Katika hatua ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametangaza rasmi kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini ifikapo Juni 20, 2025.
Akitoa tamko hilo jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa alisema kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, kifungu cha 84A, pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 178A. Kupitia vifungu hivyo, alieleza kuwa tayari amesaini notisi mbili muhimu za kuvunjwa kwa mabaraza hayo.
Aliweka wazi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Halmashauri, ndiye atakayewajibika iwapo mabaraza yataendelea kufanya vikao kinyume na notisi hizo.
"Kufanya kitendo hicho, Mtendaji Mkuu wa Halmashauri atapaswa kuwajibika, kwa kuwa Rais anatarajiwa kulivunja Bunge Juni 27, 2025, hivyo mabaraza yote ya madiwani yanapaswa kuvunjwa rasmi ifikapo Juni 20, 2025," alisisitiza.
Waziri Mchengerwa pia alitoa ufafanuzi kuhusu hatua zitakazofuata baada ya kuvunjwa kwa mabaraza hayo. Alisema kuwa kamati zote za Halmashauri zitasitishwa rasmi kuanzia Juni 20, 2025 hadi pale uchaguzi mpya wa madiwani utakapofanyika.
"Masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiwa na wakuu wa idara kama wajumbe wa kamati," alisema Mchengerwa.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hatakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi mapya makubwa kama vile kuanzisha miradi au uwekezaji mpya, wala kubadilisha miradi, uwekezaji au maamuzi yaliyopitishwa kabla ya kuvunjwa kwa mabaraza.
Waziri Mchengerwa aliwaasa wananchi, viongozi wa Serikali na watendaji wote wa Halmashauri kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki cha mpito kwa kuzingatia utawala bora, maadili ya utumishi wa umma pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kwa mujibu wa ratiba, uchaguzi mpya wa madiwani utafanyika sambamba na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba 2025. Hadi kipindi hicho kitakapofika, Halmashauri zote nchini zitaongozwa kwa mujibu wa utaratibu wa mpito ulioelekezwa.


0 Comments:
Post a Comment