Kampala, Uganda – Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, ambaye amekuwa katika mgomo wa kula kwa zaidi ya wiki moja, amekimbizwa hospitali baada ya afya yake kudhoofika.
Kwa mujibu wa taarifa za Mbunge Francis Mwijukye, Besigye alipelekwa kwenye kliniki ya Bugolobi chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya dola. "Besigye amehamishiwa Bugolobi Clinic jioni hii. Hali yake sio nzuri," aliandika Mwijukye kwenye mtandao wa X.
Kituo cha televisheni cha NTV pia kiliripoti kuhusu tukio hilo, kikieleza kuwa "hali ya afya ya Besigye ilizorota na hivyo kuhitaji matibabu ya haraka, huku usalama ukiimarishwa katika hospitali anakotibiwa."
Besigye, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, amekuwa kizuizini tangu Novemba mwaka jana katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala. Wanasheria wake wanasema alitekwa nyara nchini Kenya na kusafirishwa kwa nguvu hadi Uganda, ambako alifunguliwa mashtaka ya kumiliki silaha kinyume cha sheria katika mahakama ya kijeshi.
Wakili wake, Erias Lukwago, alisema: "Besigye amekuwa akipinga kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi. Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi kwamba raia hawawezi kushtakiwa katika mahakama za kijeshi, lakini hadi sasa serikali bado haijatekeleza uamuzi huo."
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano wa Uganda, Chris Baryomunsi, alithibitisha kuwa serikali inachukua hatua za kuhamisha kesi hiyo. "Tunafanya kazi kuhakikisha kwamba kesi ya Besigye inahamishiwa mahakama ya kiraia kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama ya Juu," alisema Baryomunsi.
Hadi sasa, bado hakuna taarifa rasmi kuhusu hali ya afya ya Besigye baada ya kuhamishiwa hospitalini.
0 Comments:
Post a Comment