UMATI mkubwa wa watu umejitokeza kwenye mahakama ya hakimu mkazi mkoani Arusha kufuatilia kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo inayowakabili watu sita wakiwemo wenyeviti wawili wa vitongoji kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wengi wa watu hao walikuwa wamevaa mavazi yanayovaliwa na wanachama na wafuasi wa Chadema aina ya magwanda pamoja na kofia na skafu zenye rangi za chama hicho walionekana wakiwa wamekaa kwenye makundi mpaka pale karandika la polisi lilipoingia kwenye viwanja hivyo majira ya saa nne asubuhi.
Baadhi ya watu hao akiwemo mjane wa marehemu Mwambo, Eunice walitokwa machozi ya uchungu baada ya kuwaona watuhumiwa hao wakishuka kwenye karandika hilo wakielekea kwenye chumba cha mahabusu kilichopo kwenye mahakama hiyo ambapo hali ya ulinzi ilikuwa imeimarishwa na askari polisi waliokuwa na silaha.
Shauri hilo la mauaji namba 184 la mwaka huu lilifika mhakamani hapo kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Arnold Kirekiano ambapo limeahirishwa mpaka Julai 2, mwaka huu baada ya wakili wa serikali , Diaz Makule kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi haujakamilika.
Washitakiwa kwenye shauri hilo ni wenyeviti wa serikali na vitongoji vitongoji vyao kwenye mabano , Davis Mkumba ( Kisambaramajengo) na Mathias Nathan( Magadini) ambapo washitakiwa wengine ni Said Florian, Swalihina Yohana, Mohamed Shaban na Samwel Joseph.
Awali iliodaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja mnamo April 27, mwaka huu majira ya saa tatu usiku wakiwa maeneo ya mtaa wa Mji Mwema .kata ya Usa river wilayani Arumeru walimuua Mwambo ambapo hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mauaji.
0 Comments:
Post a Comment