Baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumvua nafasi ya Uongozi Catherine Ruge, aliyekuwa Mkuu wa Dawati la Jinsia, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kupitia maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu, mwanasiasa huyo ameeleza kushangazwa na hatua zilizochukuliwa dhidi yake, akizieleza kama maamuzi yasiyofaa na yasiyozingatia misingi ya Katiba ya Chadema. Ruge amesisitiza kuwa wenye mamlaka ya kumuengua katika nafasi hiyo ni Kamati Kuu na si Mwenyekiti wa chama, akitolea mfano Ibara ya 6.2.3(b) ya Katiba ya Chadema.
"Mimi nilikuwa kiongozi na nafasi yangu iliidhinishwa na Kamati kuu ya Chadema na kwa mujibu wa Katiba ya Chama ibara ya 6.2.3 (b), Mamlaka ya utenguzi wa nafasi yangu ni Kamati kuu na sio Mwenyekiti wa chama, hivyo nilitegemea utaratibu wa kikatiba na kikanuni ungefuatwa," alisema Catherine Ruge, akielezea kutoridhishwa na hatua hiyo.
Ruge pia amekiri kushangazwa na hatua ya kuenguliwa kwake bila kupokea taarifa rasmi. Alifafanua kwamba alijulishwa kupitia ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, bila kueleza sababu za kuondolewa kwake na mashtaka ya kuhusika, jambo linalodaiwa kuwa ni kinyume na Katiba ya Chadema na haki za binadamu.
"Nimeshtushwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Chama Taifa ambaye pia ni Mwanasheria nguli kukiuka misingi ya Katiba ya Chama chetu na misingi ya haki za binadamu hasa haki ya kusikilizwa," aliongeza Catherine Ruge.
Katika taarifa hiyo, Ruge alielezea kuwa hatua za kinidhamu dhidi ya kiongozi yoyote ndani ya chama zinapaswa kufuatwa kwa mujibu wa kanuni ya Chama ya mwaka 2019, hasa Kanuni ya 6.5 inayotaka kutolewa kwa mashtaka na nafasi ya kusikilizwa.
"Kanuni ya Chama toleo la mwaka 2019 kanuni ya 6.5 imeweka pia utaratibu wa kumchukulia hatua mwanachama na Kiongozi yeyote ndani ya chama, mathalani kanuni inaweka utaratibu wazi wa kufuatwa wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu, mojawapo ni kuandikiwa mashtaka yako na kupewa nafasi ya kusikilizwa," alisema.
Catherine Ruge, maarufu kama Msubhati, ameenguliwa kutoka kwenye nafasi yake mnamo Aprili 5, 2025, siku moja baada ya kuchapishwa kwa waraka wa kundi linaloitwa G55 ambalo ameonekana kuwa mwanachama wake. Katika waraka huo, wanachama wa kundi hilo wakiungana na wengine waliokuwa watia nia ya ubunge katika uchaguzi wa 2020 na 2025, walijitokeza kupinga maamuzi ya Chadema Taifa ya kutoshiriki uchaguzi mkuu ujao.
Kundi hilo linahusisha viongozi wa Chadema wakiwemo Adv. John Mallya, John Mrema, na Julius Mwita, ambao walieleza wasiwasi wao kuhusu msimamo wa chama wa "No Reforms, No Election", wakisema kuwa upinzani wa Chadema katika uchaguzi unaweza kuwa hatari na kinyume na matakwa ya demokrasia.
Katika Waraka wao wa pamoja waliotuma kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, wanachama hao wamesema kuwa haitowezekana kuzuia uchaguzi mkuu ujao kwa Chadema kuwa nje ya uchaguzi huo.
"Kujaribu kuuzuia uchaguzi tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai. Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi na ni rahisi wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi kwenye vituo hasa katika majimbo na kata zenye kuelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote tukiwa nje," imesema sehemu ya waraka huo.
Viongozi wengine wa Chadema kama Adv. John Mallya na John Mrema wameendelea kutoa msimamo kwamba wadau wa demokrasia nchini wanaunga mkono madai ya mabadiliko, lakini wanahofia hatua ya kuzuia uchaguzi kwa kumaliza kushiriki.
"Uchunguzi na uchambuzi wetu unaonesha wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai yetu ya Reforms lakini wanasita kuunga mkono mpango kamili wa Chama chetu wa kuzuia uchaguzi kwani hali hiyo kwao inatafsiriwa kuwa karibu sawa na kufanya uasi au kuvunja katiba na sheria zilizopo licha ya ubaya wake. Kwa maneno mengine msisitizo wa kuzuia uchaguzi unaathiri au kupunguza kasi ya uungwaji mkono katika madai ya msingi ya reforms," imesema sehemu ya waraka huo.
Kwa upande mwingine, kuna mtazamo wa kutilia shaka kuhusu mpango huo wa kuzuia uchaguzi na madhara yake kwa Chadema katika muktadha wa demokrasia ya taifa. Madai ya kuzingatia misingi ya Katiba ya Chadema yanaonekana kuwa changamoto kuu kwa chama hicho, huku wanasiasa na wanachama wa chama wakitofautiana kuhusu mbinu bora za kufikia malengo yao ya kisiasa.
0 Comments:
Post a Comment