Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameongoza mamia ya waombolezaji katika shughuli ya kutoa heshima za mwisho na mazishi ya Mzee Silvin Ibengwe Emmanuel Mongella, yaliyofanyika leo Jumamosi, tarehe 7 Juni 2025, katika Kijiji cha Kabusungu, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Mzee Mongella alikuwa mwenza wa mmoja wa viongozi waandamizi wastaafu nchini, Bi. Getrude Mongella, na baba mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella.
Mazishi hayo yalitanguliwa na ibada ya misa takatifu nyumbani kwa marehemu, ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Leonard Nkwande, huku mahubiri yakitolewa na Padri George Nzungu. Katika mahubiri yake, Padri Nzungu alieleza:
“Tunaaga siyo tu mwili wa mpendwa wetu, bali tunatoa heshima kwa maisha yake ya upendo, unyenyekevu na kujitolea kwa familia, jamii na taifa.”
Akizungumza kwa niaba ya Chama, Balozi Dkt. Nchimbi alieleza kusikitishwa na msiba huo akisema:
“Mzee Mongella alikuwa nguzo ya familia na mfano wa hekima katika jamii. Tunamkumbuka kwa busara zake na maono aliyokuwa nayo katika kulea kizazi cha viongozi waadilifu.”
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Jumuiya ya Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, alieleza:
“Tumeondokewa na mzee mwenye maono makubwa. Tunatoa pole kwa familia, hasa kwa mama Mongella ambaye amehudumu kwa uadilifu mkubwa kwa taifa hili.”
Shughuli hiyo ilihudhuriwa pia na mawaziri, viongozi waandamizi wa CCM na Serikali, wabunge, pamoja na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali.
Katika salamu zake za shukrani kwa niaba ya familia, John Mongella alisema:
“Kwa niaba ya familia yetu, tunawashukuru wote kwa kutufariji na kushiriki nasi katika kipindi hiki kigumu. Baba yetu alikuwa kielelezo chema kwetu na kwa wengi waliomfahamu.”
Maziko yamehitimishwa jioni hiyo hiyo katika makaburi ya familia kijijini Kabusungu, yakihudhuriwa na waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment