Sunday, June 8, 2025

TANAPA YANUFAIKA NA MAONESHO YA KARIBU-KILIFAIR KWA KUTANGAZA HIFADHI ZA KUSINI NA MAGHARIBI

 


Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) imenufaika kwa kiwango kikubwa kupitia maonesho ya kimataifa ya utalii ya KARIBU-KILIFAIR yanayofanyika jijini Arusha, kwa kutumia jukwaa hilo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi za Taifa, hasa zile za Nyanda za Juu Kusini na Magharibi mwa Tanzania.



Akizungumza katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Lyimo, alisema maonesho hayo yamekuwa na tija kubwa kwao katika kutangaza vivutio vya utalii na kutoa elimu kwa mawakala wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi.

"Tumekuwa na siku tatu kubwa za mafanikio katika sekta ya utalii ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii imeshiriki maonesho kikamilifu pamoja na shirika la hifadhi TANAPA. 


Tumeona kuna uwakilishaji mkubwa wa kuweza kuonyesha vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi zetu za Taifa Tanzania," alisema Jully Lyimo.


Aliongeza kuwa kupitia maonesho hayo, wamekutana na mawakala wengi waliokuwa na kiu ya kupata taarifa kuhusu vivutio vilivyopo, na wengine walionyesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya hifadhi hizo.

"Tumeuza na tumejikita sana kuuza hifadhi za Kusini na Magharibi ambazo kwa nafasi kubwa hazina watalii wengi wanaotembelea ingawa zina vivutio vingi. Watalii wake bado wanaendelea kukua na bado ni wachache ikilinganishwa na hizi hifadhi za Kaskazini," alieleza.



Alifafanua kuwa baadhi ya wageni walishangazwa na uwepo wa hifadhi kama Kitulo ambayo haijazoeleka kama kivutio maarufu, lakini ina upekee wake unaowavutia watalii, wakiwemo wanaopenda utalii wa wanyama na mimea.



"Kwa ujumla tumepata kuuza hifadhi zetu, wageni wengi walikuwa wanaulizia na kushangaa hifadhi ya Taifa ya Kitulo. Watu wanapenda kutembelea utalii wa wanyama na wangependa kujua hivyo, kupitia maonesho hayo wamepata elimu nzuri," alisema Jully.



Akizungumzia hifadhi ya Taifa ya Katavi, alisema eneo hilo lina vivutio vya kipekee pamoja na fursa kubwa za kiuchumi na uwekezaji ambazo sasa zimeanza kutambuliwa na mawakala mbalimbali wa utalii.



"Katavi ina vivutio vingi sana ambavyo ni vya kujivunia na ina fursa nyingi sana za kiuchumi na uwekezaji ambazo mawakala wameweza kuzijua na kuhasika kwenda kupeleka watalii upande huo wa hifadhi hizo," alisema.



Jully alisisitiza kuwa maonesho hayo yatachangia kuongeza idadi ya watalii kutoka Afrika Mashariki na hata sehemu nyingine duniani.

"Kwa kupitia kujitangaza huko, tunaamini watalii watakuja na kuongeza idadi kubwa ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi. Tunaamini pia kuwa wawekezaji wataongezeka kwa miaka inayoenda usoni kwani wengi wametamani kwenda kutembelea maeneo hayo," aliongeza.



Kwa upande wake, Askari wa Jeshi la Uhifadhi Daraja la Pili kutoka Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Sabo Lucas, alieleza kuwa hifadhi hiyo ni maarufu kwa kuwa na makundi makubwa ya viboko, nyati, tembo na simba.



"Ni hifadhi ambayo utaweza kumwona kiboko kirahisi kuliko hifadhi zingine zote hapa Tanzania. Tunawakaribisha wananchi kufika kwa wingi kujionea vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hiyo," alisema Lucas.



Naye Askari wa Uhifadhi kutoka Idara ya Utalii ya Hifadhi ya Taifa Burungi Chato, Emmanuel Nyundo, alisema hifadhi hiyo ina fursa nyingi za uwekezaji pamoja na vivutio vya kipekee.

"Tunawakaribisha kwani fursa za uwekezaji zipo nyingi sana. Hifadhi ni kubwa na ina vivutio vingi sana, ikiwemo maziwa ya kutosha pamoja na ziwa kubwa la Victoria ambapo sehemu ya ziwa hilo ipo ndani ya hifadhi. 



Ni vizuri wageni wakatembelea kwani wana vivutio vya kutosha na maeneo ya uwekezaji bado yapo," alisema Nyundo.

Kupitia ushiriki wa TANAPA katika maonesho haya, imekuwa wazi kuwa hifadhi za Kusini na Magharibi zinapokea mwanga mpya wa kitalii, huku fursa za uwekezaji zikiwa zimetangazwa kwa ufanisi mkubwa, jambo linalotarajiwa kuinua pato la taifa kupitia sekta ya utalii.

No comments:

Post a Comment