Sakata la madai ya kupigwa kwa Kiongozi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa limechukua sura mpya baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, kutoa tamko kali akilaani ukimya wa chama kuhusu tukio hilo.
Kupitia ukurasa wake wa X, Mrema ameonyesha masikitiko yake kwa namna ambavyo CHADEMA imejibu suala hilo, akibainisha mambo matano yanayomkwaza.
"Nimesikitishwa na taarifa hii ya chama, pamoja na kutolewa kwa kuchelewa sana, masikitio yangu yanatokana na mambo yafuatayo," ameandika Mrema kabla ya kufafanua hoja zake.
Akiendelea, amesema:
-
Kutolaaniwa kwa tukio la kupigwa kwa kiongozi huyo – Mrema amehoji kwa nini CHADEMA haikulaani kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na mwanaume, bali kikaita suala hilo "tuhuma zinazosambazwa mtandaoni."
-
Chama kutotoa pole kwa mgonjwa – Amehoji ni kwa nini CHADEMA hakijatoa pole kwa kiongozi huyo aliyepigwa, ilhali hutoa pole hata kwa viongozi wa CCM wanapopata majanga. "Huu uadui wa kushindwa kumpa pole kiongozi umeanza lini?" amehoji.
-
Kutishwa kwa mgonjwa na kuwekewa masharti – Mrema amekosoa kitendo cha chama hicho kumpangia mgonjwa nani anapaswa kumpa faraja na nani hapaswi, huku hakijaonyesha nia ya kusaidia matibabu yake.
-
Chama kinadai kinafanya uchunguzi lakini kinatoa vitisho – Ameeleza kuwa si busara kwa CHADEMA kusema kinachunguza jambo ambalo kinadai ni "tuhuma za mtandaoni" huku wakati huo huo kikimtishia mgonjwa.
-
Kauli za chama zinafanana na enzi za utawala wa Hayati Magufuli – Mrema amefananisha kauli za sasa za CHADEMA na zile zilizokuwa zinatolewa wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli, kuhusu kupotea kwa wanaharakati na wanachama wa upinzani kama Ben Saanane, Azory Gwanda na wengineo.
Akitamatisha kauli yake, Mrema amesema: "Nalaani kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na wanaume, huu ni ukatili wa kijinsia na unapaswa kupingwa na kila mtu mstaarabu bila kujali nani katendewa ukatili huo."
Ameongeza kuwa ukatili wa kijinsia hauna nafasi katika jamii na ni lazima kila mtu apinge bila kujali itikadi za kisiasa.
Mpaka sasa, CHADEMA haijatoa tamko lingine kufuatia kauli hiyo ya Mrema, huku sakata hili likizidi kuzua mijadala mitandaoni.
0 Comments:
Post a Comment