WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini, wameaswa wasirudie makosa yale waliyoyafanyia toba kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakitakiwa kuipenda nchi na watu wake bila kujali tofauti za kiimani.
Aidha wamemfanyia dua maalum Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi Kiislam ya Twariqa Tul Qadiriyya, Sheikh Salimu Mubarak maarufu kama Dar-Weish Mti Mkavu ambaye anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Jeshi Lugalo jiji Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa Mei 14, 2021 na Naibu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sheikh Husein Seleman, wakati wa baraza la Eid el-Fitr lililofanyika kwenye makao makuu yao yaliyopo Ngarenaro jijini Arusha.
Alisema kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani wamepewa mafundisho ya dini yaliyolenga kuwafanya kuwa wacha Mungu ili wakifa wingie peponi na Mtume Muhamad SAW .
"Tusirudi sasa kwenye yale makosa, yale ambayo tumeyaombea toba tusirudie kuyafanya tena. Swaumu inatujenga kuwa waja wema sio watu wabaya, tuendelee kutenda mema, tuendelee kuhurumiana, tuendelee kusaidiana, tuendelee kusikilizana," alisewma Sheikh Husein na kuongeza.
"Hayo ndiyo maelekezo ya funga, haikuwa funga kututesa kwa njaa na kiu bali ni kutufanya tuwe na tabia njema,".
Naibu Mwenyekiti huyo wa aliwahimiza Waislam kuipenda nchi yaona kuindokana na tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watu kutamani kuwa wangezaliwa kwenyw mataifa ya ulaya.
"Ni vizuri upende mahali ulipozaliwa, na kuipenda nchi yako ndiyo kuwapenda wenzako. Wenzako ni Waislam na wasiokuwa Waislam. Ukiwapenda ukawa nao mkisikilizana ndiyo kuipenda nchi yako," alisema Sheikh Husein na kuongeza.
"Kwa kuwa wewe hutaki kutukanwa basi usimtukane mwenzako, hutaki kupigwa usimpige mwenzako, hutaki kufanyiwa jambo lolote baya basi usimfanyie mwenzako.Amani itapatikana kwa njia hii,".
Sheikh Hussein alisema kuwa watoto wengi walio kwenye shule za bweni hawajaruhusiwa kuungana na familia zao kusherekea Eid kutokana na ugonjwa wa corona ambao uliwasababisha mwaka jana kukaa nyumbani muda mrefu hivyo wanakazana kumalizia ratiba za masomo lakini wazazi hawana hofu kwani nchi ina amani.
"Huko Gaza watu wana bunduki wengine wana mawe, sijui hata kama wameswali Eid. Bado na Corona ipo amani na utulivu hakuna. Sisi tunapaswa sana kumuomba Mwenyezi Mungu katika nchi yetu tuzidishe upendo," alisema Sheikh Hussein.
Alisema kuwa huo ndiyo ujumbe wa Sheikh Darwesh aliomwagiza kuwafikishia waumini wa kiislam kuipenda nchi na watu walio kwenye nchi hii." Sasa wewe Muislam fanya mambo yako mema na mazuri yamvute kwenye uislam usimbughudhi wala usimtukane,".
Kwa upande wake, mgeni Rasmi kwenye baraza hilo, Mussa Mkangaa, amewataka waumuni hao kwa umoja wao kumuombea Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sheikh Salim Mubarak ili apone mapema.
"Sheikh , Salim Mubarak amebakiza mwaka mmoja atimize karne lakini ukimuangalia huwezi kuamini. Hizi zawia karibu zote amezunguka yeye kuzianzisha, kwenye kila mkoa ukipita unakuta Sheikh Salim Mubarak amepita na ametoa darasa," alisems Mkangaa .
Kuhusu suala la maendeleo aliwashauri ni vema wakaangalia ni jambo gani la kufanya ili waweze kufikia malengo yao ya maendeleo waliyojipangia.
Mkangaa aliahidi kukutana na baraza la uongozi ili waandae harambee ya kukusanya fedha ambapo aliwapa matumaini kuwa watafanikiwa kama walivyowahi kufanya mashindano ya kusoma kuruhani na mshindi alipewa zawadi ya gari.
Awali, Katibu mkuu wa Twariqa Tul Qadiriyya, Abdi Kisiu akisoma risala ya taasisi hiyo alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 wamefanikiwa kuongeza zawia kwenye mikoa wa Mwanza, Morogoro, Tanga na Dodoma.
Alisema kuwa walifaniwa kuendeleza baadhi ya majengo yaliyokuwa yamekwama na kufanikisha kuzitembelea zawia zao kwenye mikoa mbalimbali kujionea namna zinavyojiendesha.
Kisiu alisema kuw wamefanya vikao vyao kuanzia ngazi za wilaya, mkoa na taifa kwa wakati na kupeleka taarifa wizara ya ndani sanjari na kudumisha ushirikiano na taasisi nyingine ikiwemo Baraza la Waislam nchini,(BAKWATA).
Hata hivyo alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usafiri kwa viongozi kuanzia ngazi ya wilaya mpaka Taifa pamoja na ukosefu wa fedha za kuwawezesha kuendesha shughuli za taasisi.
Hivyo akaomba mgeni rasmi kushirikiana nao kuandaa harambee ili kuchangisha fedha za kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo na ununuzi wa vifaa vya ofisi.
Mwenyekiti wa wanawake, Rehema Athumani (kulia) |
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Twariqa Tul Qadiriyya, Rehema Athuman amempongeza mgeni rasmi kwa kukibali kujumuika nao kuunda kamati ya harambee ili wakusanye fedha za kutekeleza miradi ya taasisi.
0 Comments:
Post a Comment