WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa za masoko ya ajira na biashara zilizoko kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC), badala ya kujiweka kando na kuendelea na malalamiko ya ukosefu wa ajira.
Hayo yalisema mwishoni mwa wiki na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), kutoka Tanzania, Adam Kimbisa wakati akiongea na waandishi wa habari jijini hapa anapohudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea.
Alisema kuwa ni vema zinapotokea fursa Watanzania wakazichangamkia huku akitolea mfano kwenye sekta ya habari kuna fursa kwenye mataifa ya Kenya na Uganda hivyo wenye taaluma hiyo wakazichangamkia ajira hizo.
Kimbisa alisema Watanzania wengi ni waoga kujaribu kwa kile alichoeleza kuwa wanapenda kukimbilia kwenda kununua bidhaa hasa China na India lakini hawapeleki bidhaa yoyote kwa ajili ya kuuza kwenye nchi hizo huku akisisitiza nchi za EAC kuna soko la mazao mengi yanayozalishwa kwa wingi hapa nchini.
"Hapa Afrika mashariki kuna masoko nilikuwa naongea na mtu mmoja kutoka Rwanda ananiuliza kwani nini hatupeleki pamba na kata yetu tukawauzie waitumie kwenye viwanda vyao badala ya kuipeleka nchi za mbali," alisema Kimbisa.
Alisema hatua ya Tanzania kuboresha miundombinu yake ya reli ya umeme "itanufaika sana kwani itayavutia mataifa ya EAC kutumia bandari ya Dar es Salaam kutokana na kupungua kwa gharama zao za uendeshaji na muda wa kusafirisha mizigo wakitumia reli.
"Kusema kweli kama bandari yetu ikifanya kazi vizuri, na jinsi Rais wetu (John Magufuli) anavyokazana tupate reli ya umeme hawa majirani zetu hawawezi kukwepa wapende wasipende watatumia bandari ya Dar es Salaam ikiwa 'efficincy' na watatumia reli yetu ya 'standard gauge' kwa sababu itakuwa ni reli ya umeme," alisema Kimbisa na kuongeza.
Kwa hiyo ile sababu ya kusimamishwa simamishwa njiani kwamba hapo cheki mzigo hapo utamkuta trafiki itakuwa hakuna. Mzigo ukitoka ni moja kwa moja Burundi au moja kwa moja Rwanda au moja kwa moja Eastern Kongo na Uganda nao itabidi wapishie mizigo yao kwetu,".
Hapo itabidi tutengeneze 'hub' na bandari itakuwa hub vizuri kama mizigo itapokelewa na kupakuliwa halafu siku inayofuata asubuhi taasisi nyingine zilizopo bandarini kama TRA 'customs' watakuwa wapo ' efficient' na reli 'efficient' kwa hiyo mizigo itakuwa inatoka bandarini nakusafirishwa kwa reli moja kwa moja kwenye nchi husika,".

0 Comments:
Post a Comment