WAHASIBU WATANO HIFADHI YA NGORONGORO WABURUZWA MAHAKAMANI




WAHASIBU  watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCAA), wameburuzwa kwenye mahakama ya Wilaya ya Arumeru wakidaiwa  kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 35,500 sawa na zaidi ya shilingi milioni 79.5.


Wamefikidhwa mahakamani hapo leo na kusomewa shitaka la uhujumu Uchumi na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini,(TAKUKURU), Adam Kilongozi mbele ya hakimu Mkazi, Bernad Nganga wa mahakama ya Wilaya ya Arumeru.

Washitakiwa hao, Joseph  Ntwala, (36), John Mlambo, (42), Mwagu Yunus,(38) na Catherine Edward, (33) wanadaiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 25,2013 na Juni 6,2014 kwenye malango ya kuingilia hifadhi ya Ngorongoro likiwemo la Nabi mkoani Mara na Lodwale lililopo Karatu mkoani Arusha.

Washitakiwa hao walikana shitaka hilo ambapo wamepelekwa mahabusu kwenye gereza la mkoa la Kisongo  baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja aliyetakiwa kuweka dhamana ya shilingi milioni 7.9 au mali isiyohamishika yenye dhamani hiyo.

Shauri limeahirishwa  mpaka Aprili 10, mwaka huu litakaporudi mahakama hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali kwani  upelelezi umekamilika.


0 Comments:

Post a Comment