KIMEI : HAKUNA MWANANCHI VUNJO ATAKAYECHA KUUNGANISHIWA UMEME




VIJANA katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro sasa wataweza kujiajiri  kutokana na serikali ya awamu ya tano kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuunganisha nishati ya umeme maeneo ya vijijini ambapo kulionekana kutelekezwa kwa kipindi kirefu


Mbunge wa jimbo la Vunjo, Dkt Charles  Kimei aliyabainisha hayo mara baada  ya kutembelea miradi ya uunganishwaji umeme unaotekelezwa katika kitongoji cha Kilindini na Kawawa pamoja na vijiji vya Manu kitongoji cha Lole na Nganjoni kitongoji cha Urenga ambavyo miradi yake itaanza wiki tatu zijazo kupitia mradi wa umeme jazilizi "Electric densification" unaotekelezwa na TANESCO.


Dkt Kimei alisema kuwa vijana wengi katika maeneo hayo wameshindwa kujiajiri licha ya kuwa wana taaluma ya uungaji vyuma,mapambo na kazi nyinginezo zinazohitaji nishati hiyo na kuwa adha hiyo inaenda kupata ufumbuzi ndani ya siku chache.



Katika ziara yake hiyo Dkt Kimei mbali na  kushiriki zoezi la usimikaji nguzo za umeme kitongoji cha Kilindini kijiji cha Mabungo kata ya Kirua Vunjo Kusini na kuwahakikisha wananchi kuwa hakuna mwananchi  katika jimbo la Vunjo atakayekosa kuunganishiwa umeme.


"Najua ipo idadi kubwa ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Vunjo walishaziwekea nyumba zao mifumo ya umeme 'wiring' tayari kwa kupata umeme ambao mpaka sasa bado hawajapata huduma ya umeme tena baadhi yao ni muda mrefu sasa, naomba kuwatia moyo kuwa wawe wenye subira kwani ndani ya miezi 18 ijayo kila mmoja atakuwa amepata nishati hii"alisema


Aidha Dkt Kimei aliishukuru serikali kwa miradi hiyo ya umeme na kuwataka wananchi ambao bado hawajapata umeme kuwa watulivu kwani ahadi ya Mhe Rais Dkt Magufuli ni kuwa ndani ya miezi 18 ijayo kila kijiji kitakuwa na umeme.


Mwenyekiti wa Kijiji Cha Manu Joseph Chaky alisema kwa kipindi kirefu wamekosa nishati hiyo jambo likikochangia biashara nyingi kukwama na kuwa kwa sasa Wana inani tosha kuwa nishati hiyo itaenda kuwafikia.


"Vijana wapo wengi wenye ujuzi ila kwa kuwa umeme haukuwepo walishindwa kujiajiri ila kwa Sasa tuna imani kubwa kuwa umeme utafika serikali ya awamu ya tano imefanya mambo makubwa Sana hili halitawashinda"alisema


Alisema kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme wapo baadhi ya wanasiasa walikuwa wakiwahadaa kuwa wangewaletea umeme zaidi ya miongoni miwili na kuwa sasa jambo hilo limeenda kufika tamati.


Naye Erasmus Masawe mkazi wa 

kijiji cha Manu alisema kupatikana kwa huduma ya umeme kutachangia kupanuka kwa shughuli za kimaendeleo tofauti na ilivyo hivi sasa.


"Tunaenda kufungua ukurasa mpya wa mafanikio kwani tulikwamishishwa kwa kipindi kirefu Sana Jambo tunaloliona linatia matumaini kuwa umeme unakuja muda si mrefu"alisema.


Mohamed Kayanda ni meneja wa shirika la umeme nchini (TANESCO)wilaya ya Himo ambapo alisema hadi sasa jimbo la Vunjo tayari umeme umeshasambazwa kwa asilimia 80 na kuwa zoezi la uunganishwaji ni endelevu na lengo ni kuwafikia wananchi wote  kama ilivyo dira ya serikali.


"Tunaendelea na zoezi la uunganishwaji hapa kijiji cha Manu tunaanza na wananchi 200 kwanza alafu awamu ya pili tumalizie hao wengine 200 hapa tutakuwa tumemaliza ni lazima wananchi wapatiwe huduma hii"alisema


Imeandikwa na Gift Mongi

0 Comments:

Post a Comment