Saturday, May 3, 2025

Serikali Yatenga Bilioni 23.18 Kuboresha Barabara na Vivuko Katika Hifadhi za Taifa

 

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 23.18 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 2,381.7 pamoja na vivuko 69 katika hifadhi mbalimbali za taifa nchini.



Akizungumza bungeni, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa watalii kwenye maeneo ya hifadhi.


"Miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa watalii itaendelea kuboreshwa kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa hapa nchini, kwa kutumia mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu ili kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inapitika wakati wote wa mwaka," alisema Kitandula.



Aliongeza kuwa maboresho hayo yanahusisha barabara, madaraja pamoja na viwanja vya ndege ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wageni na kukuza utalii nchini.



Katika hatua nyingine, Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya maendeleo ya KfW imekubali kutoa Euro 500,000 kwa ajili ya kugharamia usanifu na upembuzi yakinifu wa barabara yenye matumizi makubwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.



"Barabara hiyo inaunganisha Golini – Lango la Naabi – Seronera yenye urefu wa kilomita 68," alisema Kitandula, na kusisitiza kuwa mchango huo ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya ndani ya hifadhi na kuinua sekta ya utalii.




No comments:

Post a Comment