WAKATI mawakili wa serikali wakikana kushikilia magari saba ya wakili maarufu jijini hapa, Mediun Mwale hali iliyoilazimu mahakama ya hakimu mkazi Arusha kumuamuru meneja wa TRA mkoani kuyarejesha magari hayo kwa mshitakiwa huyo baada ya kubainika kuwa yalichukuliwa kinyume cha sheria , Jeshi la polisi limeyakamata tena kwa madai kuwa yanachunguzwa.
Hali hiyo ilijitokeza jumanne majira ya saa 11 jioni wakati watu waliopewa nguvu ya kisheria na Mwale walipokuwa wakitoa kwenye lango kuu la TRA moja ya magari hayo aina ya Toyota Chaser yenye namba za usajili T 660 BCG ambapo walizuia na askari wakiwataka kuyapeleka makao makuu ya polisi mkoani hapa.
Akieleza sababu ya kuzuia gari hilo, mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Arusha, (OC CID) Faustine Mafwele alisema kuwa magari hayo wanayahitaji polisi kwa ajili ya uchunguzi wa kesi nyingine inayomkabili Mwale ambayo hata hivyo hakutaka kuielezea kwa undani zaidi ya kudai kuwa bado haijafikishwa mahakamani.
Hata hivyo magari mengine yalishindikana kuwaka kutokana na betri zake kutofanya kazi kwa kuwa yamehifadhiwa bila kutumika kwa muda mrefu hali iliyowalazimu ndugu wa Mwale pamoja na mafundi kuahirisha zoezi hilo mpaka jumatano ambapo yalipowaka waliyahamishia kwenye makao makuu ya polisi.
Utata juu ya kushikiliwa kwa magari haya uliibuka mahakamani wakati wakili Mwale ambaye yupo rumande katika gereza kuu la Mkoa wa Arusha la Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana, alitoa malalamiko mahakamani hapo Desemba 20 mwaka jana na kumtaja ofisa mmoja wa Polisi, Selemani Nyakulinga, kwamba alifika nyumbani kwake akiwa na wenzake na kuchukua magari hayo bila amri ya mahakama.
Aliieleza mahakama kuwa baada ya magari hayo kuchukuliwa yalipelekwa ofisi ya TRA Mkoa wa Arusha bila kuwapo sababu za kilichopelekea magari hayo kukamatwa, hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa amri ya kuachiwa kwani yalikamatwa kinyume cha kifungu namba 28 cha sheria ya kudhibiti fedha chafu na kifungu namba 24 cha Sheria ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Februari 22 mwaka huu upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili mkuu wa Serikali,Vertas Mlay ulitoa utetezi wake kwa barua, ambapo uliieleza mahakama kwamba magari hayo hayakuchukuliwa na Polisi bali na maofisa wa TRA kuhusiana na masuala ya kodi.
Alisema kuwa kuwapo kwa maofisa wa polisi wakati wa zoezi hilo kusimfanye mshitakiwa kudhani kuwa ndio waliochukua magari hayo bali walisimamia uchukuaji. Alijitetea kuwa gari namba T 520 BBJ lilikabidhiwa kwa wakili wa mshitakiwa Agosti 18, 2011 na kuhusu simu za mshitakiwa alisema kuwa hazikurejeshwa kwake kwa sababu zilipelekwa kwenye kitengo cha polisi cha uchunguzi.
Baada ya kusikiliza pande zote mnamo mwezi machi, mwaka huu mahakama ya hakimu mkazi iliamuru kurudishwa nyumbani kwa mshitakiwa magari T 690 BEW aina ya Range Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS Cadillac Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa Novemba mosi pamoja na gari T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa Desemba 8, mwaka jana baada ya kubainika yalichukuliwa kinyume cha sheria .
Hakimu mkazi mfawidhi Charles Magesa aliwaaagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini , Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha kuyarudisha magari hayo na simu za mkononi baada ya kupitia ushahidi wa pande zote na kuridhika kuwa mamlaka hizo zilikamata magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act) pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya mwenendo wa kesi za jinai.
“Ukamataji huo ni kinyume cha sheria kutokana na kitendo cha upande wa mashitaka cha kukamata magari hayo, hivyo mahakama inaamuru kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa TRA nchini na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha ambao walihusika katika zoezi la ukamataji kuhakikisha wanayarudisha yote kwa mshitakiwa nyumbani kwake walikoyachukua,” alisema hakimu huyo wakati akisoma uamuzi wake huo.
Hata hivyo Hakimu Magesa katika hukumu yake hiyo aliileza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa aliitaarifa mahakama kwamba alituma ndugu zake TRA kuulizia kuhusu magari yake ambapo ndugu zake walitaarifiwa na maofisa wa TRA kwamba magari hayo yalikamatwa kwa maagizo ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) E.S.A. Mmari, kwa barua yake ya Desemba 15, mwaka jana na ndugu wa mshitakiwa walipatiwa nakala ya barua hiyo.
Aliongeza kuwa ni muhimu kuelewa awali kabla kwamba mshitakiwa bado ni mtuhumiwa tu na mtu asiye na hatia hadi hapo itakapothibitishwa vinginevyo na upande wa mashitaka, hivyo anapaswa kutendewa kama mshitakiwa na si kama mtu aliyetiwa hatiani.
“Hoja kubwa ni kwamba magari yake pamoja na ya marafiki zake yamekamatwa na kuchukuliwa bila kuzingatia sheria, na makosa ambayo mshitakiwa ameshitakiwa nayo yapo chini ya sheria ya udhibiti wa fedha chafu ya 2006 na kifungu namba 28 cha sheria hiyo kinaeleza kwamba utaratibu wa kukamata, ukusanyaji taarifa, utaifishaji au ukamataji na udhibiti wa mali utakuwa kama ulivyo chini ya sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act & The Criminal Procedure Act 1991).
“Sheria hiyo ya matunda ya uhalifu ya mwaka 1991 inatoa utaratibu wa namna ya mali ya mtu aliyotiwa hatiani au aliyeshitakiwa na makosa yanayohusiana na sheria hiyo itakavyokamatwa…kifungu muhimu katika sheria hiyo ni kifungu namba 31 (1)” aliieleza mahakama.
Hata hivyo upande wa Jamhuri haukuridhika na uamuzi huo mdogo hivyo kuamua kukata rufaa mahakama kuu kanda ya Arusha ambapo waliomba kufanyiwa kwa marejeo kwa uamuzi huo ambapo waligonga mwamba kutokana na jaji aliyesikiliza shauri hilo , Kakusulo Sambo kukubailiana na pingamizi zilizowasilishwa Mwale akipinga hatua hiyo ya Jamhuri kwani kisheria uamuzi mdogo ndani ya kesi ambao haumalizi shauri lililopo mahakamani hauwezi kufanyiwa marejeo na walikosea kunukuu vipengele vya sheria walivyotumia kupeleka maombi hayo mbele yake.
Baada ya maombi hayo kutupwa na jalada kurudi kwa hakimu mkazi mfawidhi Magesa kwa utekelezaji wa uamuzi huo mawaliki wakuu wa serikali Fredrick Manyanda na Neema Ngowi waliibua hoja ya kutokuwa na imani na hakimu kwa madai kuwa shitakiwa ana ofisi ya uwakili Arusha inayomfanya awe na mahusiano ya kikazi na kibinafsi na hakimu huyo hivyo kumtaka ajitoe .
Hakimu magesa aligoma kujitoa kwenye shauri hilo kwa madai kuwa hoja zilizotolewa na mawakili wa serikali si za kisheria kwani hakimu hawezi kutakiwa kujitoa kwenye shauri kwa kuwa mshitakiwa ana kesi kwenye eneo ambalo ana ofisi jambo alilosema kuwa mawakili hao wa serikali walipaswa kutoa ushahidi unaoonyesha anauhusiano wa kibinafsi au atanufaika vipi na uamuzi alioutoa ili aweze kujitoa.
Hata hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilidaiwa kukiuka sheria kwa kuiandikia barua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani hapa kuzuia isitekeleze amri halali ya mahakama iliyowaagiza kumrejeshea Mwale magari yake kwa madai kuwa suala hilo linasubiri uamuzi wa mahakama hiyo Juni 20, mwaka huu jambo ambalo halikuwa kweli.
Akitoa uamuzi wake wa kutojitoa kwenye shauri hilo pia aliagiza kutekelezwa mara moja kwa amri ya mahakama ya kutaka mashitakiwa arejeshewe magari hayo huku akiutaka upande wa serikali kuacha kuchelewesha kesi hiyo kwa kisingizio kuwa wanasubiri nyaraka kutoka Marekani kwa madai kuwa suala hilo limechukua muda mrefu kama vile nchi hiyo iko kwenye sayari nyingine.
Aliwataka mawakili wakuu hao wa serikali ambao hawakuwa mahakamani hapo kuelewa kuwa walipa kodi wa nchi hii hawapendi fedha zao zitumike vibaya kama wanavyofanya kwani kila siku ya kesi huwalazimu kusafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha hivyo akawataka kuwa makini tofauti na siku hiyo ambapo hawakutoa taarifa kama hawatakuwepo wala hawakutuma mwakilishi.
Hata hivyo juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda kwani alipofuatwa ofisini kwake majira ya saa tano asubuhi muda uliotengwa na ofisi yake kwa ajili ya kukutana na wanahabari hakupatikana kwa kile katibu muhtasari wake alichoeleza kuwa ameelekea kwenye kikao kwa mkuu wa mkoa na alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani ilipokelewa na mlinzi wake aliyejibu kuwa bosi wake huyo yuko kwenye kikao hivyo atafutwe baadaye.
0 Comments:
Post a Comment