SERIKALI YA TANZANIA YABURUZWA MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI KWA KUMINYA UHURU WA HABARI





SERIKALI imeburuzwa mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, (EACJ), ikidaiwa kuminya uhuru wa wananchi kupata habari na kuwawekea vikwazo waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao.

Shauri hilo linalovuta hisia za wengi limefunguliwa mahakamani hapo na Baraza la Habari Tanzania,(MCT) kwa kushirikiana na  Kituo cha sheria na haki za Binadamu,(LHRC) na Muungano wa Asasi zinazotetea haki za binadamu,(THRDC) wakilalamikia sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016.


Shauri hilo  namba 2/2017 limesikilizwa jana kwa hatua za awali na majaji watatu wa mahakama hiyo, wakiongozwa na Jaji Monica Mugenyi, akisaidiana na Jaji, Dk Faustin Ntezilyayo na Jaji, Fakihi Jundu.

Waleta maombi wanawakilishwa na mawakili  watatu wakiongozwa na Donald Deya, akisaidiana na  Jebra Kombole na Jenerali Ulimwengu ambapo mjibu maombo ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG), aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Mark Muluambo.

Katika hoja zao za msingi upande wa waleta maombi wanadai kuwa sheria hiyo iliyopitishwa na bunge Novemba 5 mwaka jana na kuidhinishwa na Rais, Novemba 16, mwaka jana inaminya uhuru wa wananchi kupata habari kwa kuweka vikwazo ambavyo wanaona havina sababu ya msingi kuwepo.

Aidha wamedai kuwa sheria hiyo inazuia uhuru wa vyombo vya habari jambo ambalo linaenda kinyume na kipengele cha msingi cha mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) unaohimiza demokrasia, utawala wa sheria, uwajinikaji, uwazi na utawala bora.

Hivyo wameiomba mahakama hiyo kuamuru kufutwa au kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo ili ikidhi matakwa ya mkataba wa kuanzishwa kwa EAC.

Kwa upande wake mawakili wa Serikali walipinga hoja hizo kwa madai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza maombi hayo hivyo wakata maombi hayo yatupwe.

Walidai kuwa hsheria hiyo inayolalamikiwa imezingatia kipengele cha 18 cha katiba ya Tanzania juu ya uhuru wa kujieleza na sheria hiyo iko sahihi kwani  kinatoa umuhimu wa kipekee kwa ufahamu wa  umma  kwenye masuala yenye maslahi ya Taifa huku ikilinda  haki na maslahi ya watu binafsi.

Walidai kuwa sheria hiyo hakijakiuka mkataba wa kuanzishwa kwa EAC kwani imeenda sawa na kuwa sheria hiyo haiminyi uhuru wa habari badala yake kimetoa haki na majukumu kwa vyombo vya habari ambayo wataitumia wenyewe kutekeleza haki hiyo.

Baada ya mahakama hiyo kusikiliza na kujadiliana masuala ya msingi yanayobishaniwa na yale yasiyobishaniwa kwenye shauri hilo walipanga utaratibu wa kusikilisha shauri hilo ambapo mawakili wa waleta maombi wametakiwa kuwasilisha hoja zao kwa maandishi April 13, mwaka huu.

Mawakili wa Jamhuri watatakiwa  kuwasilisha hoja za majibu Mei 14, mwaka huu ambapo upande wa waleta maombi watatakiwa kuwasilisha hoja za nyongeza  Mei  28, mwaka huu endapo watahitaji kufanya hivyo.

Baada ya hapo mahakama itapanga tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa hoja za pande zote kwa njia ya majadiliano kabla ya kupanga kwa tarehe ya kutoa uamuzi.










0 Comments:

Post a Comment