Ndugu waandishi wa habari,
Natumaini mna taarifa kwamba tangu Ijumaa iliyopita, nimefungua shauri
Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, kupinga kinachofanywa na Bunge
Maalum la Katiba. Shauri hilo, limesajili kwa Na.28 la mwaka 2014.
Katika kesi hiyo, nimeomba Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi juu ya
mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba, chini ya kifungu cha 25 (1) na (2)
cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya mwaka 2011.
Aidha, nimewasilisha maombi madogo nikiomba Mahakama kutoa zuio la
muda la kusimamisha Bunge Maalum la Katiba, wakati tukisubiri uamuzi
wa kesi ya msingi. Maombi ya zuio yamepangwa kutajwa tarehe 4 Septemba
na kesi ya msingi itatajwa 15 Septemba 2014.
Ndugu waandishi wa habari,
Tangu kuripotiwa kufunguliwa kwa shauri hili mahakamani, yapo mengi
yaliyosemwa. Wapo walionipongeza na kunifariji. Wapo walionitia moyo
na kuniomba nisirudi nyuma. Wapo walionidhihaki na kunikatisha tamaa.
Wapo walionitisha.
Lakini wapo walioahidi kuniombea kwa Mwenyezi Mungu ili jambo hili
kubwa nililolifanya kwa maslahi ya taifa langu, niweze kulifikisha
mwisho nikiwa mzima na mwenye amani.
Ninafahamu jukumu hili nililolibeba ni zito sana. Linaweza
likasababisha baadhi ya watu kukosa posho ikiwa mahakama itaridhia
ombi langu la usitishaji wa Bunge la Katiba. Linaweza kunitenganisha
na baadhi ya ndugu na marafiki zangu. Linaweza kuhatarisha hata maisha
yangu.
Lakini kwa kuwa maisha yangu hayajawahi kuwa salama kwa zaidi ya miaka
tisa sasa; nimesema Mungu ndiye atakayenilinda.
Ninajua kuwa kesi hii, inaweza kusababisha gazeti langu la -----------
ambalo limefungiwa kwa muda usiojulikana na watawala kwa kuitumia
sheria katili ya magazeti, linaweza lisifunguliwe kabisa. Hii ni kwa
sababu, waliofungia ----------- ndiyo haohao niliowashitaki.
Hata hivyo, nimesema niko tayari kwa lolote. Nitakabaliana nalo kwa
kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniongoza.
Ndugu waandishi wa habari,
Nimefungua shauri hili kwa kusukumwa na uzalendo wangu na kulinda
heshima ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano waliotoa maoni yao mbele ya
Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, nami nikiwamo.
Nimefungua shauri hili baada ya kujiridhisha kuwa wananchi waliowengi,
kutoka makundi mbalimbali - serikalini hadi chama tawala - wanakiri
kuwapo tatizo katika tafsiri ya sheria kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum
la Katiba.
Baadhi ya walioko bungeni wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba, Samwel Sitta, wanasema wanaweza kufanya lolote katika rasimu.
Wanaweza kufuta rasimu; kubandua sura yote na wanaweza kubandika sura
mpya.
Siyo hivyo tu: Wanaweza hata kukusanya maoni upya kutoka makundi
mbalimbali. Kazi hii, ndiyo inayofanyika sasa bungeni.
Lakini wapo wanaoamini kuwa Bunge Maalum la Katiba, halina mamlaka ya
kufanya kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Halina uwezo kukusanya
maoni upya.
Bunge Maalum la Katiba, haliwezi kunyofoa moyo wa rasimu ya katiba
kama ilivyowasilishwa na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba na kuleta kitu kipya
ambacho hakikutokana na wananchi; na ambacho kimekusanywa kinyume cha
sheria.
Nimekwenda mahakamani baada ya kumuona Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Fredrick Werema akishindwa kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Badala yake, Jaji Werema amempotosha
rais kuwa hana mamlaka ya kusimamisha mchakato wa Katiba.
Sheria inayosimamia mchakato wa katiba mpya ni sheria tofauti na
sheria nyingine katika nchi. Sheria nyingine zote zinasimamiwa na
vyombo vya serikali. Hii inasimamiwa moja kwa moja na wananchi.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotumika sasa, haina kifungu chochote
kinachoruhusu kutungwa katiba mpya. Wabunge wote wa Bunge la Muungano
ambao sasa wamefanywa wajumbe wa Bunge la Katiba, akiwamo Werema,
waliapa kulinda katiba iliyopo na kuitetea. Rais wa Jamhuri ya
Muungano ameapa kulinda katiba iliyopo.
Lakini kwa kuwa Bunge la Jamhuri liliridhia kutunga katiba mpya kwa
kutumwa na wananchi - siyo kwa kutumwa na katiba iliyopo - rais anayo
mamlaka mapana ya kusimamisha mchakato huu.
Rais anaposimamia mchakato huu, hafanyi hivyo kama rais binafsi.
Anatekeleza matakwa ya wananchi ambao wote kwa umoja wao, wamempa yeye
mamlaka yao kusimamia raslimali, ulinzi na usalama wa mali za raia wa
Jamhuri ya Muungano.
Kwahiyo, ni ujuha kuacha mabilioni ya shilingi ya wananchi kuteketea,
kisha watawala wakadai kuwa "rais hana mamlaka ya kusimamisha mchakato
wa katiba mpya."
Kutokana na mgongano huo, kama mwananchi wa Jamhuri ya Muungano
nimewasilisha malalamiko yangu mahakamani kwa nguvu ya Ibara ya 26 (2)
ya Katiba inayosema: "Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na Sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya
katiba na Sheria za nchi."
Suala zima la maoni ya wananchi haliwezi kuachwa mikononi mwa watu
wachache. Mamlaka ya kutafsiri sheria za nchi, hawezi kuachwa mikononi
mwa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum la Katiba wala chombo kingine
kilichojinyakulia mamlaka hayo kinyemela.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Ibara ya 107 A (1), "mamlaka yenye
kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni
mahakama."
Kwa msingi huo, iwapo tafsri yangu ni sahihi, kinachofanywa na Bunge
la Katiba sasa, ni uvunjaji wa Sheria Na. 83 ya mwaka 2011, inayounda
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanisha majukumu yake na Bunge la
Katiba.
Kama tafsiri yangu ni sahihi, kinachofanywa na Bunge Maalum la Katiba,
ni kuvunja Katiba. Hakikubaliki.
Hivyo basi, kupitia kwenu, nichukue nafasi hii, kuwaomba wananchi wote
wanaolitakia mema taifa letu, kusimama pamoja nami katika kusaidia
taifa kupata katiba inayoheshimu maoni ya wananchi.
Ninawashukuru wote waliofariji; wanaonitia moyo na walioahidi
kuniombea katika hili. Ninawaomba waniunge mkono kwa hali na mali.
Nchi hii ni yetu sote.
Saed Kubenea,
Mkuregenzi Mtendaji,
HHP Limited.
AKIBA COMMERCIAL BANK PLC YAWATOA HOFU WATEJA WAKE WA KARIAKOO
-
Akiba Commercial Bank Plc imeendelea kujitoa si tu kuhudumia wateja wake
bali pia kushiriki katika juhudi za kijamii wakati wa dharura na majanga,
ikiwa ...
4 hours ago
0 Comments:
Post a Comment