MILA POTOFU, KUHAMAHAMA KIKWAZO CHANJO KWA WATOTO

MILA potofu na jamii zinazoishi kwa kuhamahama imeelezwa kuwa ni chanzo cha baadhi ya watoto na watu wazima hapa  kutopatiwa chanjo hali inayowaweka kwenye hatari ya kushambuliwa na  kuathiriwa na magonjwa ambayo yanangweza kuzuiliwa kwa chanjo.



Meneja wa mpango wa Taifa wa chanjo,Dk.Florian Tinuga ameyasema hayo leo Jumatano Juni 7,2023  wakati akizungunza na waandishi wa habari wa kanda ya kaskazini waliokuwa wakishiriki semina ya siku moja iliyolenga kuwaongezea uelewa juu ya umuhimu wa chanjo zinazotilewa na taasisi hiyo ya serikali iliyo chini ya wizara ya Afya. 


Amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii ili wazazi na walezi waelewe umuhimu wa chanjo hizo kwa watoto wao jambo ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa ingawa kwenye baadhi ya  maeneo bado kuna changamaoto.


Dkt Tinuga amesema kuwa kwa jamii ambazo wamekuwa wakihamahama wamekuwa wakiwashauri kutoa taarifa kwa uongozi wa vijiji pindi wanapokuwa wanahama au kuhamia kwenye eneo juu ya taarifa za chanjo kwa watoto walionao jambo linalowezesha watoto hao kupatiwa chanjo hizo kwa wakati endapo bado hawajakamilisha.

Hata hivyo amesema kuwa mila potofu zimekuwa zikikwamisha juhudi za kutoa chanjo kwa watu wazima ingawa  zimekuwa  hazitokei sana kwa chanjo ya mtoto chini ya umri wa miaka mitano.


" Changamoto inatokea kwa chanjo ya watu wenye umri zaidi ya miaka mitano. Ikumbukwe hakuna chanjo inayoingizwa nchini ikiwa na tatizo, kuna jopo la wanasayansi ambao limeteuliwa na Waziri wa afya kwa ajili ya kuthibitisha ubora na matumizi yake  kabla na baada ya chanjo kuingizwa nchini," amesema Dkt Tinuga na kuongeza,"..


...Sisi mpango wa Taifa wa chanjo tunasimamia chanjo katika makundi manne ikiwa kundi la kwanza ni  chanjo za watoto chini ya miaka mitano, HPV (chanjo ya kuzuia saratani ya shingo  ya uzazi) kwa upande wa wasichana wenye umri wa miaka 14 na bado mwitiko wake ni mdogo hususani kwenye dozi ya pili,".

Amesema kundi la tatu ni chanjo wanazozisimama ni zile za wajawazito ambao wamekuwa na mwitiko mkubwa isipokuwa changamoto  inatokea pale mama mjamzito anapochelewa kuanza kuhudhuria kliniki hivyo akawahimiza wanawake wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mapema ili kujihakikishia usalama wao na watoto wao kwa kupata chanjo kwa wakati.

Hata hivyo Dkt Tinuga aliendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupatiwa chanjo ya Uviko 19 iliyoanzishwa mwaka 2021 huku akisisitiza kuwa chanjo hizo zinapatikana bure katika vituo vyote vya afya nchini kwa asilimia 100 hivyo wananchi hawapaswi kutozwa fedha ili wapatiwe.



Naye Mganga mkuu wa Mkoa Arusha,  Dkt, Sylvia  Mamkwe,  amewahimiza wanawake na watoto wa kike kujitokeza kupima saratani ya shingo  ya uzazi kwani ikigundulika mapema inatibika.

Amesema kuwa kumekuwa na taarifa za kupotosha juu ya upimaji huo zikidai kuwa umekuwa ukisababisha maumivu makali kwa wanaopimwa jambo alilofafanua kuwa halina ukweli na kipimo hicho kinafanywa kwa muda mfupi  na wataalam wa afya na hakina maumivu yoyote.

"Katika saratani ambazo zinatibika ni hii ya saratani ya shingo ya kizazi inatibika na serikali imewekeza nguvu kubwa ili kuokoa watu.Tusiogope  kipimo hakiumi... watoto wa kike wapate hii chanjo ili kulinda kizazi kijacho," amesisitiza Dkt Mamkwe.



Kwa upande wake,  Ofisa Mpango wa Taifa wa Chanjo Wizara ya Afya, Lotalis Gadau  amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa waandishi wa habari  kutoka mikoa yote nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kutosha juu ya chanjo hizo ili wakaielimishe jamii.

Amesema kuwa chanjo ya shingo za kizazi inayotolewa kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 imekuwa na changamoto kwani mara nyingi chanjo ya kwanza hutolewa kwa watoto hao wakiwa shule ya msingi ambapo muda wa kumpatia chanjo ya pili ukifika unakuta tayari ameshamaliza shule hivyo kumpata inakuwa ni changamoto.

Hata hivyo amesema kuwa wamekuwa waijitahidi kutoa chanjo hizo katika muda ambao chanjo ya pili itatolewa wanafunzi wakiwa shule baada ya kubaini changamoto hizo.




"Watoto hawa ni muhimu kuchanjwa ili kuwalinda, lakini kwa wale wanaopatikana mapema wakiwa na saratani ya shingo ya uzazi  kuna dawa wanapewa na kupona,wakichelewa kupima na kubainika madhara ni makubwa yanasababisha baadhi yao kupoteza maisha," alisisitiza Gadau.



Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamekuwa wakitolewa kwenye kanda mbalimbali ambapo kwa kanda ya kaskazini yalishirikisha waandishi kutoka mkoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

0 Comments:

Post a Comment