kwa ugonjwa huo alituma timu ya wataalam kwenda kwenye eneo hilo na wamechukua sampuli zimepelekwa maabara kwa ajili ya kufanyiwa vipimp ambapo kwa sasa wanasubiri majibu.


 "Kuna maeneo tulipata watoto wenye dalili za ugonjwa huo tukachukua sampuli kwa ajili ya kufanyia vipimo zikirudi ndiyo wataweza kujua ni ugonjwa gani.Kuna maeneo kulikuwa na watoto chini ya miaka mitano wakihisiwa kuwa na dalili za surua tulichukua sampuli matokeo yakitoka ndiyo tunaweza kujua watoto hao walikuwa na tatizo gani," alisisitiss Dkt Mkombachepa na kuongeza.

"Kuna eneo lingine kuna baridi kali tulipoenda kuwafanyia vipimo tulikuta watoto wengi wana nimonia. Kulikuwa na watoto saba au nane wanasumbuliwa na nimonia,".



0 Comments:

Post a Comment