Lissu Awaambia Wananchi wa Mtama Kupigania Mabadiliko ya Mfumo wa Uchaguzi

 


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewataka wananchi wa jimbo la Mtama mkoani Lindi kupigania mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ili kuweza kuwa na ushindani huru na haki. Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani humo leo, katika mwendelezo wa ziara za chama hicho kuwaelimisha wananchi kuhusu kauli mbiu ya "no reforms, no election" (yaani bila mabadiliko hakuna uchaguzi), Lissu alisisitiza kwamba chama hicho hakiwezi kushiriki uchaguzi ambapo haki haitatendeki.



“Hatuogopi uchaguzi, mimi nimegombea tangu mwaka 1995, nilikuwa kijana mdogo nikiwa na miaka 27, nikafanyiwa rafu nikashindwa nikarudi tena, nikarudi tena, nikachaguliwa ubunge mwaka 2010,” alisema Lissu huku akionyesha uthubutu wake katika siasa za Tanzania.



Aliendelea kusema, “Nikafanya kazi ya ubunge miaka mitano, nikarudi mwaka 2015 nikachaguliwa mbunge tena, kwahiyo mtu anaesema hawa CHADEMA wanaogopa uchaguzi hebu fikiria haya.”



Lissu aliongeza kuwa CHADEMA inapigania mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kwa sababu hali iliyopo sasa haijawawezesha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa haki na wa uwazi. Alisisitiza kuwa bila mageuzi, siasa za nchi hiyo hazitakuwa na maana kwa wananchi kwani kila uchaguzi unakuwa na matatizo ya kisheria na kiutawala yanayozuia ushindani wa kweli.

Kwa upande mwingine, Lissu alikumbusha kuwa chama cha CHADEMA kimekuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia na haki za binadamu, na kuonyesha kwamba, kwa miaka mingi, chama hicho hakijaogopa kushiriki katika uchaguzi, hata pale ambapo walijua wazi kuwa kuna uwezekano wa kutofanya vyema kwa sababu ya udanganyifu au changamoto nyingine.

Aidha, Lissu aliwaambia wananchi kuwa mapambano ya kisiasa ni ya kudumu, na kwamba kila mtu anapaswa kujua kwamba uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa kujenga demokrasia ya kweli, ambayo itafaidi kila raia bila kujali itikadi za kisiasa.


0 Comments:

Post a Comment