Serikali imetangaza kuwa utoaji wa Vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press Card) vya kidijitali utaanza rasmi wakati wowote kuanzia Mei 10, 2025, baada ya waandishi wa habari kuanza kujisajili kwenye mfumo wa TAI-Habari.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Sayu mkoani Shinyanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema kuwa mchakato wa utengenezaji wa vitambulisho hivyo umekamilika na sasa uko tayari kwa utekelezaji.
"Tuliwaahidi kwamba tunawaletea Press Card (Vitambulisho vya kidijitali), ninayo furaha kuwajulisha kwamba 'press card' hizi za kidijital mchakato umekamilika, ziko tayari kwa matumizi, siku saba kuanzia sasa mtaingia kwenye kiunganishi cha Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na utaomba kitambulisho..." alisema Msigwa.
Alifafanua kuwa waandishi wa habari wanapaswa kujisajili kupitia kiunganishi cha https://taihabari.jab.go.tz kwa kufuata maelekezo ya kujaza fomu rasmi ya maombi.
"Ombi langu kwenu Waandishi wa Habari mtambue kitambulisho hiki ni mali ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania…, hivyo ukipewa wewe ndiye utakayewajibika kwa lolote litakalofanyika kwa utambulisho wa kitambulisho hiki, siyo kitambulisho umekiacha huko, mtu amekichukua kaenda kufanya utapeli tutambaini kwa sababu sasa tutakuwa tunaweza kufuatilia kwa kupitia mfumo, tukibaini tutakupata wewe," aliongeza Msigwa.
Alisisitiza umuhimu wa kutunza kitambulisho hicho akisema, "Ninachowaomba kitunzeni kama mboni ya jicho, huu ndiyo utambulisho wenu wa kazi, muwe nacho mfukoni, usikiache hovyo hovyo."
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, alihimiza waandishi wa habari kujisajili kupitia Klabu za Waandishi wa Habari katika maeneo yao ili kurahisisha mchakato wa kupokea vitambulisho hivyo.
"Wakati wa kujisajili waandishi wa habari wanapaswa kuweka kwenye mfumo vyeti vilivyo halali na kwamba ikiwa mwandishi ataweka cheti cha kughushi, Bodi ya Ithibati itachukua hatua kali za kisheria kwa sababu hilo ni kosa la jinai," alisema Kipangula.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza uwajibikaji na utambulisho rasmi wa waandishi wa habari nchini kwa kutumia mfumo wa kidijitali unaosimamiwa na Bodi hiyo.


No comments:
Post a Comment