WATANZANIA wametakiwa kubadilika kifikira na kimtazamo
kwa kutoa kipaumbele katika kuchangia fedha kwenye kusaidia mambo ya msingi
kwenye jamii hasa elimu na kuondokana na kasumba mbaya ya kutumia mamilioni ya
fedha kuchangia sherehe hasa harusi.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mdau wa Elimu, Samwel
Shami wakati akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jeremba Munasa vitabu 200
na madaftari 1,800 kwa ajili ya shule za msingi Moivaro, Maroroni na Kikatiti.
Alisema kuwa Watanzania wamekuwa wepesi katika kuchangia
sherehe huku wakishindwa kuchangia katika kuboresha elimu kwa kutoaa walau
vitendea kazi ikiwemo madaftari, vitabu vya kiada na ziada.
Shami alisema kuwa amevutika kutoa msaada huo ili
kuwahamasisha wananchi wengine kuunganisha nguvu na serikali katika kuhakikisha
watoto wanapatiwa elimu bora kwani anaamini ndiyo silaha pekee ya ukombozi kwa
jamii yoyote.
Alisema kuwa anatarajia kuendelea na zoezi hilo la
kusaidia kutoa vifaa vya elimu kulingana na uwezo atakaokuwa nao ambapo
anatazamia kupanua wigo zaidi kwa kuangalia uwezekano wa kutoa motisha kwa
walimu ili waweze kufundisha vizuri zaidi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya, Munasa alimpongeza Shami kwa msaada huo aliodai kuwa utasaidia kuboresha elimu na kufikiwa kwa malengo ya matokeo makubwa sasa (BRN).
Alimuomba aangalie uwezekano wa kusaidia walau kupatikana
kwa maabara moja ya masomo ya sayansi itakayotumiwa na wanafunzi katika mafunzo
ya vitendo ambapo inaweza kutumiwa na wanafunzi wa shule zaidi ya moja.
Munasa alisema kuwa anaamini mdau huyo wa elimu ataangalia
uwezekano wa kuwapatia kompyuta 10 ambazo mbali na kuzipelekeka kwenye sekta ya
elimu lakini pia zitasaidia wilaya hiyo katika zoezi la upimaji wa viwanja.
Aliwapongeza wakazi wa wilaya hiyo katika kuandisha watoto
kujiunga na elimu ya msingi ambapo aliwataka kuhakikisha na wale wanaomaliza
elimu ya msingi wanajiunga na elimu ya sekondari kwenye shule walizopangiwa.
Munasa alisema kuwa kama wazazi wanawapeleka watoto hao
kwenye shule binafsi ni vema wakatoa taarifa mapema ili kuiwezesha idara ya
elimu kufuatilia kama kweli watoto hao wako shule na si wazazi wamedanganya kwa
lengo la kuwakatisha masomo.


0 Comments:
Post a Comment