CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO; JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI
TAMKO KUHUSU KUONDOKA KWA WALIOKUWA VIONGOZI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kigoma Kaskazini
tunapenda kutoa taarifa kwa umma kutokana na sintofahamu inayotaka
kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu uimara wa chama chetu mkoani
Kigoma.
Tangu jana na leo kumeenea taarifa zinazowahusu watu watatu, Jaffari
Kasisiko, Msafiri Wamarwa na Mama Malunga Masoud, ambao vyombo
mbalimbali vya habari vimeandika kuwa wamehama chama chetu cha CHADEMA
na kukimbilia wanakojua wao (maana CCM inafanya kazi zake katika sura
mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;
1. Kwanza watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama
ngazi ya mkoa, kwa uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi
cha muda mrefu sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika
mkoa mzima wa Kigoma ili kiweze kukimbizana na wenzetu wa maeneo
mengine nchi nzima. Badala yake walikikumbatia na kukiatamia chama.
Wakati maeneo mengine wenzetu wakiongeza wabunge majimboni, Kigoma
chini ya uongozi wao ikauza majimbo.
2. Tunaweza kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache
ambao tunajua wako mbioni kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa ni
sawa na KOTI LILILOTUBANA. Kwa muda wao wote wa uongozi hawakuwahi
kufanya kazi yoyote ya kioganazesheni na kukieneza chama mkoa mzima.
Wao walikuwa watu wa mikutano ya hapa na pale Kigoma mjini pekee au
pale ambapo kunakuwa na uongozi wa kitaifa au wabunge.
3. Kwa muda mrefu saa wamekuwa viongozi 'waliotubana' kwa sababu
walifanya kazi kwa kuangalia zaidi maslahi yao. Sasa kuondoka kwao, ni
nafuu kwa chama. Pia ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa
wanachama makamanda waaminifu na watiifu waliofungiwa milango kwa muda
mrefu, kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa imani kubwa ya
kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge.
4. Upo ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi
hao na wengine wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine,
wamekuwa wakilalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa
maslahi na maelekezo ya CCM.
5. Katika madai yao ya kuhama chama watu hao wamesema wamefikia
hatua hiyo eti kutokana na chama chetu kuwa cha kibabe eti kwa sababu
tu Zitto Kabwe alivuliwa nafasi Naibu Katibu Mkuu ndani ya chama!
6. Madai hayo yanashangaza kwa sababu mbali ya chama kuwa na
sababu nzito za kumvua Zitto (na wenzake akina Kitila Mkumbo na Samson
Mwigamba) cheo hicho kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu, pia
tunaamini hakuna mwanaCHADEMA amejiunga na chama hiki kwa ajili ya
cheo. Ndani ya chama chetu tunaamini katika kugawana majukumu si vyeo.
7. Katika hali ya kushangaza zaidi wanasema eti Zitto amezuiwa
kugombea uenyekiti. Sasa tunajiuliza hiyo nia ya kugombea ambayo
hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa kufuata katiba, kanuni, maadili,
miongozo na itifaki za chama, waliambizana wao wenyewe na mtu wao?
Lakini kwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari
Kasisiko analipa fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya
nchi.
8. Ninaomba kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa wilaya na majimbo
ya Kasulu Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu,
Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini, tukutane kwa ajili ya
kikao cha Baraza la Mashauriano la Mkoa ili sasa tuchukue hatua
zingine za muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha chama chetu kwa
kuwaondoa vibaraka na wasaliti wote waliosalia.
9. Pia tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia
kiingilie kwa kutumia kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha
kuendelea kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua
hatua hiyo kupitia Baraza la Mashauriano.
10. Sisi wa CHADEMA Kigoma Kaskazini tunawataka wale wengine
waliosalia katika mkakati huo wa kuhamisha watu wachache lakini kwa
makundi ili eti kujenga taswira ya CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi
kadhaa wa Kanda wasisubiri. Chama chetu kitajengwa na watu wenye imani
watakaoweka maslahi na matakwa ya wananchi mbele kwa kuzingatia
misingi yetu kama inavyoelezwa katika Katiba ya Chama, kanuni, maadili
na miongozo.
Kwa niaba ya Wanachadema imara na makamanda watiifu na waaminifu kwa
mabadiliko yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge, naomba
kutoa taarifa hii.
Ally Kisala
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma
0 Comments:
Post a Comment