Marekani imesema kuwa inapanga kuwasilisha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mswada wa azimio la vikwazo vikali zaidi kwa Korea Kaskazini inayolenga kupitishwa ifikapo Jumatatu ijayo.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley wakati akizungumza katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika jana Jumatatu.
Mkutano huo uliombwa na Japani, Marekani, Korea Kusini, Uingereza na Ufaransa.
Balozi Haley aliliasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kali iwezekanavyo dhidi ya Korea Kaskazini.
Alisema licha ya kuwa vita sio jambo Marekani inalopendelea, uvumilivu wa nchi yake una ukomo.
Kwa upande wake Balozi wa Japani katika Umoja wa Mataifa, Koro Bessho, alisema nchi zinapaswa kuweka shinikizo zaidi kwa Korea Kaskazini kabla ya vitendo vya nchi hiyo kusababisha madhara makubwa. Alivitaja vikwazo vilivyopo sasa dhidi ya nchi hiyo kuwa havitoshelezi na akasisitiza juu ya umuhimu wa kuidhinishwa kwa azimio la vikwazo vikali zaidi.
Vyanzo vya habari vya kidiplomasia vimesema kuwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zingeweza kujadili kwa kina kuwawekea vikwazo raia wa Korea Kaskazini wanaofanya kazi katika nchi za China na Urusi, pamoja na kupiga marufuku usafirishaji wa mafuta kwenda Korea Kaskazini.
Wawakilishi wa China na Urusi katika mkutano huo hawakugusia kabisa suala la kuweka vikwazo zaidi.

0 Comments:
Post a Comment