BAWACHA DAR ES SALAAM WAANZA SHAMRA SHAMRA ZA MIAKA 25 YA CHADEMA KWA AINA YAKE


Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA)  Dar es salaam, ambalo linaunganishwa na mikoa ya kichama ambayo ni Kinondoni, Ilala,Temeke,Ubungo na Kigamboni, leo Jumapili 6 Agosti 2017, wameanza rasmi shamra shamra za kuelekea sherehe za miaka 25 toka kilipoanzishwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (CHADEMA)  kwa kutoa misaada kwa watoto yatima katika kituo cha Yatima Group Trust Fund kilichopo Chamazi jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Kamati  ya sherehe hizo,  Magreth  Mugyabuso akiongea mbele ya watoto yatima hao pamoja na mama mlezi wa  kituo hiko, Bibi Winfrida Lubanza amewataka watoto hao wasijione wako pekee yao na yatima kwa sababu CHADEMA  kipo nao pamoja, kama ilivyo kauli mbiu ya CHADEMA "Nguvu ya Umma" kwa hiyo nguvu ya umma wanajiunga na kushirikiana na umma katika masuala mbalimbali yanayoihusu jamii.

Amesisitiza jamii kuendelea kujitoa kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu, kwani watoto hao ndio watakuwa viongozi baadae katika Taifa hivyo wanapaswa kujaliwa.

Viongozi wengine walioshiriki leo wakiwemo wanachama,wapenzi na wakereketwa wa chama hiko ni Mbunge wa Viti Maalum Segerea,Mhe. Anatropia Theonest, Mbunge Viti Maalum Temeke, Mhe. Lucy Mageleli na Mbunge Viti Maalum Kinondoni,Mhe. Susanne  Lyimo, Mjumbe wa Kamati Kuu, Catherine Valence, Wajumbe wa Baraza Kuu, Florence Kasilima,Janet Josia,Hellen Dalali, viongozi mbalimbali  wa Chama katika Wilaya, Kata na misingi.

Akishukuru kwa niaba ya watoto yatima mama mlezi wa kituo mama Winfrida Lubanza amekishukuru CHADEMA kupitia Baraza la Wanawake (BAWACHA), kwa uamuzi waliofikia wa kwenda kuwatembelea "Toka mwaka 2017 uanze huu ndio ugeni mkubwa kuliko yote iliyofika kituoni hapa, natoa changamoto kwa taasisi nyingine na watu binafsi waige mfano wa  BAWACHA na CHADEMA kwa ujumla" Amesema.

Vifaa vilivyotolewa kwenye kituo hiko vinathamani ya shilingi 2,000,000/=, vitu vilivyotolewa ni mafuta ya kupikia, dawa za maneno, taulo za watoto (pampers) nguo, juisi,sabuni, mifuko ya saruji n.k.

Akiongea Mbunge wa Viti Maalum Segerea, Mhe. Anatropia Theonest amesema CHADEMA ni chama ambacho kimewatetea Watanzania  wakati wote ingawa kuna changamoto mbalimbali.

"Kuna watu wanasema sasa hivi watu wanaisoma namba CHADEMA tumeshazoea kuisoma namba, hali ngumu na mazingira magumu ya siasa kwa upinzani haujawahi kuwa mwepesi, lakini hatutakata tamaa mpaka tuhakikishe tunawakomboa Wananchi na kuwaletea mabadiliko ya kweli" amesema Mhe. Anatropia Theonest.

Katika Baraza Kuu la  Chama lililoketi mkoani Dodoma mwaka huu mjini Dodoma, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe.  Freeman Mbowe, alisema Kamati ya Kuu ya Chama imeazimia kuwa sherehe za miaka 25 ya Chama yataongozwa na BAWACHA kwa mwaka huu ambapo kila mkoa kutakuwa na matukio mbalimbali kabla kilele chenyewe hapo baadae mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment