Lissu Kususia Chakula Akiwa Gerezani, Wakili Kibatala Alalamikia Kunyimwa Faragha na Kuingiliwa kwa Uhuru wa Mahakama
Wakili wa Tundu Lissu, Peter Kibatala, ametangaza kuwa mteja wake ameazimia kususia chakula akiwa gerezani katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, kama njia ya kushinikiza kutendeka kwa haki katika kesi ya uhaini na uchochezi inayomkabili mbele ya Mahakama ya Kisutu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Kibatala alisema: “Natoa taarifa rasmi kwa umma kwa niaba ya mteja wetu kwamba anaanza kususia chakula. Sio kwa sababu nyingine bali anataka haki itendeke. Tutatoa taarifa rasmi kuhusu siku hasa, lakini atasusa kula chakula kitakachomtokea yupo tayari, hatokula mpaka haki itendeke.”
Kwa mujibu wa Kibatala, licha ya Lissu kushitakiwa kwa kosa la uhaini lisilo na dhamana, bado anastahili kupata haki za msingi kisheria, ikiwa ni pamoja na kuonana kwa faragha na mawakili wake. Alisema kuwa haki hiyo imekuwa finyu kwao na kwamba walilazimika kutumia lugha ya Kiingereza ili maafisa wa magereza wasielewe mazungumzo yao.
“Misingi ya kawaida ya kuhudumia wafungwa iliyopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa inasema wafungwa wote watapewa nafasi ya kuwasiliana na mawakili au wasaidizi wao wa kisheria bila kuchelewa, magereza wana haki ya kushuhudia kinachotendeka lakini sio kusikiliza tunachoongea na mteja wetu,” alisema Kibatala.
Lissu alikamatwa wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma, mwezi Aprili mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara, na baadaye kusafirishwa hadi Dar es Salaam ambako anakabiliwa na mashtaka mawili, ikiwemo la uhaini, ambalo linamuweka gerezani akisubiri uamuzi unaotarajiwa kutolewa Mei 6, 2025.
Katika kile alichokiita “mtego wa kisheria,” Kibatala alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kuacha kutumia jukwaa la Bunge kuzungumzia kesi hiyo, akisema ni ukiukaji wa misingi ya uhuru wa Mahakama.
“Hamza Johari ulijinafasi bungeni kuzungumzia kesi ya Lissu, tukikujibu tutaitwa tumevunja maadili. Njoo barabarani au njoo mahakamani tukutane. Mimi sijawahi kukuona mahakamani kwenye kesi hizi. Unaleta hadithi ambazo hujazishuhudia, ni hearsay,” alisema Kibatala.
Aidha, alimkosoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, kwa kutoa kauli zinazotetea matumizi ya Mahakama Mtandao kabla uamuzi haujatolewa rasmi, akisema hatua hiyo ni sawa na kuilazimisha mahakama kutoa uamuzi fulani.
“Bashungwa na Johari wanajibu hoja zetu mahakamani kabla hata uamuzi haujatolewa... Bashungwa ametoka hadharani kusema Mahakama iliamua kutumia mtandao kwa sababu polisi walipata taarifa za kiintelijensia kuhusu CHADEMA kufanya fujo. Hii ni kusema kama Mahakama iko chini ya Jeshi la Polisi! Hivi tunamweka Hakimu Mhini kwenye nafasi gani?” alihoji Kibatala.
Kwa upande wake, Lissu kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), unaoendeshwa na msimamizi wake, ameeleza kuwa iwapo hatofikishwa mahakamani Mei 6, ataanza rasmi mgomo wa kula chakula.
Lissu na chama chake CHADEMA wapo katika kampeni ya kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, wakilitaja kama “no reforms no election,” kampeni ambayo tayari imefanyika katika mikoa kadhaa ya kanda ya kusini na Dar es Salaam.

No comments:
Post a Comment