Japani na Urusi zilikubaliana wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo mwezi Aprili mwaka huu, kufanya utafiti kwenye visiwa hivyo vinavyozozaniwa.
Timu ya maafisa wa serikali na maafisa wa biashara wameondoka kwenye bandari iliyopo mkoani Hokkaido kaskazini mwa Japani, leo Jumanne asubuhi.
Watafanya ukaguzi wa vituo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kusindika samaki, hoteli na hospitali katika Kisiwa cha Kunashiri pamoja na kisiwa cha jirani cha Etorofu.
Wajumbe hao pia watakutana na wenzao wa Urusi ili kutathmini mahitaji ya kiuchumi ya wakazi wa maeneo hayo. Upande wa Japani unatumai kuwa matokeo ya utafiti huo yatasaidia kupunguza idadi ya miradi inayopendekezwa.
Japani na Urusi bado hazijatiliana saini mkataba wa amani kutokana na mgogoro wa maeneo unaohusisha visiwa vinne vinavyodhibitiwa na Urusi. Maafisa wa Japani wanataka kujenga uaminifu wa pande mbili kupitia miradi hiyo ya pamoja ili hatimaye waweze kutatua mgogoro huo wa maeneo.
Serikali ya Japani imeendeleza msimamo wake kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya eneo lake la urithi na kuwa vilitwaliwa kinyume na sheria baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

0 Comments:
Post a Comment