Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi leo ameongoza Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Arusha 2025 lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC), ambapo alisisitiza umuhimu wa mshikamano, usawa wa kijinsia na mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya taifa.
Katika hotuba yake, Dkt. Nchimbi alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni kielelezo hai cha uwezo wa wanawake katika uongozi na utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.
“Tunatambua Rais wetu ameweka historia si kwa sababu tu ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza taifa hili, bali kwa sababu ya mafanikio makubwa aliyoyafanikisha katika kipindi kifupi,” alisema Dkt. Nchimbi.
“Amekuwa sehemu ya Halmashauri Kuu ya CCM kwa zaidi ya miaka 20, amehudumu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, amekuwa Waziri, Makamu wa Rais na sasa Rais. Uzoefu huu unadhihirisha uwezo wa mwanamke katika uongozi wa taifa.”
Jukwaa hilo lenye kaulimbiu ya Safari ya Mwanamke Arusha 2025 lilikutanisha viongozi wa ngazi mbalimbali, wakiwemo waliowahi kuwa viongozi waandamizi wa serikali na chama.
Akina mama waliowahi kushika nafasi kubwa serikalini kama Anne Makinda, Dkt. Asha-Rose Migiro na Zakhia Meghji waliungana na wanawake vijana na wajasiriamali kujadili mafanikio, changamoto na mustakabali wa mwanamke katika jamii ya sasa.
Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa historia ya harakati za wanawake ni ndefu na ya kishujaa, na kwamba mchango wao hauwezi kupuuzwa.
“Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika harakati za kudai uhuru wa taifa hili. Wapo waliotajwa majina yao na wengine waliobaki kimya lakini walichangia kwa ujasiri mkubwa. Leo tunalipa heshima hiyo kwa kuendelea kuwatambua na kuwaamini,” alisema.
Akitazama hali ya kisiasa ndani ya Arusha, Katibu Mkuu huyo alionesha mfano wa mshikamano kwa kuwasalimia na kuwakumbatia kwa pamoja Paul Makonda na Mrisho Gambo, viongozi wawili wa CCM wanaotajwa kuwa na mvutano wa chini kwa chini kuhusu mustakabali wa uongozi wa Arusha Mjini.
Kitendo hicho kilipokelewa kwa vigelegele na shangwe kutoka kwa washiriki wa jukwaa hilo, likitafsiriwa kama ishara ya kuhimiza umoja na maridhiano ndani ya chama.
“Wanawake wa Tanzania wanatamani kuona viongozi wao wanashikamana, wanaheshimiana na wanaweka mbele ajenda ya maendeleo kuliko tofauti binafsi. Hii ni dhamira ya CCM – kusimamia amani, mshikamano na maendeleo kwa wote,” alisema Dkt. Nchimbi.
Katika tukio hilo, Paul Makonda alieleza sababu ya kuandaa jukwaa hilo, akisema alipata msukumo baada ya mazungumzo na Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Abeid Amani Karume.
“Nilizungumza na Mama Fatma Karume alipokuja Arusha na alinieleza historia ndefu ya wanawake waliopigania uhuru na kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Nikasema hili haliwezi kubaki ndani ya ofisi au familia, lazima wanawake wengine wajifunze kupitia jukwaa hili,” alisema Makonda.
Aidha, Makonda alitumia jukwaa hilo kuwaaga wananchi wa Arusha baada ya muda wake wa uongozi kama Mkuu wa Mkoa kufikia ukomo.
Aliwashukuru viongozi wa dini, wakuu wa wilaya na makundi mbalimbali kwa ushirikiano waliompa na kusema ataendelea kuenzi mema yote.
Kwa upande wake, Mama Anne Makinda alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kujiamini, kuungana na kushirikiana kwa karibu zaidi ili kufikia usawa wa kweli katika uongozi.
“Wanawake hawahitaji huruma, wanahitaji fursa. Tuna uwezo, tunahitaji tu kuaminika na kusaidiana,” alisema.
Jukwaa hilo liliambatana na maonyesho ya kazi za wanawake wajasiriamali kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha, na limeacha ujumbe mzito kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii ya sasa, huku CCM ikionekana kujitahidi kuonesha sura ya mshikamano, hata katikati ya mvutano wa kisiasa.
Kwa namna tukio hili lilivyohudhuriwa kwa wingi, sauti ya wanawake wa Arusha sasa siyo ya kuombwa nafasi — ni ya kushiriki kikamilifu katika mustakabali wa nchi yao.











0 Comments:
Post a Comment