Ask. KAKOBE; Kikwete awaombe radhi watanzania

Kakobe amlaumu Kikwete Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe,
amemshambulia Rais Kikwete kwamba ndiye aliyevuruga mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya.
Kakobe amewataka wajumbe wa UKAWA kutorejea katika Bunge Maalum la Katiba
ambalo alidai limejazwa unafiki na endapo wakiamua kurejea watakuwa wamerogwa.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam
katika maadhimisho ya miaka 25 ya kanisa
hilo lililoanzishwa mwaka 1989.
Alisema Rais Kikwete, alipolizindua Bunge
Maalum la Katiba, alitumia fursa hiyo kutoa
hoja za kuvuruga rasimu ya wananchi ambayo
iliwasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
Askofu Kakobe alisema hoja za Rais Kikwete
za kujikanganya alizozitoa siku hiyo, yalikuwa
ni majibu ya maombi ya Jumuiya ya Wakristo
wa Kipentekoste (PCT) ya kuvuruga mchakato
wa katiba baada ya kutoa upendeleo kwa
kuwateua baadhi ya wajumbe wakiwamo
viongozi wa dini, kupata uwakilishi kwa
baadhi ya Wakristo bila kutenda haki kwa
wananchi wote.
Alisema katika mambo yanayofanywa
makusudi na wanadamu, Mungu amewapa
akili ya kuyavuruga, hivyo ndiyo maana
wakiwa katika viwanja vya Sabasaba waliamua
kufanya maombi na nguvu ya Mungu
inatumika sasa kuonyesha kuwa mchakato
huu ulianzishwa pasipo haki.
"Namtaka Rais Kikwete akiri hadharani kuwa
amekosea na awaombe Watanzania radhi kwa
makosa aliyoyafanya hata kusababisha
wanasiasa upande wa upinzani kuunda
UKAWA ili haki ya wananchi ipatikane, hivyo
atumie busara kufanya hivyo kwa kuwa ndiye
baba wa taifa hili.
"Kuna kauli za viongozi wa CCM kuwa
wanataka kutawala milele... sasa mimi nasema
sawa tu wafanye hivyo, lakini kwa kwenda na
haki na siyo kwa kulazimisha kama ilivyo sasa
katika suala la katiba... hivyo ni katiba ya
wananchi wote wa Tanzania ambao wamo
vyama vya siasa na wasiokuwemo," alisema.
Askofu Kabobe alisema katika kujikweza kuwa
hajahusika kuvuruga, Rais Kikwete,
amewatumia vibaya viongozi wa dini aliodai
wanaegemea upande wa CCM kuwataka
waombee mchakato wa katiba na kuwataka
UKAWA warudi bungeni, huku akijua
watumishi hao wanapaswa kufanya kazi isiyo
na upendeleo.
"Daima nitasimama katika kweli nayo
itaniweka huru, hapa nasema wazi kwamba
Rais Kikwete ameamua kuwatumia vibaya
viongozi wa dini... nao wakaona bora
watumike ili kupata mkate na chai Ikulu
ambayo majani yake ni ya hapahapa nchini,
tena Mufindi, siyo dhahabu, wanachoendelea
kukifanya kwa wanachi ni unafiki wala siyo
maombi.
"Nilidhani Rais Kikwete atawaambia viongozi
hao wamwombee yeye aliyevuruga mchakato
huu na siyo kuuombea mchakato wa katiba
na amani... mimi najua nchi yetu ina amani
na amani itavurugwa na hao
wanaong'ang'ania hoja zao, kwani katika hili
gumzo la katiba linaloendelea mtu mjinga tu
ndiye atakayewalaumu UKAWA.
"Nawaomba viongozi wa dini wasijikombe
kombe Ikulu maana wao wanamwakilisha
Mungu... siogopi kusema kwa sasa hakuna
ninachokosa hapa duniani wala sitaki
kupendwa na rais, nitafanya yampendezayo
Mungu," alisema.
Huku akirudia rudia neno lake kwamba "sema
ukweli ili uwe huru", Askofu Kakobe alisema
anawaunga mkono UKAWA kwa hatua yao
waliyofikia hadi sasa hadi hapo Rais Kikwete
atakapoomba radhi na kukubali wakajadili
rasimu ya wananchi, kama watarudi bila
makubaliano hayo, basi watakuwa
wamerogwa.
"Nawaunga mkono UKAWA asilimia 100 kwa
100 na ninawaongeza 50 kwa hatua yao...
sasa warudi kwa kauli ya rais kukiri mbele ya
wananchi kuwa amekosea, anajirekebisha ili
wajadili rasimu ya katiba, wasipofanya hivyo
basi watakuwa wamerogwa... hakuna
maridhiano hapo maana nimefuatilia na
kubaini mazungumzo yanayoendelea
yamejawa unafiki.
"Kuwaunga mkono UKAWA kwangu si kwamba
nashabikia chama kimojawapo kinachounda
umoja huo hapana... nazungumza kama baba
wa kiroho mwenye kuwachunga watoto wengi
wenye vyama vyote vya siasa ambavyo vipo
nchini, ambao wanajua kwamba ninasimamia
ukweli tupu," alisema.